
Kostadin Papic
YANGA imetangaza rasmi kuvunja mkataba na kocha wake Mganda Sam Timbe, hatua ambayo imetoa fursa kwa kocha wake wa zamani Kostadin Papic, kurejea kufundisha kikosi hicho cha jezi za Kijani na Njano.
Hatua hiyo ya Yanga imekamilisha taarifa zilizoonekana kuwa ni uvumi na kuzagaa karibu wiki nzima kuhusu kurejea Jangwani kwa Papic.
Papic raia wa Serbia, alijiondoa Yanga mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kutofatiana na viongozi wake, na nafasi yake kuchukuliwa na Timbe aliyeiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huo huo.
Mserbia huyo aliyewahi kufundisha baadhi ya vigogo vya soka Afrika, Ghana na Afrika Kusini, ameanza rasmi kazi jana lakini bila kupewa mkataba kama ilivyo kawaida.
Badala yake, Papic ataifundisha timu hiyo kwa makubaliano maalum ndani ya karatasi mpaka hapo baadaye.
Mtihani wa kwanza wa Papic utakuwa mechi ya kwanza msimu huu wa ligi dhidi mahasimu wao wakubwa Simba Jumamosi wiki inayofuata.
Katibu mkuu wa Yanga, Selestin Mwesigwa, alithibisha kuvunjwa kwa mkataba wa Timbe, na kwamba jambo muhimu linalofuata ni kumlika haki zake.
"Ni kweli mkataba na Timbe tumeuvunja rasmi, tunaandaa utaratibu wa kumlipa," alisema Mwesigwa kwenye mazoezi ya timu jana kwenye uwanja wa Kaunda.
Mwesigwa hakuwa tayari kwenda mbali kutoa sababu za kumtema Timbe, vile vile kuweka bayana kiini cha kumrejesha Papic aliyeondoka baada ya kushindwa kuelewana na uongozi wao.
Awali, Timbe alisema kama viongozi wa Yanga wataona hafai na kutaka kumuondoa, hasa shida, ila la msingi ni kulipwa haki zake za kuvunjwa mkataba.
"Nilichukua timu mwishoni mwa kumalizika msimu wa mwaka jana na kuipa ubingwa, lakini pia niliipa ubingwa wa Kombe la Kagame. Uzuri wa kocha ni matokeo ya uwanjani," alisema Timbe.
Habari zisizo rasmi toka ndani ya klabu hiyo zinadai kuwa, mabingwa Yanga watalazimika kumlipa Timbe si chini ya shs 50 milioni kwa kuvunja mkataba.
Akizungumza na Mwananchi jana kwenye mazoezi ya timu hiyo, Papic alisema amefurahishwa kurejea tena Yanga.
"Kama unavyoniona, nimeongena na uongozi wa Yanga na tumefikia makubaliano maalum, baada ya hapo tunaweza kuangalia suala la mkataba," alisema.
Alipoulizwa ilikuaje aliondoka Yanga kutokana na kushindwa kuelewana na uongozi, na ameamua kurudi tena viongozi wakiwa wale wale, alisema: "Mambo hubadilika, na sasa tuna makubaliano mengine na ndio maana sijasaini mkataba," alisema Papic.
Aidha, baadhi ya wachezaji waliohojiwa na Mwananchi kuhusu mabadiliko hayo bila kutaka majina yako kuandikwa gazetini, walisema ingawa si jukumu lao kuleya kocha, lakini ni uamuzi huo umewafurahisha.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake