ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 20, 2011

Mapenzi ni ugonjwa wa moyo, ni asali inayotuliza moyo -4

NICHUKUE fursa hii kutoa pole kwa ndugu wote waliofikwa na maafa kwenye ajali ya Meli ya MV Spice Islanders, iliyochukua nafasi siku tisa zilizopita. Natoa pole kwa wote walionusurika lakini misukosuko ilikuwa mikubwa.

Inauma kupoteza ndugu tuliowapenda. Ni hasara kwa kila aliyenusurika kwa sababu hakuna aliyefanikiwa japo kunusuru mzigo aliokuwa nao. Wafanyabiashara wamepata hasara kubwa. Mungu ni sababu ya kila kitu ila wazembe lazima wawajibishwe.


Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi. Kama nilivyokwishaeleza katika matoleo matatu yaliyopita, usije ukaingia kwenye uhusiano ukidhani kila kitu ni chepesi. Unatakiwa kujipanga, halafu uwe mdadisi kisha upite njia inayostahili.

Ugumu mkubwa ambao upo kwenye mapenzi ni pale mtu anapotaka aoneshwe upendo kulingana na jinsi anavyopenda. Inapotokea anabaini tofauti kati ya anavyopenda na anavyopendwa inakuwa shida kubwa. Hataki kupenda zaidi, eti ataonekana wa bei nafuu.

Kila mtu anataka apendwe zaidi. Kwa nini wewe usiwe wa kwanza kujitoa kumpenda mwenzi wako kuliko yeye anavyokupenda? Ni mtihani mdogo lakini unawashinda wengi na kusababisha mvutano.

Uzoefu unaonesha kuwa watu wengi hawana imani na wenzi wao. Dosari ndogo inaweza kuwafanya wajenge imani kuwa wenzi wao hawawapendi. Kila mmoja analalamika kivyake. “Hanipendi kama mimi ninavyompenda.” Ugonjwa wa moyo huanza hapa.

Nimeshachambua mengi huko nyuma. Kwa nyongeza, leo nakutaka ujiulize maswali yafuatayo ili uepukane na ugonjwa wa moyo, badala yake, mapenzi kwako yawe asali inayotuliza moyo kwa asilimia 100.

*Tazama unavyojisikia pale unapopenda. Je, unapopenda unajisikia vizuri hata kama umpendaye hakupi upendo kama ulionao kwake? Je, kumpenda mtu, ni lazima naye akupende kwa kiwango hicho hicho? Kama ndivyo, ni kwa nini?

 *Unajisikia unapendwa hata kama mwenzi wako hayupo? Kama sivyo, ni kwa nini? Je, unajikubali na unaridhika kwa sifa ulizonazo?

*Unafanya vitu kwa ajili ya mpenzi wako? Hata kama hutaki kufanya, je unajitahidi kutekeleza ili kuliweka penzi lenu hai? Unafanya kwa ajili ya mapenzi yake na unahitaji kila unachofanya, naye akufanyie hivyo hivyo?

*Je, umewahi kumueleza mwenzi wako vitu ambavyo ukifanyiwa vinaweza kukufanya ujisikie kupendwa?  Amewahi kutekeleza vitu hivyo kwa ajili yako? Kama bado, umewahi kuvumilia na kumfundisha taratibu?

MNAFANANA?
Swali hili lipe uzito. Inawezekana kwenye maswali ya juu ukawa umevuka vizuri. Pamoja na hivyo, haioneshi kama kuna mambo ambayo wewe na mwenzi wako mnafanana. Kama hamuendi sawa, jifunze kumuelewa.

Unaamini katika sanaa, mwenzako anadatishwa na michezo. Unapenda kusoma vitabu na kutoka kwenye matembezi ya hapa na pale, lakini yeye anapenda kusafiri. Hata hivyo, unapaswa kuamini kwamba ndoa ni kujitoa muhanga.

Siyo sawa na kutoa na kuchukua. Inatakiwa uwe mwelewa, katika kuhakikisha mapenzi yenu yanafanikiwa, ni vizuri ukahifadhi mambo yako kisha ukaungana naye kwenye mambo yake. Baadaye utamfanya aungane nawe kwako taratibu.

Hilo litafanikiwa kama utaacha ubinafsi. Tabia ya kutaka upendwe zaidi ni kosa. Katika uhusiano hutakiwi kujifikiria wa kwanza. Wekeza upendo mkubwa, halafu umfanye naye akupende. Si kwa haraka, bali taratibu.

Kama kila unaloamini wewe yeye yupo mbali, jifunze mambo yake kwanza. Muelewe kisha mshirikishe yako. Leo ukimfanya ajue kwamba unapenda kuogelea, keshokutwa mpe lingine na umjulishe kuwa ungependa mwende pamoja.

Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishes.info

No comments: