Serikali imeshauriwa kutowapuuza wananchi ama kikundi chote kinachohoji mchakato wa kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya muunganio wa Tanzania kwa kuwa ikiwapuuza itakwama mbele ya safari.
Ushauri huo ulitolewa jana na Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba katika mdahalo wa katiba ulioandlaiwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
“Watanzania waachwe watoe maoni yao wenyewe na hayo maoni yachukuliwa kama yalivyo bila kuchakachuliwa,” alisema.
Alivitaka vikundi vya vya kiraia, vyama vya siasa na wanaharakati kuwapa fursa wananchi ili watoe maoni yao wenyewe badala ya wao kuwasemea.
Alisema wanaohoji mchakato wa katiba wasipuuzwe na badala yake wasikilizwe kwa kila jambo watakalosema kwani hiyo ni haki yao.
Kwa upande wake, Mkugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Joseph Butiku, alisema Katiba ndiyo msingi wa maadili na kwamba kama viongozi wa nchi wataongoza bila kuifuata itakuwa ni kazi bure.
“Katiba ndiyo msingi wa maadili, sasa endapo wewe unaendesha nchi kinyume na maadili ni kazi bure, sheria zipo lakini hazifuatwi, bila kufuata katiba hata ziandikwe katiba 100 ni kazi bure,” alisema.
Butiku alisema Tanzania inaendeshwa na katiba na kwamba vyama vyote vya siasa lazima viifuate.
Baada ya kumalizika mdahalo huo, washiriki walitoa mapendekezo mbalimbali ambayo walitaka yawasilishwe serikalini ili yajadiliwe katika mchakato unaoendelea kuhusu uandikaji wa katiba.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment