ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 13, 2011

Huruma ya JK kwa waliomwua Kombe yazua mjadala


Waandishi Wetu
UAMUZI wa Rais Jakaya Kikwete kuwapunguzia adhabu, polisi wawili waliohukumiwa kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe, umezua mjadala mzito miongoni mwa watu wa kada tofauti katika jamii.

Wasomi, wanasiasa, wanaharakati na wadau mbalimbali waliozungumza na gazeti hili kwa njia tofauti jana, walitoa maoni yanayopingana; baadhi yao waliupinga na wengine kuunga mkono.

Wakati wanaoupinga wanasema Rais hakutenda haki kwa kuwa kuna wafungwa wengi magerezani wanaohitaji huruma yake, wakati wanaomunga mkono wanamshauri aweke wazi vigezo anavyotumia kutekeleza mpango huo ili kuondoa manung'uniko ya watu.



Mawakili kadhaa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, walisema jana kuwa, mazingira ya tukio hilo la mauaji ya Kombe, yanaweza kumshawishi Rais kuchukua uamuzi aliouchukua, lakini kwa siku za usoni ni vyema vigezo vya misamaha hiyo vikawekwa wazi na kufahamika.

“Unajua kiini cha mauaji yale kama ushahidi ulivyokuwa ni 'mistaken identity' (kumfananisha mtu ambaye siye) ni tofauti na mauaji ya makusudi. Mimi nafikiri kwa msingi huo, uamuzi wa Rais ni sahihi,”alisema wakili Peter Shayo.

Kombe aliuawa kwa kupigwa risasi nne kifuani Juni 30, 1996 baada ya polisi waliokuwa wakisaka gari aina ya Nissan Patrol,  mali ya W. Ladwa, kumfananisha na mtuhumiwa sugu wa wizi wa magari maarufu kama White.

Wakili Shayo ambaye ni miongoni mwa mawakili wa kwanza baada ya Uhuru, alisema mazingira ya tukio hilo ni kuwa polisi hao walikuwa wakisaka mwizi wa gari pamoja na gari ambapo njiani walikutana na gari linaloshabihiana na wanalolitafuta.

“Sasa kama ni kweli hayo ndiyo mazingira yaliyojitokeza katika tukio hilo, mimi naamini uamuzi wa Rais ya kupunguza ile adhabu na kuwa mauaji ya bila kukusudia, yanaweza kuwa sahihi,”alisema Shayo.

Wakili huyo alisema mazingira ya tukio la mauaji ya Kombe ni tofauti na mauaji ambayo mtu anamuua baba yake na kukata kichwa kisha kwenda kukiuza… akisema ukimsamehe mtu wa aina hii, kelele zitapigwa nchi nzima.

Hata hivyo, wanasheria wengine waliohojiwa na Mwananchi jana walisema japokuwa mamlaka hayo ya Rais yapo kikatiba, ni vyema kukawapo vigezo vya misamaha, vinginevyo wasaidizi wake wanaweza kutumia misamaha hiyo vibaya.

Kauli za wanaharakati

Kwa upande wake, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilipongeza hatua hiyo, kikieleza kuwa jambo hilo ni zuri kwa Serikali kutotekeleza adhabu ya kifo.

Mkurugenzi Mkuu wa LHRC, Francis Kiwanga alisema; “Tunampongeza kwa hatua hiyo kwa sababu Serikali inaelekea kusikia kilio chetu cha muda mrefu, siku zote tumekuwa tukitaka adhabu hii ifutwe.”
Hata hivyo, Kiwanga alisema kuwa, haitoshi kuachiliwa huru kwa watu hao wawili pekee, huku kukiwa na mamia wengine wamekaa gerezani kwa muda mrefu wakisubiri utekelezaji adhabu ya kifo.

“Ingawa tunamshukuru Rais kwa kuanza kusikia kilio chetu cha muda mrefu, tunataka iwekwe katika sheria kabisa kuwa, watu waliohukumiwa kifo, hukumu zao zibadilike na kuwa za kawaida,” alisema Kiwanga.
Alisema  kuwa kwa kiasi kikubwa Rais ametimiza wajibu wake kwa mujibu wa katiba na kwamba kilichobaki sasa ni nafasi ya wanaharakati kuhakikisha adhabu hiyo inafutwa kwenye vitabu vya sheria.

Alieleza kwamba, hatua ya kuandikwa kwa katiba mpya, ni moja ya nafasi nzuri zitakazowezesha kufutwa kwa adhabu hiyo.Mkurugenzo wa Mtendaji wa Kituo cha Taarifa kwa Wananchi (TCIB) Deus Kibamba alisema hatua ya kuwaachia watu wawili tu kati ya mamia inazusha maswali mengi.

“Mtu atajiuliza ni kwa nini hao wawili tu ndiyo wametoka, ni vigezo gani vilitumika kuwachagua wao tu?” alisema Kibamba.Alisema kuwa, hali hiyo ni matokeo ya Rais kuwa na madaraka makubwa kupita kiasi, yanayompa nafasi ya kupindua maamuzi yaliyotolewa na Mahakama.Hata hivyo, alisema hatua hiyo ni  ushindi kwa wanaharakati wa haki za binadamu ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakipinga adhabu hiyo.

Wananchi wengine
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila alisema anashangwa na uamuzi wa Rais kubatilisha hukumu ya kifo kwa askari polisi aliosema walimuua kwa makusudi Mkurugenzi huyo wa zamani wa Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Kombe.

Akizungumza na Mwananchi, Mtikila alisema kuwa hajui ni kwa misingi gani Rais Kikwete alitoa uamuzi huo.
“Ninachojua nafasi aliyopewa Rais ya kutoa msamaha kwa wafungwa kwa mujibu wa katiba ni kufanya hivyo kwa ajili ya manufaa ya Taifa. Sasa, sijui hapa Taifa limenufaika na nini kuuawa kwa Kombe?,”alihoji Mtikila.

Alisema hatua ya Rais inaonyesha ni jinsi gani nchi isivyo na utawala wa sheria na isivyojali katiba ya nchi, inayosema kuwa, kila mmoja ana haki mbele ya sheria na Serikali kupitia katiba yake italinda na kuziheshimu haki za raia na kuwahakikisha ulinzi na usalama.

Kwa upande mwingine, wananchi wa kawaida nao wamekuwa na maoni tofauti kuhusu uamuzi wa Rais Kikwete kuwaachia huru polisi hao aliohukumiwa adhabu ya kifo mwaka 1998.Kupitia mtandao wa gazeti hili wananchi hao wameeleza kusikitishwa na uamuzi huo, huku wengine wakitaka Rais Kikwete kuangalia wahukumiwa wa aina hiyo wenye umri mkubwa, ili awaachie huru.

Askari walioachiwa ni Koplo Juma Mswa na Konstebo Mataba Matiku, ambao walikuwa gerezani takriban kwa miaka 16, wamechiwa huru kufuatia huruma ya Rais Jakaya Kikwete ambaye alipunguza adhabu hiyo ya kifo, kuwa kifungo cha miaka miwili jela.

Katika maoni yake mmoja wa wananchi hao ameeleza kuwa msamiati wa 'kupunguza' umetumika vibaya kwani katika hali ya kawaida adhabu imeondolewa na siyo kupunguzwa.

Alieleza kuwa adhabu kwa askari hao ingekuwa imepunguzwa iwapo ingebadilishwa kuwa kifungo cha maisha.

Madaraka ya Rais
Madaraka ya Rais ya kumsamehe mtu yeyote aliyepatikana na hatia, yamo katika Ibara ya 15 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2008.

Ibara hiyo inatamka, ”bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Ibara hii ,Rais anaweza kutenda lolote ikiwamo kuibadilisha adhabu yeyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote ili iwe adhabu tahafifu”.

Akizungumza na Mwananchi juzi, mmoja wa askari hao walioachiwa huru Matiku Mataba alisema walitoka gerezani Mei mwaka huu walikokuwa wakisubiri kutekelezwa kwa adhabu yao ya kunyongwa baada ya Rais kuwaonea huruma na kuwapunguzia adhabu.

Baada ya polisi hao kupatikana na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kile Jaji Buxton Chipeta alichosema, “Uzembe wa hali ya juu”, mjane wa Kombe, Roselyne Kombe alifungua kesi ya madai dhidi ya Serikali.

Tangu Rais Kikwete aingie madarakani 2005, hajawahi kusaini hukumu yeyote ya kifo kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Benjamin Mkapa na hadi sasa zaidi ya watu 500 wanasubiri kunyongwa.

Habari imeandikwa na Daniel Mjema, Moshi, Boniface Meena, Joseph Zablon na Fredy Azzah, Dar.


Mwananchi

No comments: