Tuesday, September 6, 2011

JK aapa kuwatoa kafara wala rushwa


Rais Jakaya Kikwete
ASEMA WAMEMCHOSHA, ATAKAYEKAMATWA ATAKUWA MFANO, MAGUFULI ATEMA CHECHE
Patricia Kimelemeta
RAIS Jakaya Kikwete amesema ataanza kuchukua hatua kwa watendaji wakuu wa Serikali na wadau wa sekta ya ujenzi wenye tabia ya kuomba na kupokea rushwa wakati wa mchakato wa zabuni ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.Rais amesema hayo kipindi ambacho nchi inatikiswa na tuhuma nzito za ufisadi zinazohusisha vigogo mbalimbali serikalini wakiwamo baadhi kutoka Ikulu.

Katika kuthibitisha ukubwa wa tatizo hilo la rushwa na ufisadi nchini, Rais Kikwete akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya ujenzi Dar es Salaam jana alisema sekta hiyo nayo inanuka rushwa kutokana na baadhi yao kutoa fedha ili kupata kandarasi.

“Sasa hivi kila kona rushwa, ukienda barabarani polisi wanaomba rushwa, watendaji wakuu wa Serikali wanachukua rushwa na makandarasi nao wanatoa rushwa ili waweze kupata zabuni, ni tatizo, lazima tuikemee, itatufikisha kubaya,” alisema Rais Kikwete.
Mkuu huyo wa nchi katika kuonyesha ukubwa wa tatizo la rushwa  alisema: “Ukifika barabarani, trafiki anakusimamisha na kukulazimisha kuwasha ‘wipers’ hata kama hakuna mvua, kumbe ana malengo yake ya kutaka kukuomba rushwa, kuna tatizo.”

“Katika sekta ya ununuzi wa mali za umma ndiyo kabisa, wanaagiza mali za Serikali kwa kuongeza gharama, kuweka cha juu ili wakifanikiwa waweze kugawana huku wakifahamu kwamba fedha zinazotumika ni za Serikali. Lazima watendaji kama hao waangaliwe kwa umakini sana kwa sababu wanaweza kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.”

Alisema kutokana na hali hiyo, kila mmoja analo jukumu la kuhakikisha anabadilika na kuacha tabia ya kuomba au kuchukua rushwa kwa sababu tabia hiyo inachangia kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Rais Kikwete alisema kiongozi bora ni yule anayechukia rushwa na kufanya kazi zake kwa uadilifu na weledi na siyo kuendekeza tamaa na kuwaomba rushwa anaowatumikia.

Dk Magufuli atema cheche
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alimwagiza Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads) kuvunja Bodi ya Ununuzi ya Mali za Umma kwa sababu imejaa rushwa.Mbali na agizo hilo, Dk Magufuli pia aliziagiza bodi ya wahandisi, makandarasi na wasanifu majengo, kukagua miradi ya maendeleo inayofanywa katika halmashauri ili kuona kama imekidhi viwango vya ubora kulingana na gharama ya fedha zilizotumika.
“Ninaziagiza bodi hizi zote kukagua miradi ya maendeleo katika halmashauri kuangalia kama zinaendana na gharama halisi ili tuweze kuwachukulia hatua wakurugenzi na watendaji waliosimamia miradi hiyo,” alisema Magufuli.

Dk Magufuli alisema wakati umefika wa kuwachukulia hatua watendaji wanaoshindwa kuwajibika kwa mujibu wa sheria na kufanya wanavyojua wao.

“Naomba kwa ridhaa yako Mheshimiwa Rais, niache nifanye kazi yangu, hata kama watakuja ofisini kwako kuleta malalamiko wasikilize lakini waache, mimi nachapa kazi kama ulivyonikabidhi,” alisema Dk Magufuli.

Dk Magufuli alisema kutokana na hali hiyo, wadau wa sekta ya ujenzi wanapaswa kutimiza majukumu yao ili kuondoa adhabu zinazoweza kujitokeza.

Mwananchi

No comments: