Wednesday, November 9, 2011

Ujenzi wa daraja la Kigamboni sasa kuanza mwakani

Hatimaye ujenzi wa daraja la Kigamboni lililokuwa likisubiriwa na wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam, unatarajia kuanza mapema mwakani.
Daraja hilo linatarajia kujengwa eneo la Kurasini ambapo litaunganisha mji wa Kigamboni na sehemu zingine za jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza katika maonyesho ya wiki Mashirika ya Hifadhi za Jamii, yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Ofisa Mkuu wa miradi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), John Ndazi, alisema tenda zilizotangazwa kwa ajili ya kupata kampuni itakayojenga daraja hilo zitafunguliwa mwezi ujao.
Ndazi alisema baada ya kupata kampuni moja, kazi ya ujenzi itaanza mapema mwaka ujao ambao utagharimu dola za Marekani milioni 130. Alisema serikali itatoa asilimia 40 ya fedha hizo na NSSF itatoa asilimia 60 na kwamba baada ya ujenzi wake kukamilika, magari yatakayokuwa yanapita katika daraja hilo yatakuwa yanalipia.
“Magari yote yatakuwa yanalipia wakati yanapita katika daraja hilo kwa kipindi cha miaka 25 na baada ya hapo daraja litakuwa mali ya serikali,” alisema. Daraja hilo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya NSSF ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu na wananchi wengi lakini kwa bahati mbaya uanzishwaji wake umekuwa kitendawili.
Aidha, NSSF imesema inatarajia kujenga nyumba 18,000 za bei nafuu ambazo itaziuza kwa wanachama wake.
Maonyesho hayo ya wiki ya mifuko ya hifadhi yalifunguliwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka na kuhudhuriwa na wananchi mbalimbali.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake