Wednesday, November 9, 2011

Al-Mahmoudi kurejeshwa nyumbani-BBC

 Al-Baghdadi al-Mahmoudi.


Mahakama ya rufaa mjini Tunis, imeidhinisha kusafirishwa hadi nchini Libya kwa aliyekuwa waziri mkuu nchini humo, Al-Baghdadi Al-Mahmoudi.
"Si uamuzi wa haki, ni uamuzi wa kisiasa," wakili wake, Mabrouk Korchid, aliambia shirika la habari la Reuters.
Ombi la kurejeshwa nyumbani Libya liliwasilishwa na serikali mpya ya Libya, Baraza la Kitaifa la Mpito (NTC).

Bwana Mahmoudi ameelezea wasiwasi kuhusu usalama wake iwapo atasafirishwa hadi Libya.
Bwana Korchid, pia aliteta kuhusu hatua hiyo, akisema: "kama atapata matatizo yoyote nchini Libya, mfumo wa sheria wa Tunisia utakuwa umechangia katika matatizo hayo."
Bwana Mahmoudi, amekuwa waziri mkuu hadi pale Kanali Muammar Gaddafi, alipoondolewa madarakani mapema mwaka huu.
Mwezi Septemba alizuiliwa katika eneo la Tamaghza, Kusini mwa Tunisia, karibu na mpaka wa Algeria.
Alihukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani kwa kuingia nchini humo kinyume cha sheria, uamuzi ambao ulibatilishwa baada ya kukata rufaa.
Hata hivyo, Bwana Mahmoudi baadaye alizuiliwa katika gereza karibu na mji wa Tunis akisubiri uamuzi juu ya ombi la kutaka yeye arejeshwe nyumbani, shirika la habari la AFP limeripoti.
Mwezi Agosti, Tunisia ilitambua rasmi NTC kama serikali ya Libya na imethibitisha kushirikiana nao katika masuala ya kiusalama.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake