Mamlaka ya Usafirishaji Nchi Kavu na Baharini (Sumatra) imeanza kufanya kazi ya ukaguzi wa meli za abiria na mizingo za Zanzibar baada ya kufukuzwa miaka mitano iliyopita.
Ofisi za mamlaka hiyo zilifungwa visiwani humo mwaka 2006, baada ya kubainika kufunguliwa kwa huduma zake huko Zanzibar kulifanyika kinyume cha sheria kwa sababu shughuli za usafiri baharini hazimo katika orodha ya mambo ya Muungano.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana mjini hapa, Mkurungezi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Haji Vuai Ussi alithibitisha kuwa Sumatra imerejesha tena huduma za ukaguzi wa meli zote zilizosajiliwa Zanzibar.
Alisema hatua ya mamlaka hiyo kurejesha huduma zake Zanzibar ni utekelezaji wa uamuzi wa kikao cha Baraza la Usalama wa Taifa kilichofanyika Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, mara baada ya ajali ya Mv. Spice Islander Septemba 10, mwaka huu.
Ussi alisema tangu Sumatra ilipoanza kufanyakazi ya ukaguzi meli, tayari meli mbili zimezuiwa kutoa huduma baada ya kugundulika na matatizo ya kiufundi, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa abiria na mizigo. “Tumeanza kushirikiana na Sumatra katika utekelezaji wa uamuzi wa Baraza la Usalama la Taifa,” alisema Mkurugenzi huyo.
Alitaja meli zilizozuiwa kutoa huduma katika mwambao wa Zanzibar na Tanzania bara kuwa ni Mv Seagull na Mv Serengeti.
Alisema uamuzi wa kuruhusu Sumatra kufanyakazi Zanzibar ni hatua ya kukabiliana na upungufu wa wakaguzi wa meli na wanasheria na kwamba kurejea kwa wataalam wa mamlaka hiyo visiwani kutarahisisha shughuli za ukaguzi wa meli kufanyika kwa muda muafaka.
Alisema ZMA ina wakaguzi wawili tu, kati ya sita wanaohitajika kwa kazi hiyo huko Unguja na Pemba, na kwamba mamlaka hiyo tayari imekamilisha hatua za ajira yao tangu mwaka jana.
Ussi alisema upungufu wa wakaguzi unasababisha meli kutofanyiwa ukaguzi kwa wakati muafaka kwa mujibu wa sheria ya usafiri baharini ya mwaka 2006 ya Zanzibar inayozingatia taratibu za Shirikisho la Kimataifa la Usafiri baharini (IMO) juu ya meli kufanyiwa ukaguzi kila mwaka.
Zaidi ya meli 80 za abiria na mizigo zimesajiliwa Zanzibar.
Naibu Waziri wa Mindombinu na Mawasiliano Zanzibar, Issa Haji, alisema serikali inatambua tatizo la upungufu wa wakaguzi wa meli.
Alisema upungufu huo unatokana na uchanga wa ZMA, kwani ilianzishwa mwaka 2006 tu na kwamba bado serikali inaendelea kuiimarisha mamlaka hiyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment