ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 29, 2011

Sheikh auawa kinyama


Sheikh wa Msikiti wa Shamsiya, Haruna Mlala (39), uliopo katika mtaa wa Ibungilo Kirumba wilayani Ilemela jijini hapa, ameuawa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na majambazi usiku wa kuamkia jana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana saa 7:00, baada ya kundi la majambazi kuvamia nyumbani kwake na kuvunja mlango kisha wakaingia ndani na kuanza kumshambulia.
“Mara baada ya majambazi kuvunja mlango wa nyumba yake, waliingia ndani na kumkuta mtoto wake anajisomea. Walimuamuru awaonyeshe aliko baba yake na mara baada ya kuwaonyesha alikolala, majambazi wale walimuamuru Sheikh huyo kutoka chumbani na kumtaka atoe brief case (sanduku dogo) iliyokuwa na fedha,” alisema Kamanda Barlow.
Hata hivyo, Sheikh huyo hakuwa na sanduku hilo linaloaminika kuwa lilikuwa fedha, hali iliyowafanya majambazi hayo kushambulia na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda Barlow alisema baada ya kutenda unyama huo, majambazi hayo yalitoweka na Sheikh huyo alikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu, lakini alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo kabla ya kuanza kupatiwa matibabu.
Alisema kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Sheikh huyo alijaribu kupambana na majambazi hao, lakini walimzidi nguvu kutokana na majeraha ya kichwani na sehemu mbalimbali
za mwili aliyoyapata na kupoteza damu nyingi.
Aliongeza kuwa, Polisi inamshikilia mtu mmoja kuhusiana na tukio ambaye hakumtaja jina kwa maelezo kuwa uchunguzi unaweza kuvurugika.
Majambazi hao walifanikiwa kuiba simu moja aina ya Sumsung yenye thamani ya Sh. 85,000.
CHANZO: NIPASHE

No comments: