Wednesday, November 9, 2011

Unaishi mbali na mpenzi wako?-3

RAFIKI zangu leo nahitimisha mada hii ambayo imedumu hapa kwa wiki tatu.
Nazungumzia namna ya kudumisha penzi kwa mwenzi ambaye anaishi mbali nawe.
Nilieleza mengi katika matoleo yaliyopita ikiwemo namna ya kila jinsi kuonesha upendo wake kwa mwenzake.
Kama mtakumbuka sawasawa, wiki iliyopita nilianisha aina ya zawadi ambazo zimependekezwa kutumwa kwa wanawake na wanaume.
Hebu twende tukaone zawadi nyingine kabla ya kumalizia na vipengele vya mwisho. Karibuni marafiki.


(i) Maua
Hii ni kati ya zawadi zilizopendekezwa na wataalamu wa mambo ya mapenzi.
Maua ni mazuri sana kwa mwezi aliye mbali, lakini ni vyema kuzingatia na umbali alipo, kwani maua huweza kusinyaa kabla ya kumfikia (hasa kama ukimtumia yaliyo halisi, kwani ndiyo haswa mazuri zaidi.

(iii) Anapendelea nini?
Kutokana na kumfahamu sana mpenzi wako, bila shaka utakuwa unafahamu aina ya vitu anavyopendelea zaidi.
Hii ni nafasi yako kuonesha ubunifu wako na jinsi unavyomjali hata akiwa mbali kwa kumtumia vitu ambavyo huwa anavipenda lakini alipo hawezi kuvipata!
Mathalani, anapenda sana zabibu, lakini amekwenda mkoa ambao zao hilo halipo, hii ni nafasi yako kumtumia.
Inawezekana anapenda sana kusoma vitabu, lakini sehemu aliyopo hawezi kupata, basi nunua majarida, magazeti na matoleo yote ambayo hajayapata kisha mtumie, hakika utakuwa umemfurahisha sana na kumfanya afurahi kupata vitu hivyo.

Hapo umuhimu wako kwake utakuwa mkubwa zaidi ya awali. Ni njia bora zaidi ya kudumisha penzi la mbali.

ACHA KUMSALITI
Ukitaka kufurahia mapenzi, lazima usiwe msaliti. Upo msemo usemao, ukimsaliti mpenzi wako ujue nawe utasalitiwa, sasa ili uepukane na hilo ni vyema ukajiwekea dhana ya uaminifu wewe kwanza.

Jisemee mwenyewe; “Kwanini nimsaliti mpenzi wangu? Nampenda sana lakini...nikimsaliti hatajua, lakini na yeye akinisaliti je?” tafakari maneno hayo kwa makini sana kuna kitu utajifunza.

Jichunge mwenyewe, usikubali kabisa kuharibu thamani yako kwa kumruhusu mtu mwingine aujue mwili wako.
Kumbuka kwamba mwili wako ni kwa ajili ya mpenzi wako pekee, endelea na dhana hiyo siku zote, utafurahi!

Hutaona faida yake kwa haraka lakini fikiria hili kwa makini, kama wewe umeamua kuwa mwaminifu kwa mwenzi wako kwa kutambua thamani yake, kwa nini Mungu asikulindie huko aliko?
Lakini lazima ufahamu jambo moja, Mungu anaweza kukulindia mwenzi wako ikiwa naye anakupenda kwa dhati na ana nia ya kuishi na wewe hapo baadaye.

Hata hivyo, kama mwenzi wako ni tapeli, mambo yake ni ya hovyo, Mungu atakuonyesha, ukweli utakuwa wazi na utajua kitu cha kufanya. 
Achana na usaliti na huo utakuwa mwanzo wa kuelekea kwenye kuujua ukweli.

MUAMINI
Hili halikinzani sana na kipengele kilichopita, baada ya kuhakikisha kwamba humsaliti, sasa ni wakati wako wa kuhakikisha kwamba unamwamini katika kiwango cha mwisho.
Usimwoneshe mashaka sana na nyendo zake.
Wakati mwingine unaweza kumpigia simu asipokee, hilo lisikupe shida.

Kuna baadhi ya watu, akimpigia simu mpenzi wake akiona hajapokea, tayari hisia zake zinakuwa mbali na muda huo huo anamwandikia meseji mbaya za ukali na kumtuhumu kwamba anajua wazi kwamba yupo mahali anamsaliti! Acha. Huna haja ya kufanya hivyo, onyesha kumwamini.

Kama umempigia na simu yake haipatikani, ni wakati wako wa kumwandikia meseji ya kumpa pole kwa kazi kutokana na kutambua kwako kwamba muda huo alikuwa bize.
Mwandikie hivi; “Najua ni majukumu mengi uliyonayo muda huu ndiyo yaliyosababisha ushindwe kupokea simu yangu, usijali kwa hilo.
Nakupenda sana na ninatambua kwamba mimi ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha kwamba nakuwa karibu na wewe kwa kila kitu, nakupenda mpenzi wangu, kazi njema.”

Ujumbe huo utamfurahisha, kama alikuwa na nia ya kukusaliti, hawezi kufanya hivyo kwani atakuwa anajua kwamba anamsaliti mwenzi ambaye anamwamini katika kiwango cha mwisho. Kumuamini kwako kutamfanya aone ni jinsi gani ambavyo wewe mwenyewe unavyojiamini na usivyo na wazo la kumsaliti! Kwa nini yeye akufanyie hivyo? Lazima atabadilisha wazo lake.

Usimwandikie hivi; “Najua upo na wanawake zako huko...ama kweli fimbo ya mbali haiui nyoka, endelea kunisaliti tu.”

Ukifanya hivi, utamfanya azidi kukusaliti na kama alikuwa hana wazo hilo, anaweza kujikuta anafanya hivyo. Kubwa zaidi ni kwamba atafikiria kwamba, ikiwa wewe unamuwazia hivyo, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba hata wewe unamsaliti huko ulipo. Bila shaka wazo la kutafuta mwenzi mwingine linaweza kumwingia.
Kwa nini uruhusu hali hiyo? Hakika unaweza kuacha na kumfanya mwenzi wako azidi kufurahia penzi lako.

MSAPRAIZI
Kufanya safari ya mshtukizo (surprise) ni kati ya mambo ambayo yatamfanya mwenzi wako afurahi.
Lakini lazima uwe makini kabla ya kufanya jambo hili. Ni vyema ukawa na uhakika kwamba mna kipindi kirefu hamjakutana na kila mmoja (hasa yeye) ana shauku sana na wewe.

Nenda bila kumtaarifu, fikia hotelini, kisha mpigie simu ukijifanya upo sehemu ambayo alikuacha.
Baada ya hapo, ukishahakikisha umeteka hisia zake vyema, sasa unaweza kumweleza ukweli kwamba upo katika makazi yake mapya.
Hakika itakuwa furaha kubwa, ingawa pia inawezekana ikawa huzuni, hasa kama alikuwa anakusaliti.
Kama ikiwa hivyo, si haba kwani angalau utakuwa umefahamu ukweli kwamba mwenzi wako hakuwa wako, kwani ni msaliti na aliyekuwa anakupotezea muda wako. Hapo hutakiwi kushauriwa cha kufanya, akili kichwani mwako!

Joseph Shaluwa ni mshauri wa mambo ya mapenzi, anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love na Lets Talk About Love vilivyopo mitaani.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake