ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 16, 2011

Mo Ibrahim: Hatutoi tuzo kwa marais wezi



Mwenyekiti wa Taasisi ya MO Ibrahim, Dk. Mohamed Ibrahim, amesema hawezi kuwazawadia marais wezi, wauaji na wanaokiuka haki za binadamu zawadi wakati wa utawala wao, kwa kuwa kufanya hivyo ni sawa na kujitukana mwenyewe.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa Mkutano wa Jukwaa la Viongozi wa Vyombo vya Habari Afrika (AMLF) mjini Tunis mwishoni mwa wiki, Ibrahim alisema amekuwa akipokea malalamiko mengi yakilenga kukosoa tuzo kwa marais waliomaliza utawala wao ambao walifanya vizuri katika kuendesha nchi kuwa anawahonga, na kueleza kuwa ni jambo la ajabu kumhonga mtu ambaye hana tena madaraka.

“Yaani unamhonga mtu ambaye amekwisha kumaliza muda wake wa utawala ili akuisaidie nini? “ alihoji Ibrahim.
Alisisitiza kuwa katika nchi za Afrika madaraka yote ya nchi yamemzunguka Rais, ndiye anagawa vyeo, ndiye mwenye maamuzi ya juu, kwa maana hiyo kama unataka kubadili nchi za Afrika ni lazima uanze na taasisi inayoitwa urais.
Alisisitiza tuzo hiyo inayotolewa kwa marais waliomaliza muda wao wa utawala kiasi cha Dola za Marekani milioni tano huenda kwa wale tu waliothibitisha kwa viwango vyote kuonyesha uwajibikaji, utawala bora, kuzingatia demokrasia na kuheshimu misingi ya haki za binadamu, kamwe si wezi.
“Mimi sina fedha kuliko wezi, wapo marais wezi Afrika, si mnawafahamu sitaki kuwataja, wapo, lakini angalau waliokufa kama Abacha (Sani Abacha wa Nigeria) na Mobutu (Mobutu Seseseko wa Zaire sasa DRC), hawa walikuwa na fedha nyingi za wizi. Sasa hawa mimi nitapata wapi fedha za kuwahonga hawa? Tuzo yetu ni heshima,” alisisitiza.
Tangu kuanza kwa tuzo hiyo marais wa Afrika wastaafu waliofanikiwa kuinyakua ni pamoja na Rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chissano (2007), Rais wa zamani wa Botswana, Festus Mugae (2008) na mwaka huu alikuwa Rais wa zamani wa Cape Verde, Pedro Verona Pires. Mwaka 2009 na 2010 hakukuwa na mshindi.
Katika mkutano huo, pia alizungumzia juu ya viwango vya kupima maendeleo ya nchi za Afrika (MO Index) katika maendeleo ya watu, huduma za afya, mfumuko wa bei, usalama, demokrasia na utawala bora akisisitiza kwamba MO isilaumimiwe kutokana na matokeo ya viwango hivyo kwa sababu wao hupokea takwimu husika kutoka taasisi 23 za kimataifa ambazo wameingia nazo makubaliano.
Alitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa Benki ya Dunia, Shirika la Afya Duniani (WHO), Umoja wa Mataifa (UN) na Transparency International (TI) na kwamba kazi yao ni kuzichambua na kuziwasilisha kulingana na kila nchi ilivyo.
Alisema kwa kawaida amekuwa akipigiwa simu na baadhi ya marais wa Afrika hasa pale nchi zao zinapoboronga na jibu lake limekuwa rahisi tu kwao: “Kumbe umefanya vibaya asante kwa kunifahamisha kwa kuwa nami sijui.”
Ibrahim alisema kuwa katika vigezo vyao wameamua sasa kuanza kukusanya maoni kutoka kwa wananchi wa Afrika juu ya masuala yanayohusu rushwa na kigezo hicho kitaingizwa katika kupima hali ilivyo kwa nchi hizo.
Wapo katika maandalizi ya awali ya kuanza kujenga uwezo wa kufanya kazi hiyo. Alisema vigezo vyao kwa mara ya kwanza vimekuwa ni kioo cha kuakisi hali halisi ilivyo kwa nchi za Afrika, kitaalam, jambo ambalo hapo kabla halikuwako.
CHANZO: NIPASHE

No comments: