Waziri Nahodha aibukia jimboni
Atafuta suluhu ya CCM, Chadema
Mbowe atoboa siri upigaji kura
Atafuta suluhu ya CCM, Chadema
Mbowe atoboa siri upigaji kura
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Esther Bulaya, ameliomba msamaha Jeshi la Polisi kwa kile kinachodaiwa kuwatukana askari wa jeshi hilo siku ya tukio la kurusha risasi lilihusisha vyama vya CCM na Chadema.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Kitengo cha Tathmni na Ufuatiliaji wa Jeshi la Polisi, Isaya Mngulu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha polisi cha Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora.
Bulaya anadaiwa kuwatukana polisi muda mfupi baada ya tukio la hilo ambalo CCM wanadai Mratibu wa Chadema wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga, Mwita Waitara, alirusha risasi ambazo mbali na kuvunja vioo vya magari mawili likiwemo la Bulaya, ilimjeruhi kada wa CCM.
Mungulu hakutaja wazi matusi yaliyotolewa na Bulaya, lakini alisema siku moja baada ya tukio hilo, mbunge huyo alikwenda katika kituo hicho cha polisi na kuomba radhi.
“Wimbo wetu wa maadili unasema uwe mvumilivu wakati wa hatari usemi wetu tunaouchukulia sasa hivi ni ukichokozwa usichokozeke. Hilo kwa kweli lilitokea, lakini kwetu kutukanwa matusi tunaona ni jambo la kawaida,” alisema Mungulu.
NAHODHA AHIMIZA KUVUMILIANA
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsa Vuai Nahodha, amesema serikali itatumia fedha zote ilizonazo kuwasaka watu wanne wanaotuhumiwa kummwagia tindikaji kada wa CCM, Mussa Tesha.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa mjini hapa jana. “Tutatumia kila uwezo tulionao na fedha tulizonazo kuhakikisha kuwa tunawapata watu wote wanne wanaotuhumiwa kummwagia tindikali kijana huyu,” alisema.
Alisema juzi alikwenda gerezani kumwona mtuhumiwa wa tindikali, George Salum, na alimwambia kuwa anayehusika ni George Nyati na sio yeye.
Hata hivyo, alisema kuwa alipata habari kuwa Tesha anaendelea vizuri hospitalini na anaweza kuona tena na hata asipoona, anawatambua watu waliommwagia tindikali.
Waziri Nahodha alisema wataitisha gwaride la utambuzi ili aweze kuwatambua waliotenda uhalifu huo.
Katika hatua nyingine, Nahodha alisema wapiga kura wa Igunga hawatafuti mfalme bali wanatafuta mbunge wa kuwawakilisha bungeni.
Alisema kutokana na kukithiri kwa taarifa za matukio ya kusikitisha na yenye kutia aibu yanayoendelea Igunga, amelazimika kwenda kujionea hali ilivyo na kuhakikisha hali inakuwa shwari na kila raia anapata haki yake ya kupiga kura.
“Napenda kuweka wazi kwa wanasiasa wenzangu kuwa hali hii haipendezi na inatia aibu Tanzania, lakini pia tukumbuke kuwa Tanzania ni muhimu kuliko sisi wanasiasa na vyama vyetu, sisi leo tupo kesho hatutakuwepo, lakini Tanzania hii itabaki hivi hivi,” alisema.
Alieleza kusikitishwa kwake na matukio ya kumwagiwa kwa mtu tindikali, kutumika kwa lugha za matusi zisizo na heshima na watu kujeruhiana kwa kupigana mapanga.
“Haya mambo yanasikitisha sana, Watanzania jamani ni wastaarabu sana na wako makini pia wana viongozi wanaoheshimika duniani kote, wanaujua ukweli na uongo wetu, uchafu na usafi wetu, tutumie maneno ya heshima, tuwaachie Watanzania wenyewe wafanye maamuzi ya busara,” alisema.
Nahodha ambaye awali alikutana na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Tabora, alisema yupo Igunga kwa ajili ya kusimamia suala zima la ulinzi na usalama na si kuipigia kampeni CCM.
Waziri huyo akimalizia mkutano huo, alisema hali hiyo ya mvurugano anaielewa na kwa kuwa pia yeye ametokea eneo lililokuwa na siasa kama hizo (Zanzibar), hivyo hali hiyo ya Igunga anaiona kama changamoto na alihimiza uvumilivu.
“Hii jamani ni siasa tu, lakini sote tukubali kuwa baba na mama yetu ni Tanzania, naamini iwapo mtaendelea na tabia ya kuzungumza kwa wazi, kamwe hakuwezi kutokea mifarakano,” alisema na kuahidi kuyafanyia kazi hoja zote zilizowasilishwa kwake.
Kuhusu suala la kudhalilishwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, alisema hakuna kiongozi ambaye hakosei hivyo inawezekana kiongozi huyo alikosea, lakini tatizo lilikuwa hazikutumika taratibu za kisheria kumwajibisha.
“Sisemi mimi Nahodha eti ni Waziri wa Mambo ya Ndani sikosei au Rais hakosei la hasha, DC kama binadamu inawezekana alikosea ila tukubali watu wanapokosea tutumie njia nzuri zaidi ili kujengeana heshima,” alisema.
Kuhusu uhamasa baina ya Chadema na CCM, alisema ni vyema wakajirudi na kutafuta mwafaka kwani wote wanatoka nchi moja ambayo ina mambo mengi yenye maslahi kwa vyama vyote viwili.
MWITA WAITARA WA CHADEMA
Katika mkutano huo, wawakilishi wa vyama walitoa madukuduku yao ambapo Mratibu wa kampeni wa Chadema, Mwita Waitara, alielezea suala la Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario, kuendesha mkutano wa serikali katika eneo la mkutano wa Chadema, ni kitendo cha kupanga mikakati ya kuisaidia CCM dhidi ya Chadema.
Aidha, alizungumzia suala la madai ya kutaka kutekwa kwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Easther Bulaya na kurushiwa risasi.
“Ninachosema mimi kuwe na usawa wa kushughulikia matukio ya uhalifu na mtu anapofanya kosa, ashughulikiwe kama yeye na chama kisihusishwe, kwa sasa hakuna ugomvi na polisi bali ugomvi uliopo ni wa makada wa CCM na Chadema hapa kuna uhasama,” alisema.
Waitara alitaka kuhakikishiwa juu ya kutokushiriki wa polisi katika mchakato wa kuchakachua kura kwa kuwa katika chaguzi zingine polisi wamekuwa wakihusishwa.
AKWILOMBE WA CCM
Naye kada wa CCM, Shaibu Akwilombe, aliomba ufikiriwe utaratibu mzuri kwa ajili ya watu wanaosubiri matokeo utakaoepusha vurugu kwa kuwa sheria iliyopo inasema mtu akipiga kura akae umbali wa mita 100 kutoka kituo cha kupiga kura jambo ambalo ni hatari iwapo watajikusanya wengi wakiwa na itikadi tofauti.
“Kituo kimoja kina wapiga kura 400, wote wakikaa umbali huo kulinda kura, kuna uwezekano wakafanya kampeni za kuzuia watu wasiende kupiga kura, jambo ambalo linaweza kusababisha vurugu, nashauri watu waondoke tu baada ya kupiga kura,” alisema.
Katibu wa CCM Wilaya ya Igunga, Neema Adam, alikiri kutokea kwa mfululizo wa matukio ya kujeruhiana, kuchaniana picha na mabango, lakini alikanusha matukio hayo kuhusishwa na CCM.
USALAMA KUIMARISHWA JUMAPILI
Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa kutakuwa na ulinzi na usalama wa kutosha siku ya kupiga kura Jumapili ijayo na kuwataka waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura wajitokeze kutumia haki yao hiyo ya msingi ya kuchagua mbunge wao.
Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi nchini, Paul Chagonja, alisema ni kosa kwa mtu yoyote kutumia uvumi, maneno ya uongo, hisia au visingizio vyenye lengo la kushawishi watu wengine kuacha kwenda kupiga kura.
“Ni kosa kushawishi au kuhamasisha watu wengine kukusanyika kwa dhamira ya kufanya vurugu, fujo katika kituo cha kupigia na kuhesabia kura au mahali popote,” alisema Chagonja.
Alisema jeshi hilo litahakikisha zoezi la upigaji kura linafanyika kwa uwazi kwa kushirikiana na maofisa wenye dhamana ya usimamizi wa uchaguzi, mawakala wa vyama vya siasa walioteuliwa na vyama vyao pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
MAWAKALA WAONYWA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imepiga marufuku mawakala wa vyama vya siasa kuorodhesha majina na namba za kadi za wapiga kura wakati wa zoezi la kupiga kura.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mwenyekiti wa Nec, Profesa Amon Chaligha, alipokutana na viongozi wa vyama vyote vya siasa vya mjini Igunga.
Vile vile, alipiga marufuku wagombea, vyama au wakala wa kupiga kampeni siku ya uchaguzi kwani mwisho wa kampeni ni siku moja kabla ya siku ya uchaguzi. Profesa Chaligha alisema watu wakishamaliza kupiga kura warudi nyumbani kwa vile vituoni watakuwepo mawakala wa vyama kusimamia taratibu zote za upigaji na kuhesabu kura.
LIPUMBA: CUF ITASHINDA
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, amesema kuwa ana imani kuwa chama chake kitashinda kwa asilimia kubwa kutokana na mgombea wao, Leopold Mahona, kukubalika katika Jimbo la Igunga. Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba alisema kuwa chama chake kimefanya kampeni za kutosha katika jimbo hilo na kwamba wanategemea kupata kura nyingi katika uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili.
Alisema kuwa kufanyika uchaguzi mdogo ndani ya mwaka mmoja baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu inaonyesha dhairi kuwa CCM hakina uwezo wa kuongoza nchi kwa kusababisha kuwepo na uchaguzi mwingine.
“CCM haina uwezo wala dira ya kuongoza nchi kwani hata mwaka haujamalizika toka Uchaguzi Mkuu kufanyika tayari wamesababisha kuwepo kwa uchaguzi mdogo wakati aliyeshinda alikuwa na afya njema, akili timamu na hana kesi yoyote ya jinai,” alisema.
Alisema uchaguzi wa Igunga ni ushahidi mwingine wa wazi kuwa CCM haipo makini na hawawezi kufanya mabadiliko katika taifa pindi wanapojiandaa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Mbowe atoa madai mazito MwenyekitiI wa Chadema, Freman Mbowe, ametoa shutuma nzito kuwa CCM kimeingiza karatasi za kura ambazo zimeshapigwa.
Mbowe alitoa madai hayo jana kwenye mikutano ya kampeni akisema karatasi hizo zimepelekwa wilayani Nzega ambako zimehifadhiwa katika nyumba ya kiongozi mmoja wa serikali zikisubiri kuingizwa Igunga.
Alibainisha kuwa Usalama wa Taifa wanahusika na mchezo huo mchafu ambao umelenga kuisaidia CCM ambayo hivi sasa mambo yanakiendea kombo.
“Tunazo taarifa kuwa CCM kwa kushirikiana na Usalama wa Taifa wameingiza masanduku ya karatasi za kupigia kura ambazo tayari zimeshampigia kura mgombea wao,”alisema.
“Haki ya Mungu safari hii hatutakubali kuchakachuliwa, wananchi msiwe na wasiwasi hakuna kura ya mtu itakayoibiwa, tumejipanga kisawa sawa, tutambapana nao mpaka kieleweke,” alisema
Aliongeza kuwa kama CCM na vyombo vya dola wataingiza masanduku ya kura hizo Chadema itawasha moto mkubwa ambao hautaweza kuzimika kirahisi.
Mbowe alisema usalama wa Taifa ndiyo wanaongoza kufanya mbinu haramu za wizi wa kura kwa lengo la kuhakikisha CCM inaendelea kutawala.
Alibainisha kuwa bila usalama wa taifa na polisi CCM haina uwezo wa kupambana na Chadema katika uchaguzi wowote ule
Naye Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Kansa Mohamed, alisema wamebaini kura hewa zinazotaka kuingizwa na CCM ni 13,000.
Mkuu wa Tathimini na Ufuatiliaji wa polisi, Isaya Mungullu alisema hajapata taarifa za kuwapo kwa kura hewa.
Mungullu alisema kuwa kama Chadema inajua kuna kura hewa zimeingizwa hapa nchini ni vema ikalipeleka suala hilo katika Tume ya Maadili ya Uchaguzi
Wakati huo huo, NIAPASHE ilishuhudia viongozi mbalimbali wa kiserikali wanapishana katika hoteli waliyofikia viongozi wa CCM, ya Peak.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario, saa 1:00 asubuhi akiwa kwenye na gari la serikali kwenye hoteli hiyo kwa kile kilichoonekana kuwepo kwa kikao cha faragha na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, na viongozi wengine wa chama hicho.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment