ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 7, 2011

UTAENDELEA KULIA SABABU YA MAPENZI HADI LINI?

NAKUKARIBISHA kwa moyo mkunjufu katika safu yetu hii ambayo tunazungumza juu ya mapenzi. Sina neno rahisi la kukuambia zaidi ya kukuhakikishia kwamba utapata dawa ya tatizo lako la muda mrefu katika mada hii.

Unalia kila siku kwa sababu ya mapenzi? Unateswa, kunyanyaswa na kutukunwa? Kama ndivyo, ukweli ni kwamba wewe ni mtumwa bila kujijua. Upo katika utumwa wa mapenzi. Leo ni siku yako ya kutoka huko.

Rafiki zangu, uwanja wa mapenzi ni mpana sana, wakati mwingine unatakiwa kutumia akili na uwezo wako wa mwisho wa kufikiri ili uweze kung’amua ufanyacho kama ni sahihi au lah! 


Lakini kama unataka mambo yako yakuendee vizuri zaidi na zaidi na uache kujuta, lazima umshirikishe Mungu. Mweke yeye namba moja katika ndoa/uhusiano wako, mweke mpenzi wako mikononi mwake na mwisho utaona mafanikio.
Machozi yako hayatamwagika tena ikiwa utamtanguliza yeye.

Wengine hujisahau mapema, wanajiona wanaweza kila kitu bila msaada wa Mungu, nani amekudanganya? Usijidanganye ndugu yangu, wengi ambao wanamtumainia Mungu mambo yao huwanyookea.

Katika mapenzi kuna aina nyingi za uhusiano, wengine huwa na mtu kwa muda mfupi wakati wapo ambao wanatamani sana kuishi na wenza wao baada ya kuwa katika uhusiano wa kawaida.

Inapendeza sana kama wote mtakuwa mnawaza katika umoja, yaani lililopo kichwani mwako ndilo lililomo kichwani mwa mpenzi wako, vinginevyo lazima mmoja wenu atalia!

Unapokuwa katika uhusiano na mpenzi ambaye moyo wako umemfia na unatamani kufunga naye ndoa, lakini wakati huo huo mpenzi wako huyo hana muda na jambo hilo ni hatari sana.

Inawezekana unafahamu juu ya jambo hilo na unachojaribu kufanya ni kumlazimisha/kumshawishi zaidi ili awe na fikra kama zako jambo ambalo mara nyingi husababisha mtafaruku.

Hata hivyo, siyo kila aliye katika uhusiano usio na dira ameamua yeye kwa mapenzi yake, wapo
wanaolazimishwa na wazazi au walezi lakini pia kuna ambao hudhamiria kuwashawishi wenzi wao wabadili uamuzi ili mwisho waweze kuolewa. Mpo?

Utumwa kivipi?
Unaweza kuwa katika utumwa wa mapenzi kwa kulazimisha hisia zako mambo ambayo moyo wako haukubaliani nayo. Hapo sasa ni kama utakuwa umeingia gerezani. Hapo namaanisha ni ile hali ya kuwa au kuishi na mpenzi ambaye humpendi kwa moyo wako lakini unalazimika kuwa naye kwa sababu binafsi.

Maana ya pili ni kuishi na mpenzi ambaye hakupendi na unajua kabisa hana mapenzi na wewe lakini unalazimisha ukiamini kwamba siku moja anaweza kubadili uamuzi wake. Aina hizi mbili za utumwa ndizo zinazowasumbua wengi na kuendelea kuteseka katika uhusiano ambao mwisho wake ni matatizo.

Wakati unafanya hayo, unatakiwa ukumbuke jambo moja muhimu; wewe ni mtu mzima na unaendelea kukua, umri unasogea hivyo kuendelea kung’ang’ania penzi la mtu ambaye hana mwelekeo (kwa namna moja kati ya mbili nilizoainisha hapo juu) unajiweka katika nafasi ya kutoingia kwenye ndoa. Umenipata? Hebu endelea hapo chini.

Penzi bila pendo la kweli...
Uhusiano wa aina hii ni ule ambao mmoja wao anakuwa hana mapenzi kwa mwenzake lakini analazimisha kuwa naye kwa sababu ya kupata masilahi. Mapenzi ya aina hii siku hizi yameenea sana.

Unakuta mwanamke anaamua kuwa na mwanaume fulani ingawa anajua wazi kwamba hampendi lakini kwa sababu jamaa kishaonyesha mapenzi kwake na anajua wazi anampenda, basi anakubali kwa sababu ya kupata kitu!

Tatizo linakuja pale ambapo jamaa anaamua kufunga naye ndoa moja kwa moja, mara nyingi kwanza huanza kusita lakini baada ya kufikiria kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri kwa marafiki hasa wale wenye tamaa kama yeye, huamua kuingia katika ndoa na mwanaume ambaye hajampenda akitegemea kupata maisha mazuri.

Hii ni kwa pande zote, hata majimama ya mjini wanahonga ili wapate penzi, kazi yao ni kutafuta penzi la kweli kwa gharama yoyote. Uchunguzi unaonyesha kwamba wanawake/wanaume wa aina hiyo ni wale ambao wapo katika ndoa ambazo hawana mapenzi nazo, hivyo hutumia fedha za wenza wao kununua penzi lingine nje. Huu ni utumwa!

Wewe unayefanya hivyo, fikiria kwamba unaishi na mpenzi ambaye unajua kabisa humpendi lakini unamwongopea kwa nje. Unaishi naye kwa manyanyaso, unamtesa, humpi haki yake ya ndoa ipasavyo n.k, fahamu kwamba siku akigundua kwamba unamsaliti au akikufumania, yatakukuta makubwa!

Huna haja ya kuunyima moyo wako haki ya kuwa na yule unayempenda zaidi. Mapenzi hayalazimishwi. Fedha, mali na anasa zote hutafutwa na hata siku moja haziwezi kununua penzi la dhati.

Anza kubadilika ndugu yangu, ondoa fikra zako mbaya na uingize ufahamu mpya utakaokuweka katika ramani ya maisha ya kibinadamu na siyo ya kinyama kama uliyonayo sasa.
Mada bado haijaisha. Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni mshauri wa mambo ya mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Lets Talk About Love vilivyopo mitaani.

Chanzo:Global Publishers. 

No comments: