Amtaka atoke mahabusu kesho ili kuleta utulivu
JK, Prince Charles wa Ungereza watakuwa Arusha
Mkutano wa Mnyika waingia dosari, Polisi wavamia
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demekrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, atatoka mahabusu kesho (Jumatatu) na kufanya mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya NMC Ltd.
JK, Prince Charles wa Ungereza watakuwa Arusha
Mkutano wa Mnyika waingia dosari, Polisi wavamia
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demekrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, atatoka mahabusu kesho (Jumatatu) na kufanya mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya NMC Ltd.
Mbowe ambaye alifika jijini hapa kumuona Lema katika Gereza la Kisongo, ambako amewekwa mahabusu tangu Jumatatu iliyopita, alisema amemwelekeza atoke kesho.
“Nimekuja hapa kumpa maelekezo Mbunge Lema atoke Jumatatu kwa sababu Jumanne vikao vya Bunge vinaanza na ni muhimu kwake kuhudhuria,” alisema.
Alisema wakati akienda kumuona gerezani, tayari makamishna wawili kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, pamoja na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha na Ofisa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha, walimtembelea mahabusu kumsihi akubali kutoka ili kuleta utulivu jijini hapa.
Alisema chama chake kimekubali kumwekea dhamana na kumwelekeza atoke mahabusu, kwa sharti walilowapa polisi kwamba baada ya kutoka mahakamani apokelewe na wafuasi wake na kusindikizwa hadi viwanja vya NMC Ltd ambako atazungumza na wapiga kura wake kuelezea yaliyojiri.
Alisema wameamua kufanya hivyo kutokana na vikao vya bunge kuanza Jumanne na kwamba anahitajika kuwepo bungeni.
Awali alisema chama hicho kilipanga kufanya mikutano mikubwa ya hadhara kwa muda wa siku saba kuanzia Jumatatu.
Alisema mikutano hiyo ilipangwa kuanza majira ya saa 4 asubuhi hadi saa 12 jioni, lakini Jeshi la Polisi limewaomba wasitisha kufanya mikutano hiyo kwa sababu katika wiki hiyo kutakuwa na ugeni wa watu mashuhuri jijini hapa.
Alisema polisi walisema ugeni wa kwanza ni ujio wa mtoto wa mfalme wa Uingereza, Prince Charles, ambaye atawasili jijini hapa tarehe 9 na baadaye atakuja Rais Jakaya Kikwete.
Kutokana na ugeni huo, Mbowe alisema polisi wameomba mikutano hiyo isifanyike ili kuleta hali ya utulivu.
Hata hivyo, alisema chama chake kimebeba dhamana hiyo na kuamua kusitisha kwa sharti kwamba Lema aruhusiwe kusindikizwa na wapiga kura wake baada ya kutoka mahakamani hadi kwenye viwanja vya NMC na kuzungumza na wananchi.
Alisema iwapo atazuiwa kufanya hivyo, basi chama chake kitatoa taarifa ya kufanyika kwa mikutano hiyo, licha ya kuwepo kwa ugeni huo.
“Polisi wasijaribu kuzuia wanachama kumpokea Lema wakati akitoka mahakamani Jumatatu wala kuzuia mkutano wake akizungumza na wananchi…mbunge amekaa mahabusu kwa wiki nzima, hivyo alikuwa na ujumbe mzito wa kuueleza umma, ni vema akipewa nafasi ya kuzungumza na wapiga kura wake,” alisema.
Alisema yapo mambo mengi yanayolalamikiwa kama vile suala la umeya, udiwani, manyanyaso ya polisi ambayo watayaeleza katika mkutano huo.
Alisema iwapo polisi watamzuia kufanya mkutano huo, watalazimika kufanya mikutano yao kama kawaida na kwamba ujio wa mtoto wa mfalme utakuwa ni kielelezo kizuri sana cha kupeleka ujumbe kimataifa.
“Mikutano ya siku saba ni maamuzi magumu sana ambayo chama ilifikiria kuchukua, bado ujio wa mtoto wa mfalme kwetu tunauona kuwa ni mzuri wa kupeleka ujumbe, pengine itakuwa ni wakati muafaka kwa dunia kujua yanayotokea Arusha na Tanzania kwa ujumla,” alisema.
MKUTANO WA MNYIKA WAINGIA DOSARI, OPOLISI WAVAMIA
Jeshi la Polisi mkoa wa Kinondoni limewakamata watu waliokusanyika kwa ajili ya kumsubiri Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, kuwahutubia kwa madai ya kuhofia Al Shaabab.
Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na Diwani wa Sarange, Ephahim Kinyafu, Katibu Mwenezi wa jimbo, Ali Makwiro, mfanyakazi Ofisi ya Mbunge, Julius Mgaya na dereva wa gari ambalo lilikuwa limewekwa kipaza sauti, Jafari Mbaga.
NIPASHE Jumapili jana jioni ilishuhudia purukushani kati ya jeshi la polisi na wafuasi hao ambao walikusanyika eneo la Ubungo karibu na baa ijulikanayo kama Corner baa, kwa lengo la kumsubiri Mbunge wa jimbo hilo.
Wakati wakiendelea kumsubiri, ghafla majira saa 10:27 jioni zaidi ya polisi wanane wakiwa na magari na vitendea kazi mbali mbali walifika eneo hilo na kuanza kuwakamata viongozi hao pamoja na wananchi waliokuwa wamevalia sare za chama hicho.
Hata hivyo, kamata kamata hiyo ambayo ilidumu takriban dakika tano, ilisababisha wafuasi waliokuwepo eneo hilo kuduwaa na kushindwa kufanya chochote dhidi ya polisi hao.
Baada ya askari hao kuwakamata watu hao pamoja na gari lililokuwa limebeba spika, waliondoka eneo hilo na ndipo Mnyika alipowasili eneo hilo na kulazimika kutumia gari lake kama jukwaa kuwahutubia wananchi waliobaki.
Mnyika, aliwaeleza wananchi kuwa, polisi hawajafuata utaratibu.
“Polisi hawajafuata taratibu kwani wanawakamata viongozi waliochaguliwa na wananchi na wanawakataza kuongea na nyinyi kwa kisingizio kuwa kuna Al Shaabab, je swali la kujiuliza hawa Al Shaabab wanafuata nini hapa, nilitegemea wangenikamata mimi,” alisema na kuongeza:
“Ningependa hili la tishio la Al Shaabab ambalo linatumika kama kisingizio Rais atoe tamko, atueleze kuwa nchi ipo kwenye hatari, nakumbuka Jumamosi iliyopita jeshi la polisi hili hili lilizuia maandamano ya wanaharakati waliokuwa wakipinga Dowans na siku hiyo kulikuwa na mpira wa Simba na Yanga na mimi nilikuwa na mkutano Mbezi Msigani na ulifanyika vizuri mbona kisingizio hichi hakikutajwa,” alisema.
Aidha, alisema baada ya mkutano huo ataelekea polisi ili kujua hatma ya waliokamatwa kwa sababu polisi walitakiwa waandike barua kama alivyofanya yeye wakati wa kuomba kufanyika mkutano huo.
Akizungumzia kuhusu lengo la kuitisha mkutano huo, Mnyika alisema lililenga kueleza mafanikio ya jimbo, kukusanya maoni ya katiba ili ayapeleke bungeni.
Pia alisema lengo lingine lilikuwa ni kugawa nyaraka kwa wananchi zilizoelezea suala katiba ambazo hata hivyo mbunge huyo alieleza zimechukuliwa na polisi hao.
Kufuatia tukio hilo, Mnyika aliwaeleza wananchi kuwa, polisi watalazimika kulipa gharama zote ambazo zimetumika kufanikisha mkutano huo.
Katika maoni ya wananchi yaliyotolewa kwenye mkutano huo yalieleza kitendo cha serikali kutowashirikisha kwenye mchakato wa katiba mpya, upanda kwa gharama za maisha na kukataa kulipwa kwa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema wamelazimika kuuvunja mkutano huo kutokana na barua waliyoipokea kutoka kwa mbunge huyo kutojitosheleza baadhi ya mambo pamoja na kuhofia matukio ya kigaidi ambayo yamekuwa tishio nchi mbalimbali duniani.
Kenyela alisema alipokea barua hiyo jana (juzi) huku ndani yake ikionyesha imeandikwa kutoka Alhamis ya wiki hii (Novemba 3).
"Barua hii ya Mnyika iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho,'Maombi ya kushiriki ziara jimbo la Ubungo' ilikuwa na mapungufu kwanza haikutaja tarehe wala siku ya ziara hiyo, zaidi ilibainisha maeneo ya ziara kuwa ni Kibo na Usewe na muda ambao ni kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 12:00 jioni," alisema.
Kenyela alisema kutokana na tatizo hilo kujitokeza kwenye barua hiyo, jana (juzi) alilazimika kumwandikia barua mbunge huyo kumweleza upungufu huo kwenye barua yake.
Alisema barua aliyoiandika kwa Mnyika pamoja na sababu ya kutokuwa na tarehe na muda wa ziara iliyopangwa, pia alimweleza kuwa haikueleza ni ofisi/taasisi zipi ambazo atazizindua na majina ya wahusika wake.
"Hofu yetu sasa hivi ni haya matukio ya ugaidi yanayoendelea duniani, tulifikiri mbunge huyu angetujibu barua tuliyomwandikia badala yake, ameamua kufanya mkutano," alisema.
Hata hivyo, Kenyela hakubainisha idadi ya watu wanaowashikilia kutokana na tukio hilo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake