Saturday, November 12, 2011

Anakwambia muachane?

Akili za kuambiwa changanya na zako

Mungu kwa ukarimu wake ametuwezesha mimi na wewe tukutane kwa mara nyingine.

 Kona hii inatuunganisha, inatufanya tuwasiliane kwa ukaribu na kupeana kile chenye maana katika maisha ya kimapenzi.

Wiki iliyopita, kuna msomaji wangu alinitembelea ofisini kwetu. 

Alikuja na kilio kwamba mchumba wake amemuacha kwa sababu ya uchafu.

 Nilipomdadisi, niligundua kweli kutokuwa msafi, ndilo jambo lililomponza. Jamani tuwe wasafi ili tuwe bora katika mapenzi.

Tuache uvivu na uchafu kwa maana hata siku moja, usitegemee kuwa na mvuto ikiwa huwezi kujiweka nadhifu.

 Mwenzi wako hatajisikia huru na kuzidisha upendo kwako wakati unatoa harufu ya kuudhi.

Tundu za pua yake zinateswa na kwapa lako, kwa hiyo anapunguza upendo. 

Unaoga sawa lakini nguo ya ndani haibadiliki, kila siku hiyo hiyo tu, matokeo yake siku unatakiwa uvue, inabidi uombe kwanza taa izimwe. Ni aibu!

Wewe mwenyewe nguo yako ya ndani huikubali, iweje kwa mwenzio? Nguo ya rangi nyeupe inabadilika mpaka kuwa udongo. 

Hutunzi harufu ya kinywa kiasi kwamba ukiongea, mwenzako anafikiria bora ufike mshindo haraka ili ashike hamsini zake.

Kwa kukazia hapo, nikupe ushauri kuwa unatakiwa uwe mzuri katika kuangalia maeneo muhimu. 

Ujue kukabili jasho la kawaida na lile la mafuta. 

Kwapa na eneo nyeti, utambue kuwa huhitaji usafi maalum, vinginevyo utanuka kila siku.

Deodorant msamiati, basi jiweke safi.

 Ukienda haja siyo wazo lako liwe kuwahi kutoka uendelee na shughuli zako, bali hakikisha unajisafisha kwa ujazo unaotosha. 

Maeneo hayo yana jasho la mafuta kwa sababu yanazibwa na joto ndiyo maana harufu yake ni kali.

Turudi kwenye muktadha wetu wa leo; furaha ni neno la kawaida sana. 

Limezoeleka na ndiyo maana hata mtu anayeangalia komedi na kuvunjwa mbavu anaweza kusema anacheka kwa sababu amefurahi. 

Tafsiri inakosewa!

Furaha ya kweli ni uhuru wa moyo wako. 

Unapomaliza siku na kufanya mapitio ya siku nzima, unagundua ukweli kwamba siku imekwisha salama. 

Hakuna mgogoro wa aina yoyote uliokumbana nao. 

Hii ndiyo tafsiri ya kweli.

Mpenzi sahihi atakupa furaha ya kudumu. 

Ikiwa kuna kasoro chache za kibinadamu, zinasahihishwa na kuendelea na maisha yenu kwa kiwango bora chenye amani kwa wote. 

Kumbuka kuwa wewe na yeye ni binadamu, hakuna malaika kati yenu.

Ni wewe ndiye unayeweza kupambana kwa ajili ya furaha yako.

 Unapoumia, hakuna mtu wa pembeni anayeweza kufikiria au kuhisi kile ambacho kinakutesa. 

Kwa maana hiyo, kuwa wa kwanza kutanguliza maslahi yako mbele kabla ya kuamua kinachokuhusu.

Unaweza kupoteza fedha lakini ukazipata kutokana na kuhangaika, lakini mpenzi yule yule ni ngumu!

 Akiondoka, anayekuja hawezi kuwa na vigezo bora kama wa mwanzo.

 Hata hisia zako za kupenda, zitapungua kadiri unavyokutana na misukosuko ya mapenzi.

Kisaikolojia, inatolewa muongozo kuwa kadiri mtu anapokumbana na migogoro kwenye uhusiano, ndivyo hisia zake zinavyopotea. 

Kwamba katika kila ugomvi, kuna kiwango cha uaminifu hutoweka endapo upande wenye kosa utashindwa kukiri na kuomba radhi.

Mathalan umesaliti, hata kama mtapata suluhu lakini kile kiwango cha mwanzo cha uaminifu hakitakuwepo tena.

 Inawezekana mkaoana na kuzeeka pamoja lakini kumbukumbu mbaya ikawa inarejea na kuharibu furaha. Mkawa vituko mbele ya wajukuu zenu.

Mantiki ya maneno yangu ni kwamba mwisho pigania furaha yako.

 Kama hakufai na umegundua hivyo ni ruhusa kuachana naye bila shinikizo lakini using’ang’anie mwenye kasoro nyingi kwa maana atakufanya upoteze hata tabasamu lako la asili kwa sababu muda mwingi unanuna.

LAKINI KUNA RAFIKI MSEMA OVYO
Nimekutolea mifano juu na umeona. 

Umejiridhisha mwenyewe kuwa pamoja na kasoro zake bado anastahili kupewa hifadhi ya moyo wako. 

Lakini kuna huyo anayekwambia uachane naye. Je, unampa nafasi gani?

Jibu unalo, lakini kwangu nikikushauri kitaalamu kama muongozo ni kuwa unatakiwa uangalie moyo wako unakupa jibu gani kuliko kusikiliza rafiki anachosema.

 Ujazo wake kwenye moyo wako haujui na hatambui ni kiasi gani utaathirika ukimkosa.

Je, rafiki anakuja na hoja au ngonjera? Anaponda badala ya kukupa njia ya kufanya.

 “Ooh, achana naye, kwanza yule malaya sana atakuua.” Somo hili likupe sababu ya kuwaona marafiki wenye uelewa wa hisia kwa sababu utakapokosa usingizi usiku kwa sababu ya mawazo hatakuwepo.

Kama mwenzi wako hafai au anafaa, jibu lipo ndani ya kuta za moyo wako. 

Ndiyo maana linapokuja suala la kupokea ushauri wa kimapenzi, unatakiwa umuone mtu ambaye ana sifa ya kutoa ushauri. 

Tafuta washauri na siyo wapondaji.

Unaweza kuwaazima masikio marafiki zako, wakampaka mwenzi wako badala ya kukupa ufumbuzi wa kile kinachokusumbua. 

Mwisho ukaona yao ni mazuri halafu kwa hasira ukafikia hatua ya kuchukua uamuzi wa kuachana naye, utajuta baadaye.

 Itakutesa zaidi baada ya kubaini kuwa mmoja wa waliokuwa wanamponda ndiye kamchukua.
Itaendelea wiki ijayo.


www.globalpublishers.info

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake