ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 13, 2011

Mbeya yazidi kutifuka


  Kamanda wa kikosi cha FFU awasili kuokoa jahazi
  Wamachinga watoa masharti, Mr II Sugu awatuliza
  Barclays Bank tawi la Mwanjelwa nusura livunjwe

Mapambano kati ya wafanyabiashara ndogo ndogo wa Jiji la Mbeya maarufu kama wamachinga na polisi mkoani hapa yaliendelea jana ingawa baadaye yalitulizwa baada ya Mbunge Mr Sugu pamoja na Kamanda wa Kikosi cha FFU kujitosa na kuokoa jahazi.
Mapambano hayo yaliingia siku ya
pili huku serikali ya mkoa ikitoa taarifa kuwa watu 235 wametiwa mbaroni, mmoja amepoteza maisha na wengine 17 wamejeruhiwa vibaya, watano kati yao kwa kupigwa risasi za moto na polisi.
Miongoni mwa waliojeruhiwa ni askari wawili ambao walipigwa mawe na wanaendelea na matibabu katika hospitali ambayo hata hivyo haikuwekwa wazi na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Anaclet Malindisa.
Wakati vurugu hizo zikionekana kutulia juzi (Ijumaa) majira ya saa 2:00 usiku, jana hali ilibadilika tena ambapo mapambano yalianza upya kwa wamachinga kuendelea kuchoma matairi na kufunga barabara huku wakiimba nyimbo kuwa wanamtaka mbunge wao Joseph Mbilinyi “Mr Sugu” waongee naye na kwamba hawawataki viongozi wa jiji na serikali wilaya na mkoa.
Kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi mkoani hapa, limelazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatuliza wamachinga hao lakini hadi kufikia majira ya saa 7: 40 mchana bado hali ilikuwa tete katika eneo la Mwanjelwa ambako ndiko chanzo cha vurugu hizo.
Kufuatia vurugu hizo kuendelea kupambana moto, Kamanda wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) nchini, Telesphory Anaclet, alilazimika kuwasili jijini Mbeya kwa ajili ya kuongeza nguvu kukabiliana na wamachinga.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema kutokana na vurugu hizo watu 235 wamekamatwa, watano wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi za moto na 12 wamejeruhiwa wakati wakijinusuru kwenye vurugu hizo na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Hata hivyo wakati Kandoro akitoa taarifa hizo, wanahabari walitaka kujua kama kuna vifo vilivyotokea ndipo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Malindisa alipoeleza kwamba kuna mtu amefariki kutokana na vurugu baada ya kupata taarifa hizo akiwa kwenye mkutano huo na wasaidizi wake.
Malindisa hata hivyo hakutaja jina la mtu aliyefariki.
Kandoro aliendelea kueleza kuwa vurugu hizo zimeishtua serikali hasa kutokana na maandalizi ya matairi na mawe yaliyoandaliwa na watu walioshiriki vurugu hizo na kwamba miongoni mwa waliokamatwa wawili walibainika kutaka kuvunja Benki ya Barcrays tawi la Mwanjelwa.
Hata hivyo alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa vurugu hizo zilikuwa zimepangwa na kikundi cha watu ambacho hata hivyo hakukitaja na kwamba wamachinga si chanzo cha vurugu hizo.
“Dalili zinaonyesha kuwa hizi vurugu ni kama zilipangwa katika kuhakikisha jiji la Mbeya hususani Mwanjelwa halitawaliki, na wala siyo suala la kusema wamachinga wameathirika isipokuwa watu wanatafuta kisingizio cha kuvuruga amani iliyopo,” alisema Kandoro.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alisema vurugu za wamachinga zilizoendelea jana (Jumamosi) ni hatua ya wafanya vurugu hizo kutaka kushinikiza vyombo vya dola kuwatoa nje wenzao 235 waliokamatwa na polisi juzi Ijumaa.
Kandoro alisema vurugu hizi zinamwingiliano na siasa kwani bendera za Chama cha Mapinduzi (CCM) zilichomwa moto huku za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) zikiendelea kupepea mitaani.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kitendo cha watu walioshiriki katika vurugu hizo kueleza kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu kuwa ni Rais katika nchi ya Mbeya na kwamba hawamtambui yeye (Kandoro) aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kisheria.
Alisema kauli hizo na maandishi ya kwenye mabango waliyobeba ni sawa na uhaini na kwamba vitendo hivyo havipaswi kuachwa kuendelea badala yake hatua kali zitaanza kuchukuliwa dhidi ya watu watakaobainika kueneza madai hayo.
“Kwanza nataka niwaambie kumwita rais katika nchi hii ni mmoja tu ambaye ni Rais Jakaya Kikwete, na mimi Abbas Husein Kandoro ni mwakilishi wake katika Mkoa wa Mbeya mpaka hapo atakapoaamua kunipeleka mahala pengine, Evance Balama ni DC wa Mbeya kwa hiyo hapa hakuna mtu yeyote ambaye ni rais,” alisema Kandoro.
Alisema kimsingi hayo ni maneno ya kihaini yanayosemwa na watu na kwamba sasa itafika wakati wa kuanza kuchukuliana hatua kwa kumkamata mtu anayesema maneno hayo ya kihaini.
Kandoro alisema serikali ya mkoa wa Mbeya inatambua kuwa Mbilinyi ni Mbunge halali aliyechaguliwa na wananchi wa Mbeya mjini na nafasi yake inatambuliwa lakini kumuita kama rais wanataka kumchafulia tu na waache mara moja.
Madai ya wananchi kwamba Kandoro ndiyo chanzo cha vurugu hizo za wamachinga.
Kandoro alisema hata hivyo anashangaa kuwepo kwa madai kwamba yeye ndiye chanzo cha vurugu za wamachinga Mbeya wakati hakuna hata siku moja aliyozungumzia suala la wamachinga waondolewe na kupelekwa sehemu fulani.
Aliwasihi wananchi wa Mbeya kuzungumzia masuala ya maendeleo na siyo kumzungumza mtu kwani kimsingi hakuna suala la Kandoro ni utaratibu tu uliowekwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuweka mji katika mpangilio unaotakiwa.
Alisema hata hivyo wananchi lazima watambue kuwa nchi hii bado ni changa sana watu wanahitaji kuzingatia mhimili wa sheria ili wasonge mbele kama watakubali kuvunja mhimili wa sheria kwa kila mtu kufanya atakavyo nchi itashindwa kutawalika.
Alisema hata katika nchi zilizoendelea utawala wa sheria ni msingi mkubwa wa kusukuma maendeleo na ukikosea katika hilo utakwama na kushindwa kuendesha nchi katika mstari unaotakiwa.
Kandoro alisema wananchi lazima watambue kuwa mji una taratibu zake, unatakiwa uwe msafi na mahala popote penye msongamano mkubwa wa watu ukikosea na kuacha uchafu ukiendelea utasababisha maafa makubwa kwa afya ya watu.
CHADEMA YAMTAKA JK AMWAJIBISHE RC
Mwandishi Wetu Muhibu Said anaripoti kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete, kumwajibisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, kwa madai kwamba, amepungukiwa na sifa za uongozi na hivyo kuzua vurugu zinazotokana na mapambano kati ya wafanyabiashara ndogodogo (Wamachinga) na Jeshi la Polisi katika kila mkoa anaopelekwa kuuongoza.
Pia kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, kuwawajibisha viongozi wote wa jeshi hilo waliohusika na kupanga mashambulizi aliyoyaita “manyanyaso” dhidi ya wamachinga mkoani humo juzi.
Viongozi hao aliwataja kuwa ni pamoja na Kamanda wa Polisi (RPC), Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO), mkoani humo.
Vilevile, kimemwagiza Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, maarufu kama Mr. II, kutumia fursa ya maswali ya papo kwa papo bungeni kwa Waziri Mkuu Alhamisi ya wiki ijayo, kudai tamko la serikali litakaloeleza ufumbuzi wa kudumu dhidi ya tatizo la wamachinga kutokuwa na maeneo yanayoeleweka ya kuendesha biashara zao.
Kauli hiyo ya Chadema ilitolewa na Mkurugenzi wake wa Habari na Uenezi wa Taifa, Erasto Tumbo, alipozungumza na waandishi wa habari, katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam jana.
MBILINYI AFANIKIWA KUTULIZA GHASIA
Habari nyingine iliyoandaliwa na waandishi wetu Emmanuel Lengwa na Thobias Mwanakatwe, Mbeya inaeleza kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la Mr.II Sugu jana alifanikiwa kutuliza vita kali baina ya wafanyabiashara ndogo ndogo na vikosi vya polisi vya kutuliza ghasia kutoka mikoa mitatu ya Nyanda za Juu Kusini iliyodumu kwa siku mbili mfululizo jijini Mbeya.
Sugu ambaye alisafiri usiku kucha kutoka Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge, alifika jijini Mbeya majira ya saa 3:00 asubuhi na kwenda moja kwa moja katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, kuonana na Kamati ya Ulinzi na Usalama kabla ya kuzungumza na wamachinga katika kituo cha daladala cha Kabwe kilichopo eneo la Mwanjelwa Mjini hapa.
Akizungumza na maelfu ya wananchi pamoja na wamachinga waliojitokeza kwenye mkutano huo, Sugu alisema amekubaliana na viongozi wa Mkoa pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuwa wamachinga hao waendelee na shughuli zao kama kawaida katika maeneo waliyokuwa wakifukuzwa hadi pale Halmashauri ya Jiji itakapowapatia maeneo mazuri ya kufanyia biashara zao.
"Tumekubaliana kuwa wamachinga waendelee na shughuli zao wakati Uongozi wa Halmashauri ya Jiji ukijiandaa kuja na mikakati itakayokubaliwa na wamachinga wenyewe juu ya kuwapatia eneo zuri la kufanyia biashara," alisema Sugu huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wakimsikiliza.
Sugu alisema pia wamekubaliana kuwaachia watu wote waliokamatwa na Polisi kuanzia juzi hadi jana kutokana na mapambano yaliyokuwa yakiendelea baina ya askari na wamachinga waliokuwa wakipinga kuhamishwa kwenye maeneo yao ya biashara.
Alisema pia amekubaliana na viongozi wa Mkoa wa Mbeya kuwaondoa askari wote mitaani na kuwaacha wananchi wafanye shughuli zao kwa amani bila hofu kama ilivyokuwa zamani kabla ya kutokea kwa mapambano hayo.
"Kwa makubaliano hayo mkutano huu ndio nataka uzike matatizo ya wamachinga katika Jiji la Mbeya na kama yatajirudia mimi nitaungana na ninyi kuingia mitaani," alisema Sugu.
Hata hivyo, Sugu aliwaomba wamachinga kutoendelea na vurugu na badala yake leo waamkie kwenye biashara zao na shughuli nyingine za kiuchumi kama ilivyokuwa zamani kabla ya kuibuka kwa vita hiyo.
Awali Sugu aliwaeleza wananci hao kuwa wakati akiwa kwenye Kamati ya Ulinzi ya Mkoa, alipewa taarifa kuwa Mtu mmoja alikufa kwa kupigwa risasi na Polisi, watu 28 walijeruhiwa kwa risasi na wengine 238 walikamatwa na Polisi na kuwekwa ndani kutokana na vurugu hizo.
Sugu alitumia fursa hiyo kuwapa pole wafiwa, wale waliojeruhiwa, waliokamatwa na wamachinga wote kutokana na misukosuko waliyoipata katika sakata hilo.
Aidha Mbunge huyo aliwapongeza wamachinga hao kwa kuendesha harakati zao zote bila kupora kitu cha mtu, hali ambayo alisema wamefikisha ujumbe kwa wahusika bila ya kuonyesha kuwa walikuwa na nia ya kufanya uhalifu mwingine.
Alisema kwa kufanya hivyo wamemrahisishia yeye (Sugu) kama mbunge wao, kazi ya kujenga hoja za kuwatetea na kuelezea hisia zao kwa kuwa wameonyesha kuwa madai yao ni ya msingi.
Katika Mkutano huo, Sugu aliongozana na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Evance Balama ambaye hata hivyo wananchi walikataa kata kumsikiliza kwa madai kuwa alishindwa kuwasaidia kutatua matatizo yao mapema.
Licha ya Balama kupewa kipaza sauti na kujaribu kuwaeleza wananchi kuwa yuko upande wao, wamachinga walipaza sauti na kupiga kelele za kuzomea na kutamka kuwa hawamtaki, hali ambayo ilisababisha Mkuu huyo wa wilaya kurejesha kipaza sauti kwa Sugu aendelee kuzungumza na wapiga kura wake.
Vurugu hizo zilianza Ijumaa majira ya saa 3:00 asubuhi na kudumu hadi jana mchana mpaka wamachinga walipomwona Sugu na kutangaziwa kuwa alikuwa anakuja kuzungumza nao.
Jitihada za Jeshi la Polisi, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Wananchi (JWTZ) kupambana na wamachinga ili kuzuia vurugu hizo ziligonga mwamba kwa siku mbili mfululizo, na wakati wamachinga wakipambana, muda wote walikuwa wakiimba nyimbo za kumkataa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro.
Naye Beatrice Shayo kizungumza kwa njia ya simu kutoka Mkoani Dodoma na Mbunge wa viti maalamu Mkoani Mbeya, Mary Mwanjelwa (CCM), alisema kuwa ameshtushwa na vurugu hizo na kuwapa pole wakazi wenzake wa Mwanjelwa.
Mwanjelwa amewataka wakazi hao kuwa na subira kwani malalamiko yao yanashughulikiwa na kwamba tayari ameshazungumza na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusiana na jambo hilo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

1 comment:

Anonymous said...

safi sana wananchi wa mbeya huo ndio mshikamano mzuri sio tunakuwa wajinga na serikali inatupeleka jinsi itakavyo, ni lazima wajue nasi tunahaki zetu za msingi sio wanatupeleka kama kuku