ANGALIA LIVE NEWS
Friday, October 28, 2011
Wafuasi CCM, Chadema wakwamisha kesi Arusha
Peter Saramba, Arusha
VURUGU zimeibuka jana mahakamani wakati wa kesi ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema baada ya wanachama, wapenzi na wafuasi wa vyama vya Chadema na CCM kukwamisha usikilizaji wa shauri hilo.
Kabla ya vurugu hizo kutokea wafuasi wa vyama hivyo waliingia kwa wingi na kujazana kwenye ukumbi na kusababisha hewa nzito.Wananchi walikaidi maombi ya askari polisi, Kaimu Msajili wa Wilaya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Charles Magesa na viongozi wa Chadema akiwamo Lema walisisitiza kuendelea kukaa ndani ya ukumbi huo uliokuwa umejaa kupita kiasi.
“Makamanda, pamoja na kwamba ni haki yenu kusikiliza kesi hii ambayo ni ya kwenu, Jaji hawezi kuingia na kuendelea na kesi kwa jinsi ukumbi ulivyojaa. Naomba waliokosa viti watoke nje ili kesi iendelee,” alisema Lema
Ombi hilo la Lema aliyekuwa akisaidiana na wakili wake, Method Kimomogoro kuwasihi waliozidi ukumbini watoke nje, lilikataliwa na waliokosa viti waliamua kuketi chini wakisisitiza hakuna hota mmoja wao aliyetoka nje.
“Katika hili kamanda utatusamehe sana. Hatoki mtu humo ndani hata mmoja. Kwanza Jaji aliagiza wafunge vipaza sauti ili tuliokosa nafasi ndani ya ukumbi wa mahakama tuweze kusikiliza mwenendo wa kesi tukiwa nje, lakini hadi leo msajili hajatekeleza,” alisema mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Chebeti
Kutokana na mvutano huo uliodumu kwa saa moja na nusu kuanzia Saa 5:00 mpaka Saa 6:30, wakili wa walalamikaji, Alute Mughwai aligoma kuingia mahakamani kuendelea na kesi akidai hakuna hewa na usalama wa kutosha huku Jaji Aloyce Mjuluzi anayesikiliza shauri hilo akiendelea kusubiri ofisini kwake taarifa za muafaka wa pande hizo mbili.
Baada ya juhudi za kuwashawishi wananchi hao kushindikana, Jaji Mjuluzi aliamua kuingia mahakamani na mawakili wote wa upande wa walalamikaji, waliomba kesi hiyo iairishwe mpaka leo ili kutoa nafasi ya kuwapo utaratibu mzuri utakaosaidia shauri hilo kuendelea.
“Mheshimiwa Jaji sisi upande wa walalamikaji tuko tayari kuendelea na shauri hili, lakini kama unavyoona, chumba chako cha mahakama hakiko tayari kwa jinsi watu walivyojaa, hata wateja wangu wako nje baada ya kukosa nafasi ya kukaa,” alisema Wakili Mughwai.
Kwa upande wake, wakili wa serikali, Angela Chacha alishauri mahakama itoe maelekezo yatakayohakikisha watu wanaingia ukumbini kulingana na uwezo na viti vilivyopo huku wakili Kimomogoro akiomba utekelezaji wa amri ya Jaji Mjuluzi ambaye alimuagiza msajili wa mahakama kufunga vipaza sauti ili watu waweze kufuatilia kesi hiyo.
Jaji Mjuluzi alikubaliana na maombi ya mawakili hao na kuahirisha kesi hiyo mpaka leo.Ukumbi huo una uwezo wa kuingiza watu 100 waliokaa kulingana na viti vilivyopo, lakini waliokuwapo jana walikuwa zaidi ya watu 500 ambao walikaa hadi kwenye korido huku baadhi wakiwa wamejazana milangoni na madirishani.
Hali hiyo iliwalazimisha waandishi wa habari ambao walikuwa miongoni mwa waliokosa nafasi kutoka nje kumpisha Jaji kuingia ndani na kufanya vivyo hivyo wakati alipotoka baada ya kuahirisha kesi hiyo.
Baada shauri hilo kuahirishwa, wananchi waliokuwa wakitoka mahakamani hapo kurejea mjini walisikika wakihamasishana kuwahi saa 12:00 asubuhi leo ili kupata fursa ya kuingia ukumbini huku wakionya kutokuwa tayari kuzuiwa labda mahakama ifunge vipaza sauti vitakavyowawezesha kusikiliza wakiwa nje.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment