
KATIKA toleo la wiki iliyopita, nilieleza mfano wa Pricilla ambaye aliachwa na Shauri katika hatua ambayo alikuwa ameshawekeza mapenzi makubwa kwake. Kilio cha mrembo huyo kinaweza kumtokea yeyote kwa sababu hakuna anayejua kesho. Makala haya lengo lake ni kutoa picha ili kubaini hatari ya baadaye.
Mantiki ni kuwa endapo utabaini dosari za mwenzi wako mapema, utaweza kujua wapi pa kushika. Muhimu kutambua ni kwamba mtu ambaye hana malengo na wewe ni rahisi kumjua kwa njia ya kumchunguza. Maswali utakayomuuliza, yatakuwezesha kujua hatima yako ipoje.
Mantiki ni kuwa endapo utabaini dosari za mwenzi wako mapema, utaweza kujua wapi pa kushika. Muhimu kutambua ni kwamba mtu ambaye hana malengo na wewe ni rahisi kumjua kwa njia ya kumchunguza. Maswali utakayomuuliza, yatakuwezesha kujua hatima yako ipoje.
UTAMBULISHO
Kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye hajakata shauri la kuyajenga maisha yake kuwa endelevu ni tatizo kubwa. Itakuumiza kichwa kuelewa msimamo wake, wakati mwenzako hata mshipa hautashtuka. Vema kulijua hilo na uanze kupambana kuanzia leo.
Namaanisha kuwa kabla ya kutafakari kama mwenzi wako ana malengo na wewe au kinyume chake, sharti ujue kuhusu dira ya maisha yake. Inawezekana hajawa tayari kuwa na mwenzi wa kudumu wa maisha yake, hivyo chukua hatua haraka iwezekanavyo.
Kama dira yake inasomeka, basi jambo la kufanyia kazi ni msimamo alionao kwako. Je, anataka muishie kuwa wapenzi tu au anakusudia kuingia na wewe kwenye ndoa? Nalo hilo ni jukumu ambalo unapaswa kufanyia kazi. Nakusisitiza uchukue hatua kulingana na matakwa yako.
Hana malengo ya kudumu na wewe, je nawe unapenda kupoteza muda? Vipi malengo yako kwake ni kuzugia au wewe umeshaanza safari ya kujenga maisha endelevu? Akili ipo kichwani kwa sababu haitakiwi baadaye ujute peke yako kwamba amekupotezea muda.
Kipimo kizuri cha awali kabisa kujua kuwa kama mwenzio ana malengo na wewe ni utambulisho. Je, anakutambulisha kwa familia yake? Ni kwa kiwango gani cha utambulisho? Inawezekana akakutambulisha, wewe ukadanganyika kumbe anakucheza shere.
Utambulisho wake ufanyie kazi. Je, ameshatambulisha wangapi kabla yako? Inawezekana familia yake imeshapokea wakwe wengi mpaka hawaoni uzito tena. Kuna familia nyingine zinalea vijana wao kwa misingi wanayoita ‘uzungu’ kwamba yupo huru kufanya chochote, wazazi hawajali.
Wazazi hawaoni kero kuletewa mtu leo wakiambiwa ni mkwe wao, baada ya miezi miwili wakaletewa mwingine tena. Aina hii ya watu ipo, kwa hiyo chambua mambo na uone wapi pa kushika. Usikimbie eti kwa sababu nyumbani kwao alishatambulisha watano, jiulize kwa nini hao aliachana nao?
Pengine wewe ndiye mwenye bahati baada ya kutofautiana na waliopita. Hawakuwa wake, ila wewe ndiye wa maisha yake. Hivyo, chekecha ubongo ili ujue hatima yako mapema. Usijirahisi au kulainika mapema, matokeo yake ukachezewa, mwisho ukaachwa na kuingizwa kwenye kapu la waliotambulishwa na kupigwa chini.
Jambo lingine ni kuwa usikubali utambulisho uishie kwa marafiki. Uhusiano wako na yeye, unapaswa kuwa rasmi. Mpeleke kwa wazazi wako naye akupeleke kwao. Baada ya hatua hiyo, wekeni hoja mezani za maisha yenu baada ya urafiki na uchumba. Je, mnaelewana? Basi vizuri sana.
Ikiwa hakuna maelewano. Anakupiga chenga kukutambulisha kwa wazazi wake. Pengine ameshakutambulisha lakini anarukaruka kila unapofungua mazungumzo kuhusu hatima yenu. Hataki mjadili ndoa, anafurahia mazungumzo ya kujirusha na ngono. Huyo ishi naye kwa machale.
VIPI MCHAKATO WA NDOA?
Pengine mmeshakubaliana kuhusu kufunga ndoa lakini vipi michakato? Anaratibu mambo kwa roho safi au anajivuta? Maisha ya ndoa hutawaliwa na matarajio ya furaha, kwa hiyo mhusika hutekeleza ratiba zilizo mbele yake bila kusukumwa. Muogope sana mtu ambaye mnakubaliana jambo kwa ajili ya maisha yenu lakini hatekelezi mpaka akikumbushwa.
Ndoa ni ya watu wawili wanaopendana na wameamua kwa moyo safi kuishi pamoja. Hii ina maana kuwa utekelezaji wa mipango ya ndoa, inatakiwa ifanywe na kila upande kwa shauku kubwa. Anayetegea aangaliwe upya. Je, ana kasoro za kujisahau na uvivu au bado anajishauri?
Kufunga ndoa ni wito, je, mwenzi wako anao? Kama ni mvivu au ana kasoro za kujisahau, unaweza kumhimiza ili muweze kwenda kulingana na ratiba lakini kama anajishauri, ni vizuri nawe ukatafakari kama ni sahihi kuingia kwenye maisha ya ndoa na mtu ambaye hayupo tayari. Mtu anayejishauri kufunga ndoa na wewe, maana yake hayupo tayari, bado anajiuliza.
Itakuja kukusumbua baadaye atakapolazimisha muachane kwa sababu hana cha kupoteza. Hakupendi kwa dhati na hakuingia kwenye ndoa kwa moyo mmoja. Hakikisha kuwa uliye naye leo, anakuhitaji pengine kuliko wewe. Mwenda pole hajikwai, mapenzi yanahitaji muda, siyo kwenda kwa pupa.
Kama umepitia kikamilifu tangu mwanzo, utakuwa umesoma kikamilifu tabia za mtu ambaye hana malengo na wewe. Hivyo, basi nitakuwa nimetii maombi ya wasomaji wangu wengi waliokuwa wananilalamikia kuwa hawawaelewi wapenzi wao kiasi kwamba wanahisi wanapotezewa muda.
Mimi na safu yangu hii, lengo kuu ni kukuweka uwe na moyo huru. Mapenzi yasikuvuruge akili, badala yake uwe ni mtu mwenye kuyafurahia kila siku.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake