Friday, September 2, 2011

Ujue uongo mtamu kwenye uhusiano!

NIANZE kwa kuwapongeza Waislam wote nchini na dunia nzima kwa kumaliza salama funga ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan na sasa wameanza mwezi Shawwl. Hongereni maana mmemaliza kutimiza moja ya nguzo tano za imani yenu.

Hapana shaka mlitumia vizuri kipindi hicho kwa kuachana na mabaya na kufanya yale ambayo ni fahari kwa Mwenyezi Mungu muumba wa Mbingu na Nchi.
Naam! Idd imeisha salama salimini na mambo mengine yanaendelea kama kawaida.

Ndugu zangu, ni vyema kuendeleza yale mema yote ambayo mliyatenda katika mwezi uliopita, msiyaache na kusubiri tena mwakani. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunampenda Mungu, ambaye bila shaka atatulipa kila kilicho na heri.


Rafiki zangu, leo ni Ijumaa nyingine tena, tunakutana katika ukurasa wetu huu muhimu kwa ajili ya kuwekana sawa kuhusu mambo ya uhusiano na mapenzi. Weka ubongo wako tayari kupokea kitu kipya. Naamini baada ya kusoma kichwa cha mada hii hapo juu, kimekuchanganya kidogo.

Mwingine atakuwa anajiuliza: “Huyu Shaluwa vipi tena? Yaani kuna uongo mtamu katika mapenzi?”
Ni sahihi kujiuliza swali hilo, lakini nataka kukuhakikishia rafiki yangu, uongo mtamu upo, tena mtamu kuliko hata asali! Kwa kawaida uongo unakatazwa kuanzia kwenye mafundisho ya dini na hata katika jamii. Mtu muongo si mwaminifu. Hakubaliki.

Hata mwanasiasa ambaye ni muongo, wapiga kura wake hawamchagui tena atakaporudi mara ya pili; kwanini? Kwa sababu aliwaongopea. Hiyo ni kweli kabisa, lakini hapa katika Let’s Talk About Love nataka kukupa kitu kipya kabisa ambacho hujawahi kukipata mahali popote; uongo mtamu!

UONGO
Rafiki zangu, sitaki kueleweka vibaya katika hili lakini kama nilivyosema mwanzo, uongo ni kitu kizuri kwenye jamii. Mtu anayedanganya hakubaliki. Kwa tafsiri ya haraka, mwongo si mwaminifu.

Haaminiki kwa sababu ni rahisi kutunga mambo ambayo hayapo na akayatengenezea mazingira yakaonekana ni ya kweli. Huyu hafai hata kidogo. Lakini rafiki zangu, katika uhusiano upo uongo ambao unakubalika.

Nasema unakubalika maana una lengo la kutengeneza uhusiano, kuufanya uendelee kuwa na nguvu na si kuupoteza. Huo ndiyo uongo unaokubalika. Kabla sijaenda mbele zaidi hebu twende tukaone kwanza tofauti ya ungo mtamu na mchungu.

UONGO MCHUNGU
Haikubaliki hata mara moja kumdanganya mpenzi wako kuhusu taarifa zako muhimu. Nasema hivyo kwa sababu utakuta mwingine anafanya kazi mahali fulani, lakini kwa sababu ya kutaka ukubwa anadanganya kwamba anafanya kwenye taasisi fulani kubwa.
Kama mtakumbuka kisa cha Kabwela na Uledi, kwenye cheka na viigizo, Kabwela                                                       kamdanganya mkewe anafanya kazi ‘airpot’ kama mtu anayeruhusu ndege ziruke. Eti bila yeye kusaini ndege haiwezi kuanza safari!
Siku moja, mambo yameharibika ofisini, vyoo vyote vimeziba na hiyo ndiyo kazi ya Kabwela, kwa bahati mbaya siku hakufika ofisini, ikabidi rafiki yake anayeitwa Uledi aagizwe aende nyumbani kwake akamwite.

Uledi akafunga safari hadi kwa Kabwela, hakumkuta nyumbani, alikuwepo mkewe tu. Uledi bila kujua kwamba Kabwela alimdanganya mkewe kazi anayofanya ‘akaropoka’ kwamba Kabwela anahitajika ofisini kwa vile vyoo vyote vilikuwa vimeziba!

Aibu gani hiyo?
Siwezi kueleza kwa kirefu kisa hicho lakini mwisho wake ni kwamba, mwanamke alibeba kila kilicho chake na kuondoka kwa Kabwela, kisa? UONGO. Kama Kabwela angemwambia ukweli hata Uledi angesema nini, isingekuwa tatizo kwa mkewe maana angekuwa anafahamu kazi ya mumewe.

Wapo wanaodanganya wanatoka katika familia zenye uwezo mkubwa kifedha, huku wengine wakijipachika majina ya koo maarufu ili waheshimiwe na wapenzi wao, huo ni utumwa, mbaya zaidi kuna siku ukweli unajulikana halafu unabaki na aibu zako. Kuwa mkweli.

UONGO MTAMU
Naam! Upo uongo ambao unakubalika rafiki zangu. Unajua kuna baadhi ya mambo ukiyasema kwa usahihi kama yalivyo yanaweza kuleta athari kwenye uhusiano, ndiyo maana nimesema kwamba upo uongo mtamu.

Inawezekana umefanya kitu ambacho hakimpendezi mpenzi wako, ama kwa kujua au kutokujua, lakini baada ya kuhisi labda amegundua na kukuuliza, unakataa. Ukikubali kwa kitu ambacho hakipendi inaweza kusababisha penzi kuvunjika.

Unabaki kuwa uongo mtamu kwa sababu kwanza una lengo la kulinda penzi, lakini pia hauna madhara kwa mpenzi wako. Huo ndiyo uongo mtamu ninaouzungumzia hapa.

Natamani sana kuanza kukuchambulia huo uongo mtamu, lakini kutokana na ufinyu wa nafasi yangu, nakuomba sana univumilie hadi wiki ijayo tutakapozama kwa undani kuhusu uongo mtamu, USIKOSE!
Eid Mubarak!
www.globalpublishers.info

No comments: