ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 19, 2011

Wabunge Chadema wahamishiwa Tabora


Wabunge wawili na mwanachama mmoja wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambao wanatuhumiwa kumshambualia Mkuu wa Wilaya Igunga, Fatuma Kimario,  juzi jioni walihamishiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Tabora, wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi waliokuwa wamebeba mabomu ya machozi na risasi za moto.
Wabunge hao ni Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylivester Kasumbayi, Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Kiwanga na Kaimu Kamanda wa Baraza la Vijana Taifa (Bavicha) Wilaya ya Igunga, Anwari Kashaga.

Wabunge hao pamoja na Kashaga, wanadaiwa kumfanyia shambulio la aibu Kimario,  katika Kijiji cha Isakamaliwa wilayani hapa Alhamisi iliyopita.
Kimario anadaiwa kutekwa katika Kijiji cha Isakamaliwa ambapo alidai alikwenda kwa ajili ya shughuli za kiserikali huku Chadema kikidai kuwa alikuwa akikipigia kampeni Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mkuu wa Kitengo cha ufuatiliaji na Tathmini wa Jeshi la Polisi nchini, Issaya Mungulu, alilithibitishia NIPASHE kuhamishwa kwa watu hao kwenda mjini Tabora kusubiri kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Tabora leo.
“Ni uamuzi tu tuliofanya  kutokana na mazingira ya hapa kutokuwa mazuri …tumewapeleka kule jana jioni na mashtaka watakayoshtakiwa nayo yanaandaliwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali,” alisema Mungulu.
Hata hivyo, alisema idadi ya watu waliokamatwa kutokana na tukio hilo haijaongezeka na kwamba bado ni watatu kama ilivyokuwa juzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Igunga, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lussu, alisema hakukuwa na sababu yoyote ya polisi kuhamishia kesi hiyo Tabora bali woga na hofu ya polisi ya kukabiliana na yeye mahakamani.
Alisema kitendo cha Jeshi la Polisi kuwapeleka viongozi waliokamatwa Tabora badala ya kuwafungulia mashtaka Igunga, kinadhihirisha ilivyo kawaida kwa jeshi hilo kujificha nyuma ya taarifa za kiitelejinsia kujaribu kuhalalisha kitendo hicho.
“Ni wazi kwa kila mwenye macho na kila mwenye kufikiria kwamba lengo halisi la kuwatoroshea viongozi wetu Tabora ni kuhakikisha kuwa hawapati msaada wa wakili pamoja na wadhamini ambao wangeupata kiurahisi kama wangeshtakiwa kati Mahakama ya Wilaya ya Igunga,” alisema.
Lissu alisema kisheria Mahakama ya Wilaya na hata Mahakama ya Mwanzo  ya Igunga, ina mamlaka ya kusikiliza kesi zinazohusu shambulio la aibu au wizi ambazo ndizo walizoelekezewa viongozi wao.
“Hakuna sababu yoyote ile ya kuwapakia kwenye gari kwa ulinzi mkubwa wa mabunduki  utafikiri ni majambazi na  kuwapeleka Tabora karibu kilomita 200 kutoka Igunga sababu pekee wanafikiria kuwa Tabora hakufikiki wakiwapeleka Tabora hawatapata wakili, hawatapata watu wa kuwadhamini wataendelea kusota mahabusu,”alisema na kuongeza kuwa:
“Jana usiku baada ya Katibu Mkuu wa chama chetu, Dk. Willibroad Slaa, kupata taarifa hizi amenielekeza leo (jana ) nilale Tabora na kesho (leo), nitakuwepo Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora ili kuhakikisha viongozi na mwanachama wetu wanapata ulinzi wote wa kisheria wanaostahili. Kama polisi wanafikiri hatuwezi kufika Tabora wamekosea sana, Tabora sio mbinguni, mimi sina uhakika wa kufika mbinguni nina uhakika wa kufika Tabora leo (jana),” alisema.
Kuhusu kukamatwa kwao, alisema viongozi wao walitumia mamlaka ya kisheria ya kumkamata mhalifu pindi anapomkuta akifanya uhalifu katika mazingira ambayo hayana polisi karibu.
“Mkuu wa Wilaya alikuwa anafanya uhalifu anaifanyia kampeni CCM. Viongozi wa dini, wazee maarufu wa vijiji akiwaeleza habari ya kampeni za uchaguzi Igunga katika eneo ambalo kwa mujibu wa ratiba ya NEC, Chadema walipaswa kuwa pale,” alisema.
Kwa upande wa kuvuliwa hijabu kwa Kimario, Lissu alisema kama nguo ilichanika wakati akikataa kudhibitiwa, basi sheria ya nchi inaruhusu kutumika kwa nguvu na kwamba kama anafikiri kuwa ana hoja wanamsubiri mahakamani.
“Kwa taarifa tulizo nazo sisi ni kwamba alijaribu kukataa kudhibitiwa na raia waliokuwa wakitimiza wajibu wao kisheria na kwa hiyo kama zinavyoruhusu sheria zetu, ilibidi `reasonable force', itumike kumdhibiti na kuhakikisha kuwa yuko chini ya ulinzi hadi hapo polisi watakapofika mahali pale,” alisema.
Alisema kuwa Kasulumbayi kama raia wa Tanzania, hakufanya kosa lolote kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kuhusu mkanganyiko wa ratiba ya mikutano ya kampeni, Lissu alisema ratiba wanayoitumia ni ile iliyoandaliwa na vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi na msimamizi wa uchaguzi na kwamba ndiyo iliyotumika Septemba 15, mwaka huu katika Kijiji Isakamaliwa.
Alipoulizwa kuhusiana na Jeshi la Polisi kudai kuwa muda waliopangiwa kuwa na mkutano ulikuwa kati ya saa 4:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana kulikuwa na ulinzi, Lissu alisema kuwa wanavyofahamu polisi walifika katika eneo hilo baada ya mkuu wa wilaya kudhibitiwa na kwamba wakati wa muda wa kampeni waliopangiwa kulikuwa hakuna ulinzi.
“Kama wanadai kuwa hatukutakiwa kuwa pale, DC (Mkuu wa Wilaya), alitakiwa kuwa pale, kuwa na mkutano pale wa kupokea fomu za maombi kuwa wasimamizi wa uchaguzi ndio kazi yake itakuwa vizuri hii kesi wasiifute, wasiwasi wangu ndio huo hawatathubutu kuonyesha pua zao mahakamani,” alisema.
Kuhusu chama hicho kufanya mkutano baada ya muda uliopo katika ratiba, Lissu alisema hakuna kifungu cha sheria ambacho kinachokataza chama kufanya mkutano katika eneo lolote lililopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iwapo wamechelewa kufanya hivyo katika muda uliopangwa na NEC.
“Sheria inasema hata mkigongana kwenye ratiba mnakaa mnazungumza, sio kosa la jinai kuchelewa kufanya mkutano, kama unafanya mkutano umekuta hakuna mtu mwingine umechelewa. Lakini sheria inasema ni marufuku mkuu wa wilaya, waziri, mkuu wa mikoa kutumia raslimali za serikali kufanya mkutano wa kampeni,” alisema.
Akizungumzia kuhusiana na hatua watakayochukua iwapo viongozi hao hawatafikishwa mahakamani leo, Lissu alisema itabidi na yeye wamuweke mahabusu.
“Watu wamekamatwa tangu jana asubuhi (juzi), sheria zetu zinasema wawe wamepelekwa mahakamani ndani ya saa 24, wamelala jana (juzi), watalala leo (jana), kesho (leo), wasipowapeleka mahakamani itabidi wanitafutie na mimi chumba cha kuniweka kwa sababu sitatoka kwenye kituo cha polisi mpaka watu wangu wapelekwe mahakamani,” alisema.
Kuhusu kupeleka malalamiko yao katika Balozi zilizopo nchini,  alisema utaratibu wa kuwasilisha malalamiko hayo ya jinsi CCM kinavyocheza rafu katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, unafanyika katika ofisi za makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Kada wa CCM abambwa na shahada za kura
Balozi wa nyumba kumi, katika Kijiji cha Mwayunge Mashariki,  Kata ya Igunga mkoani hapa Nghoboko Masele,  anadaiwa kukamatwa na vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwa na shahada ya kupigia kura na orodha ya majina ya wapiga kura pamoja na namba za shahada zisizo zake. 
Akizungumza na NIPASHE, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa la Chadema (Bavicha), John Heche, alisema kuwa balozi huyo alikamatwa jana asubuhi akiwa katika harakati za kuandikisha majina ya wapiga kura na namba za shahada zao. 
“Tumemkamata akiwa na orodha ya majina ya wapiga kura na namba za shahada zao zaidi ya 40 na tulipomhoji alisema kuwa ametumwa na Mwenyekiti wa CCM, wa Wilaya ya Igunga kuorodhesha majina hayo kazi ambayo wamepewa wenyeviti wa vitongoji wote wanaongoza kwa tiketi ya CCM,” alidai Heche. 
Alisema balozi huyo aliyekutwa akizunguka katika nyumba za watu kuorodhesha majina ya wapiga kura. 
“Alituambia kuwa anayekataa kufanya hivyo anamwambia hatapiga kura na hatapata chakula cha msaada kinachotolewa na serikali kwa ajili ya njaa,” alisema. 
Alipoulizwa Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Jeshi la Polisi, Isaya Mungulu, alisema kuwa yuko nje kidogo ya kituo cha Polisi na hana taarifa juu ya kukamatwa kwa balozi huyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: