Bendera ya CCM WAKATI kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Igunga zikikaribia kuanza, vyama vya CCM, Chadema na CUF vimeanza kukwaruzana vikigombea kutundika bendera za vyama vyao ili kutia hamasa kwa wananchi wakati kuelekea uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu.
Waandishi wa habari wa Mwananchi waliopo Igunga, walishuhudia mpambano wa vyama hivyo huku kila kimoja kikitaka kupandisha bendera za chama chake kwenye nguzo za umeme na maeneo mbalimbali ya viunga vya mji wa Igunga.
Vyama vya CCM, Chadema na CUF ndivyo ambavyo bendera zao zinaonekana kushamiri katika jimbo hilo, lakini kuanzia jana bendera za CCM zilionekana kuwa nyingi zaidi, huku kukiwa na madai kwamba ziliwekwa juzi usiku hasa katika sehemu ambazo kuna bendera za Chadema.
Chadema waishutumu CCM
Akizungumzia mchuano wa kuweka bendera za vyama vyao, mratibu wa kampeni za Chadema jimboni humo, Mwita Mwikwabe Waitara alidai kuwa, juzi CCM ilikuwa iking’oa bendera za Chadema na kuweka zake.
Bendera ya Chadema Waitara alisema alizungumza na Katibu wa CCM wilayani Igunga, Neema Adam ambaye alimweleza kwamba amemuagiza Meneja wa Tanesco ang’oe bendera za Chadema zilizopo kwenye nguzo za umeme na kuweka za CCM kwa kuwa chama hicho ndicho tawala.
“Saa mbili usiku jana (juzi) tukaona bendera za CCM zinawekwa na sisi tukaangalia kama watang’oa za kwetu na sisi tutang’oa za kwao,”alisema Waitara.
CCM yakana
Akizungumzia suala hilo, Neema alisema hawawezi kung’oa bendera za Chadema na kwamba viongozi wa chama hicho wanatapatapa wakijua kuwa hawatashinda uchaguzi mdogo jimboni humo.
“Sisi kwetu hawa (Chadema) ni wadogo sana na hawawezi kututishia, jimbo tutalichukua, bendera zao zipo na sisi zetu zipo, waache kutapatapa,”alisema Neema na kuongeza:
“Mimi kwanza unavyosema nimezungumza na meneja wa kampeni wa Chadema, kwanza simjui na sijawahi kuzungumza naye.”
SAU walia mchezo mchafu
Chama cha Sauti ya Umma (SAU), kimelalamikia mchezo mchafu ambao kinadai unafanywa na baadhi ya viongozi wa CCM katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mdogo wa Igunga.Kufuatia hali hiyo, SAU kimesema kinaandaa malalamiko rasmi ambayo kitayawasilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Akizungumza na ofisini kwake mjini Igunga jana, Katibu wa SAU wilaya hiyo, Shaaban Kirita alidai kuwa rushwa ya fedha imekuwa ikiwalenga vijana na kinamama jimboni humo.
Kirita alisema mbali na kupewa fedha, vijana wameelekezwa kujiorodhesha wakiwa na shahada zao kwa ahadi kwamba watapelekwa kambini kufundishwa kazi kisha kupewa ajira jambo ambalo alisema lengo ni kuwaondosha ili wasipige kura.
"Matukio hayo yapo wazi na Takukuru wanaona lakini hawachukui hatua zozote jambo ambalo linaweza kutufanya tukachukua hatua wenyewe," alisema Kirita na kuongeza kuwa mpango huo hivi sasa upo katika kata ya Mbutu.
Alisema tukio jingine ni lile la kumwagwa kwa kifusi cha kokoto katika mto Wembele uliopo eneo la Mbutu ambako kimsingi kunatakiwa kujengwa daraja jambo ambalo linaashiria kuwa hiyo ni rushwa.
Alisema kwa muda mefu wakazi wa Igunga na wilaya ya Meatu mkoa wa Shinyanga wanakabiliwa na kero ya kukosa daraja katika eneo hilo, hivyo kuhoji kwa nini kifusi hicho kiwekwe sasa?
"Unajua daraja llile ni kiungo muhimu baina ya Igunga na Meatu na kuna watu kadhaa wamewahi kupoteza maisha eneo lile wakati wa mvua wanapojaribu kuvuka kufuata huduma mbalimbali zikiwemo za matibabu mjini Igunga," alisema.
Kwa mujibu wa Kirita, serikali ya CCM haijawahi kushughulikia ujenzi wa daraja katika eneo hilo, lakini akasema anashangazwa na hatua za kumwaga kokoto katika kipindi hiki cha uchaguzi.Alisema ujenzi huo ni hadaa kwani mvua zikinyesha na maji kupita katika mto huo ni wazi kuwa kokoto zote zitasombwa na maji.
Alisema hata mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni ya watendaji wa vyombo mbalimbali vya serikali yanatia wasiwasi kwani huenda yakawa na lengo la kukibeba CCM ambayo ni wazi itapoteza jimbo hilo kwa SAU.
Msimamizi aonya
Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Igunga, Magayane Protus alikiri kupata tuhuma nyingi za kuwapo kwa vitendo vya rushwa na kwamba malalamiko yote yamewasilishwa ofisi ya Takukuru kwa hatua zaidi.
Tayari vyama vyote vinavyotarajia kushiriki uchaguzi huo vimekwishapata wagombea na hatua iliyopo sasa ni kujiandaa kwa kampeni kuelekea uchaguzi hapo Oktoba mbili.
Mwananchi |
No comments:
Post a Comment