ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 30, 2011

Kamati ya kumchimba Jairo yahoji mashahidi asilimia 55


Idadi ya mashahidi waliohojiwa na Kamati Teule ya Bunge inayochunguza tuhuma dhidi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ya kuingilia haki, kinga na madaraka ya Bunge na kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi, David Jairo, imeongezeka kutoka asilimia 50 hadi 55.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ramo Makani, aliliambia NIPASHE jana kuwa kati ya mashahidi hao, wamo pia vigogo mashuhuri.
“Tunaendelea vizuri,” alisema Makani.

Alipoulizwa kama tayari watu mashuhuri kama Luhanjo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utou, walikwisha kuhojiwa na kamati yake, alijibu: “Kama unataja watu wa karibu hiyo, tumeanza kuwahoji na tunaendelea.”
Hata hivyo, Makani, ambaye ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM), hakuwataja vigogo hao kwa vile taratibu za kazi za kamati yake hazimruhusu kufanya hivyo.
Alisema wanatarajia kukamilisha kazi katika muda waliopewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, na kwamba, kwa kiwango kikubwa hawatahitaji muda wa ziada.
Katika tuhuma hizo, Luhanjo anadaiwa kutamka mbele ya waandishi wa habari kwamba: “Alichofanya Jairo ni utaratibu wa kawaida kabisa ...na kama Jairo ataweza kuwashtaki waliomdhalilisha ni yeye tu.”
Miongoni mwa kazi za kamati hiyo, ni pamoja na kuchunguza sakata lote la kumsafisha Jairo dhidi ya tuhuma za kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwashawishi wabunge kupitisha bajeti ya wizara hiyo ya mwaka wa fedha wa 2011/2012, zinazomkabili.
Mbali na Makani, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo, ni Gosbert Blandes (Karagwe-CCM); Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema); Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF) na Martha Umbulla (Viti Maalum-CCM).
Kamati hiyo inafanya kazi kwa kuongozwa na hadidu za rejea tano; mojwapo ikiwa ni kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilishwa kwa uwasilishaji wa hotuba za bajeti za wizara bungeni.
CHANZO: NIPASHE

No comments: