ANGALIA LIVE NEWS
Thursday, October 13, 2011
Nape: Kuna kundi limeasi CCM
Joseph Zablon
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekiri kumeguka baada ya katibu wake wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kueleza kwamba, kumeibuka kundi la watu wenye nguvu ya pesa, wanaokisaliti chama kwa kuendesha propaganda za kupotosha dhana ya kujivua gamba.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam jana, Nape alisema kundi hilo linamhujumu pia Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, lakini akasema, chama kimejipanga kuwashughulikia wanaounda kundi hilo.
Alipotakiwa kutaja hujuma za kundi hilo dhidi ya mwenyekiti wa CCM, Nape alisema "Ni nyingi, moja ni kusambaza hoja ya kutaka nafasi ya urais itenganishwe na ile ya mwenyekiti wa chama."
“Wanafanya hujuma nyingi kwa mwenyekiti, lakini mojawapo ni hiyo ya kutaka kutenganishwa kwa kofia hizo mbili,” alisema Nape ambaye alisisitiza kuwa watu hao walianza kwa kuasi imani ya chama na sasa wanaendesha kampeni ya watu kuasi uamuzi halali wa vikao vya CCM.
"Juhudi hizi zimekuwa zikifanywa na kikundi kidogo sana cha watu wachache ambao kwa namna moja au nyingine wameathiriwa na mageuzi haya tunayoyafanya. Tatizo kakundi kenyewe kana nguvu kiasi ya pesa ndio maana kelele zao zinaonekana kuwa kubwa lakini, zisizo na mashiko," alisema Nape
Aliongeza: "Chama tunafahamu na kufuatilia kwa makini kila kinachoendelea, hakuna tusichokijua juu ya juhudi hizi na zingine nyingi, zikiwamo jitihada za kutaka kumhujumu hata Mwenyekiti mwenyewe (Rais Jakaya Kikwete). Nasistiza tunazifahamu."
Nape alisema kinachotokea Arusha hivi sasa kwa UVCCM ni sehemu ya mwendelezo ya usaliti kwa chama chake ambo alisema ulianzia Igunga wakati wa uchaguzi mdogo na kusisitiza kuwa wahusika wanajulikana na njama zao hizo zitashindwa.
Kauli ya Nape imekuja siku chache tangu Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Beno Malisa atoe kauli ya kukikosoa chama na Serikali yake akiwataka makada wa CCM kuacha kuingilia siasa za Chadema pia kuitaka Serikali itafute suluhu ya matatizo yanayokabili wananchi.
Malisa pia alitaka wote waliohusika na kuvunjwa kwa mkataba wa Dowans, wawajibike kutokana na kile alichokiita ni kulitia taifa hasara.
Lakini Nape jana alisema msimamo wa CCM katika suala la kuilipa Dowans uko wazi.
“Msimamo upo wazi na kilichofanywa na Tanesco kwenda mahakamani ndio msimamo wa Serikali ambayo ni ya chama kilichopo madarakani,” alisema.
Uchaguzi wa Igunga
Katika mkutano huo, Nape bila kuwataja wahusika alisema, juhudi za hivi karibuni za kundi hilo ni kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwashawishi baadhi ya makada ili wakisaliti chama ili kuuwezesha upinzani ushinde katika uchaguzi wa Igunga, ambao hata hivyo, mgombea wa CCM, Dk Dalaly Kafumu alishinda.
Alibainisha kuwa kundi hilo lilifanya hujuma kwa CCM katika uchaguzi huo na kwamba kauli mbiu yake ilikuwa, "Tushindwe, tuheshimiane".
Hata hivyo, alisema baada ya mkakati huo kushindwa, kundi hilo sasa linatumia watu tofauti kuimba "wimbo wa zamani".
Nape alisema ameamua kuweka wazi suala hilo ili kila mwanaCCM ajue kinachoendelea ndani ya chama hicho, akisisitiza kuwa wanalijua kundi hilo na njama zake na kwamba wahusika watashughulikiwa.
Alisema harakati za kundi hilo ni za muda mrefu na kwamba zilishika kasi baada ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kutoa uamuzi wa kuwataka baadhi ya makada wa chama hicho kujivua gamba.
Nape alisema nguvu za vyama vya upinzani zinazoonekana sasa zinatokana na wasaliti hao ndani ya CCM ambao wanatumia kila hila kuipotosha dhana ya kujivua gamba ambayo imepongezwa mara mara mbili na vikao vya NEC na hata UVCCM.
Katibu huyo wa Itikadi ya Uenezi alisema jitihada za kundi hilo zinachagizwa na uroho na ubinafsi ambao haujali maslahi ya chama kama taasisi na nchi kwa ujumla.
“Nashangaa kwa nini hawajitokezi na kuibua hoja zao hizo katika vikao halali, badala yake wanapitapita kugawa fedha na kuwatumia watu wengine kufanya hujuma na usaliti,” alilalamika Nape.
Alisema kundi hilo linapotosha dhana ya kujivua gamba ambayo iliungwa mkono na vikao vya NEC mara mbili na pia vikao vya UVCCM.
Kwa mujibu wa Nape, uamuzi wa NEC upo wazi, na ni ule ule uliyotangaza dhana ya kujivua gamba akisema hakuna kitakachobadilika.
Alisema anawashangaa wasaliti, kwani mabadiliko hayo yameanza kuzaa matunda kwa ushindi wa viti 17 kati ya 22 vya udiwani pamoja na ubunge Jimbo la Igunga.
“Sasa nawaeleza kuwa tumeshinda Igunga ili tuheshimiane na bahati mbaya kwao kwani walichotegemea sio kilichotokea, nawasihii wasiweweseke, watulie na kuyatafakari upya wayafanyayo huku wakikumbuka kuwa hakuna tusichokijua,” alisema Nape.
Nape aliwataka wana CCM kutulia na kuzipuuza jitihada za kundi hilo kwani mageuzi wanayoyafanya ndani ya chama ni kwa maslahi ya chama na nchi na kwamba harakati za kulinda raslimali za Taifa zilianza enzi za Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine.
Alisema kuwa atasimama kidete kuhakikisha ufisadi unatokomezwa kwa kuwa hata yeye siku moja hatakuwepo, lakini, vita hiyo vitaendelea.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment