
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira
HOJA kwamba mbio za urais wa mwaka 2015 ndizo zinazokigawa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ilidhihirika jana pale suala hilo lilipojitokeza katika vikao vya usuluhishi vya chama hicho vinavyoendelea mkoani Arusha.Vikao hivyo ni vile vinavyoendeshwa na mlezi wa chama hicho mkoani hapa, Stephen Wassira ambaye ameambatana na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigella wakisaka suluhu ya msuguano wa kisiasa ndani ya CCM ambao umekitikisa chama hicho tangu kutangazwa kwa mpango wa kujivua gamba.
Suala la mbio za urais jana liliibuka ndani ya kikao cha Baraza la Vijana Mkoa wa Arusha, lakini wajumbe wa kikao hicho wakaonywa kwamba “ni uhaini kuzungumzia urais wakati huu ambao Rais Jakaya Kikwete hajamaliza muda hata mwaka mmoja kati ya mitano ya awamu yake ya pili na ya mwisho ya uongozi”.
Wasira ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), juzi alianza mchakato wa vikao vinavyowashirikisha viongozi na baadhi ya makada wa chama hicho wa wilaya na mkoa wa Arusha, eneo ambalo limekuwa kitovu cha vurugu zinazoonekana kukitikisa CCM hadi ngazi ya taifa.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao cha jana zilisema, licha ya kuelezwa kuwa ni uhaini kuzungumzia nafasi hiyo kwa sasa, pia vijana hao waliambiwa kwamba hoja hiyo inatumiwa na watu wenye malengo binafsi kwa nia ya kuwagawa wana CCM.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho ambazo Mwananchi lilizipata zinadai kuwa mjumbe aliyetoa tahadhari hiyo ni mwenyekiti wa UVCCM, Wilaya ya Monduli, Julius Kalanga aliyesema kuwa wananchi wanapaswa kuwa makini na watu wanaoeneza hoja hiyo.
“Pengine hatuwezi kujua kwamba watu hawa tayari wamemwandaa mtu wao wanayepanga kumpenyeza kwa wapiga kura katika Uchaguzi Mkuu ujao,”chanzo chetu kilimnukuu Kalanga na kuongeza:.
"Watanzania wa sasa wako makini na uelewa wao ni mkubwa kuliko wengine wanavyodhani, hawatakuwa tayari kuletewa rais aliyefungwa na kubebwa kwenye kapu kwa faida na maslahi watu wachache wenye malengo binafsi".
Kalanga ni miongoni mwa vijana waliopewa onyo na halmashauri ya CCM Mkoa wa Arusha Juni mwaka huu, kwa madai ya kushiriki kwenye mgogoro uliowahusisha vijana wakiongozwa na mwenyekiti wao wa mkoa, James Ole Millya kwa upande mmoja na Katibu wa CCM Mkoa, Mary Chatanda kwa upande mwingine.
"Wanaoeneza propaganda za urais 2015 wanafanya hivyo kwa lengo la kupima upepo na kutugawa katika makundi ili waweze kututawala kifikra. Vijana kama jeshi na nguvu ya chama tunapaswa kusimama kidete kukabiliana na genge hili kwa maslahi ya chama na taifa kwa ujumla," alikaririwa Kalanga.
Busara za Wassira
Habari zaidi kutoka ndani ya kikao hicho kilichodumu kwa zaidi ya saa sita zilidokeza kuwa, busara za Wassira ziliwezesha makundi yanayopingana kufikia mwafaka kwa kupeana mikono.
Mapema Wassira aliwaambia vijana hao kwamba Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa taifa wa CCM angependa kuona wanachama wa chama hicho kikongwe wakipatana na kuwa na umoja ambao ndio siri ya mafanikio.
Kada huyo alinukuliwa akiwaasa vijana wanaolumbana kuondoa tofauti zao kwa kusameheana ili washirikiane kukijenga chama chao tayari kukabiliana na upinzani unaoendelea kupata nguvu kila kukicha huku wananchi wakionekana kuanza kukipa mgongo chama hicho tawala.
"Hakuna binadamu aliyekamilika, sote tuna mapungufu yetu. Muhimu kwa sasa ni kusameheana na kuweka pembeni tofauti zetu kwa maslahi ya chama. Tujenge chama chetu na hatuwezi kufikia malengo hayo bila kuwa na umoja," alikaririwa akiasa Wasira.
Kauli hiyo ilionekana kuzaa matunda kwani mwisho wa kikao hicho wajumbe walifikia mwafaka wa kupatana ambapo vijana waliokuwa wakihasimiana wakiwemo mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Arusha, Godfrey Mwalusamba na mtangulizi wake, Ally Bananga walipeana mikono kama ishara ya mapatano.
Mwalusamba pia alipatanishwa na kupeana mikono na bosi wake, Ole Millya huku katibu wa CCM Mkoa, Chatanda naye akitangaza msamaha kwa vijana wote waliokuwa wakiendesha kampeni za kumng'oa katika nafasi yake au kumwamisha kituo cha kazi.
Baada ya mapatano hayo, Wasira aliwapa jukumu vijana wa chama hicho kusaidia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi katika jimbo la Arumeru Mashariki linaloshikiliwa na Jeremiah Sumari anayekabiliwa na maradhi yanayomkwamisha kutekeleza ipasavyo majukumu yake.
Mbali na Wasira na Shigela, mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo na mbunge wa Viti Maalum (vijana), mkoa wa Arusha, Catherine Magige.
Kauli hiyo ya Wasira ambaye jana jioni alikutana na wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Arusha katika juhudi za kunusuru chama hicho na mpasuko,
Tuhuma za rushwa
Mapema zilizuka tuhuma kwamba baadhi ya wajumbe wa Baraza la Vijana wilayani Arusha, kudaiwa kuhongwa fedha kwa lengo la kuwachafua baadhi ya viongozi wa umoja huo mbele ya Wassira.
Vyanzo vya habari vilieleza kuwa fedha hizo zilitolewa na mmoja wa vigogo ndani ya CCM ngazi ya wilaya, siku moja kabla ya kutua kwa Wassira kwa lengo la kuwachafua viongozi wa UVCCM mkoani hapa.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, rushwa hiyo ilitolewa usiku wa Oktoba 25 mwaka huu kwa baadhi ya wajumbe ambao walipewa fedha hizo, ili wawataje baadhi ya viongozi kuwa chanzo cha mgogoro.
“Kuna kiongozi ngazi ya CCM wilaya alikuwa akitembea usiku wa kumkia jana na kapu la fedha, lengo lake lilikuwa ni kuwashawishi baadhi ya wajumbe wa baraza wawachafue viongozi wetu (anawataja) kuwa ndio chanzo cha mgogoro,” kilidokeza chanzo hicho.
Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare jana alikanusha tuhuma hizo na kuwataka waandishi wa habari kutookota maneno aliyoyaita kuwa ni ya barabarani.
Alisisitiza kuwa Wassira yupo Arusha kuangalia hali ya chama mkoani humo kwa kuwa yeye ni mlezi wake na sio kufuatilia migogoro.
“Hivi jamani kuna nini mnatafuta...acheni kuokota maneno ya barabarani bwana, Wassira ni mlezi wetu wa chama na amekuja kutuangalia sisi tunaendeleaje,”alisema.
Hata hivyo, wajumbe wawili wa Baraza la Wijana wilayani humo (majina tunayo) wanadaiwa kufurumusha makombora mazito ndani ya kikao cha juzi kwa wakituhumu viongozi wao kwamba ndio chanzo ya mgogoro mkoani hapa.
Mmoja wa vijana hao alinukuliwa akitoa kauli nzito mbele ya Wassira katika kikao cha juzi, akiwatuhumu baadhi ya viongozi kwamba wao ndio chanzo cha mgogoro unaofukuta huku akisisistiza kuwa wanaendeleza sera ya kutaka nchi na CCM visitawalike kwa maslahi yao binafsi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment