ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 20, 2011

Ngeleja atajwa kuchota fedha TPDC

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja Bungeni Dodoma jana
Neville Meena, Dodoma
KAMATI ya Nishati na Madini ya Bunge imeanika uozo katika uendeshaji wa sekta ya gesi nchini, huku ikiitaja Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT) kufanya udanganyifu mkubwa ulioikosesha Serikali mabilioni ya shilingi.

Kamati hiyo ilifanya uchunguzi jinsi sekta hiyo inavyoendeshwa kupitia kamati ndogo iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti, Diana Chilolo na kubaini kwamba PAT ilifanya udanganyifu unaofikia Dola za Marekani 64 milioni (Sh110 bilioni).

Akisoma taarifa hiyo, mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Mbunge wa Bukene (CCM), Selemani Zedi alisema ukaguzi uliofanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ulibaini kuwa PAT walijirudishia fedha hizo kama gharama walizotumia kuzalisha gesi kati ya mwaka 2004 na 2009.

“Kati ya hizo Pan African Energy Tanzania Ltd wamekiri kwamba wamejirudishia isivyo halali kiasi cha Dola za Marekani 28.1 milioni ambazo ni sawa na Sh46 bilioni na kwamba kiasi cha Dola 36 milioni zilizobaki (sawa na Sh64 bilioni) wanaandaa vielelezo vya kuthibitisha uhalali wa kujirudishia gharama hizo,” alisema Zedi.

Kutokana na kubaini ufisadi huo, kamati hiyo imependekeza kusitishwa kwa mkataba baina ya TPDC na PAT na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote waliohusika na udanganyifu ambao umeikosesha Serikali gawio la Dola 20.1 milioni sawa na Sh35 bilioni.

Alisema miongoni mwa njia zilizotumiwa kufanya ufisadi huo ni katika malipo ya kusafirisha gesi ambako PAT ilijipatia kiasi cha Dola za Marekani 20 milioni.

Aliitaja njia nyingine kuwa ni kuweka gharama za uzalishaji wa gesi katika nchi za Nigeria, Gabon na Uganda inakofanya kazi hiyo katika gharama za hapa nchini, hivyo Tanzania ikawa inabeba gharama zote kutoka katika nchi hizo.

Zedi alisema Kamati hiyo pia inataka fedha ambazo PAT ilijilipa kinyume cha sheria na taratibu, zirejeshwe mara moja serikalini na kwamba Wizara ya Nishati na Madini lazima isimame kidete kutetea maslahi ya taifa kwa kushirikiana na TPDC.

“Mpaka Kamati inaandaa ripoti hii, Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd, imeshindwa kuwasilisha uthibitisho wa uhalali wa kujirudishia gharama nyingine zinazofikia jumla ya Dola za Marekani 36 milioni, hali hii inaonyesha shaka kubwa katika uendeshaji wa sekta ya gesi nchini,” alisema Zedi na kuongeza:

“Kitendo cha PAT kuchukua gharama ambazo haikustahili na hatimaye kuisababishia Serikali na TPDC hasara, ni uzembe wa hali ya juu na ni uvunjivu wa sheria za nchi.”

Kamati hiyo ilibainisha kuwa tatizo kubwa katika sekta ya gesi ni kutokuwepo kwa sheria inayosimamia sekta hiyo na badala yake kutumia sheria ya petroli ambayo ina mianya mingi inayoruhusu ufisadi.

Fedha za mafunzo
Taarifa hiyo ya Kamati ndogo ya Nishati na Madini pia ilibaini kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa na TPDC kwa ajili ya kusomesha wataalamu wa shirika hilo na wale wa wizara katika sekta ya nishati hiyo.

Zeli aliliambia Bunge kuwa Wizara ya Nishati na Madini ilipokea kiasi zaidi ya Sh1.5 bilioni kutoka TPDC ambacho ni asilimia 50 ya fedha zilizokusanywa lakini fedha hizo zimekuwa zikitumika kinyume cha sheria.

“Kwa mujibu wa vielelezo kutoka TPDC, inaonekana kuwa Sh 20 milioni zilitumika kama mchango wa maandalizi ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2010/2011 na fedha nyingine zimetumika kulipia tiketi za ndege.”

Imebainika kwamba Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alichukua kiasi cha Sh76.8 milioni kwa ajili ya safari, fedha zilizotolewa na TPDC Mei 6, 2010. Kwa mujibu wa kielelezo namba 19 cha taarifa hiyo, matumizi hayo ya Ngeleja yameandikwa kwa Kiingereza ‘Travel on Duty Minister for Energy and Minerals.’

Kielelezo hicho kinaonyesha kuwepo kwa matumizi mengi ya fedha hasa za safari za kwenda nje ya nchi kwa watendaji kadhaa wa wizara hiyo, matumizi ambayo ni kinyume cha malengo ya fedha hizo.

Baadhi ya matumizi yaliyoko kwenye kielelezo hicho ambacho pia ni sehemu ya taarifa iliyowasilishwa bungeni na kiasi cha fedha kwenye mabano ni  fedha zilizolipwa kwa shughuli za wizara Julai 1, 2009 (Sh40 milioni) na marejesho ya gharama za tiketi ya ndege kwa aliyekuwa Kamishna wa Petroli wizarani hapo Bashir Mrindoko (Sh5.42 milioni), Septemba 9, 2009.

Fedha nyingine zilikwenda kwa ofisa aitwaye P. Victus ambaye Oktoba 8, 2009 alilipwa posho ya safari (Perdiem) Sh3.97 milioni, Oktoba 28, 2009. Yalifanyika pia malipo kwa Victus na Shilla yab Sh5.3 milioni na fedha za kununua tiketi za ndege kwa maofisa wa wizara ya Nishati na Madini Sh14.3milioni.

Desemba 3, 2009 kulikuwa na safari ya kikazi kwa maofisa wa wizara kwenda India ambayo iligharimu kiasi cha Sh10 milioni, wakati Desemba 7, mwaka huo kulikuwa na vikao vilivyoitwa ‘ACM’ ambavyo viligharimu kiasi cha Sh17.1milioni na kingine Sh24.8milioni.

Kadhalika, malipo ya Sh13.2 milioni yalifanyika kwa safari za maofisa ambao hawakutajwa, wakati Januari 21, 2010 kiasi cha Sh4.1 kilitumika kwa ajili ya malazi na mkutano ambao pia haukuelezwa kuwa ni wa nini.
Januari 27, 2010 kulikuwa na malipo ya posho kwa Wizara ya Nishati na Madini kiasi cha Sh85.8 milioni, Februari 23, 2010 kiasi cha Sh5.5milioni kikatumika kulipa gharama za tiketi ya ndege na Septemba 22, 2010 kiasi cha Sh14.84 kilitumika kwa ukarimu katika mkutano wa masuala ya nishati uliofanyika nchini Mexico.

Chimbuko la uchunguzi

Kamati ya Nishati na Madini ilipewa kibali cha kufanya uchunguzi huo na Spika wa Bunge, Anne Makinda baada ya kueleza nia yake katika taarifa kuhusu maoni yake kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini Julai 15, mwaka huu.

Uchunguzi huo ulianza Septemba 5, mwaka huu ulifanywa na Kamati ya Wajumbe tisa, Christopher Ole Sendeka (Simanjiro - CCM), Chilolo (Viti Maalumu -CCM), Yusuph Abdallah Nassir (Korogwe Mjini - CCM), Mwanamrisho Abama (Viti Maalumu - Chadema), David Silinde (Mbozi Magharibi - Chadema), Mbarouk Salum Ali (Wete - CUF), Sarah Msafiri (Viti Maalumu - CCM) na Zedi.

Uchunguzi wa Kamati hiyo ulijikita katika mkataba baina ya Serikali na Songas, pamoja na ule unaoipa Kampuni ya Pan African Energy mapato makubwa yanayotokana na uzalishaji wa petroli (Production Sharing Agreement), badala ya fedha hizo kwenda TPDC.


Mwananchi

No comments: