Spika wa Bunge, Anne Makinda, leo atakabidhiwa ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza sakata linalomkabili Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema ripoti hiyo itakabidhiwa muda wowote leo mara baada ya kipindi cha maswali na majibu.
“Hajakabidhiwa bado, atakabidhiwa kesho (leo), nadhani mara baada ya muda wa maswali na majibu kumalizika,” alisema Dk. Kashililah. Tayari orodha ya shughuli za Bunge inaonyesha kuwa ripoti hiyo ni miongoni mwa hoja zitakazowasilishwa na kujadiliwa katika mkutano wa Tano unaonza leo mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Bunge kupitia Idara yake ya Habari, Elimu kwa Umma na Mahusiano ya Kimataifa jana, ilisema Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa ili kuchunguza uhalali wa Jairo kuchangisha fedha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini ili kupitisha bajeti ya wizara hiyo bungeni.
Pamoja na hilo, kamati hiyo pia itawasilisha taarifa ya uchunguzi kubainisha endapo kitendo cha Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, cha kutoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya uchunguzi wa suala la fedha zilizochangisha, hakikuingilia kinga na madaraka ya Bunge.
Luhanjo anatuhumiwa kuingilia haki, kinga na madaraka ya Bunge na kumsafisha Jairo dhidi ya kashfa inayomkabili. Jairo anakabiliwa na kashfa ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanikisha kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Katika tuhuma hizo, Luhanjo anadaiwa kutamka mbele ya waandishi wa habari Agosti 27, mwaka huu, kwamba: “Alichofanya Jairo ni utaratibu wa kawaida kabisa...na kama Jairo ataweza kuwashtaki waliomdhalilisha ni yeye tu.”
Jairo alisimamishwa kazi Julai 21, mwaka huu, kupisha uchunguzi dhidi yake, baada ya kuwapo shaka ya mazingira ya rushwa, kutokana na uamuzi wake wa kuziagiza taasisi na idara zilizo chini ya wizara yake kila moja kuchanga Sh. milioni 50 ili kufanikisha makadirio ya wizara kupitishwa na Bunge.
Uchunguzi huo ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa siku 10 na kuukamilisha.
Agosti 24, mwaka huu, Jairo alirejea kazini baada ya Luhanjo kuamuru hivyo kwa madai ya kutopatikana na hatia, na kupokewa kwa vifijo na nderemo na wafanyakazi wenzake wizarani hapo.
Hata hivyo, siku moja baada ya kurejeshwa kazini, Rais Jakaya Kikwete, alimsimamisha tena kazi.
Kamati hiyo teule yenye wajumbe watano, ilitangazwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, muda mfupi kabla ya kuahirisha Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi, Agosti 26, mwaka huu. Iliundwa baada ya wabunge kuridhia ufanyike uchunguzi huo.
Miongoni mwa kazi zake, ilikuwa ni pamoja na kuchunguza sakata lote la kumsafisha Jairo dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Wajumbe wanaounda kamati hiyo, ni pamoja na Mwenyekiti wake, Ramo Makani (Tunduru Kaskazini-CCM); Gosbert Blandes (Karagwe-CCM); Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema); Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF) na Martha Umbulla (Viti Maalum-CCM).
Kamati hiyo ilifanya kazi kwa kuongozwa na hadidu rejea tano; ya kwanza ikiwa ni kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilishwa kwa uwasilishaji wa hotuba za bajeti za wizara bungeni.
Hadidu rejea hiyo ya kwanza itakuwa na vipengele vitatu; ambavyo ni kuchunguza uhalali wa utaratibu huo kisheria na kwa mujibu wa kanuni iwapo fedha hizo huwa zinakasimiwa katika bajeti husika pamoja na matumizi halisi ya fedha zilizokusanywa.
Hadidu rejea ya pili, ni kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu uchunguzi alioufanya kuhusiana na agizo la Jairo kuchangisha fedha taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha uwasilishaji wa bajeti ya wizara hiyo bungeni. Pia kuchunguza mfumo wa serikali kujibu hoja zinazotolewa bungeni na taratibu za kuliarifu Bunge matokeo ya utekelezaji wa hoja hizo.
Nyingine ni kuchunguzwa kwa usahihi wa utaratibu uliotumiwa na Luhanjo, kwa suala la Jairo na kubaini iwapo utaratibu huo umeathiri dhana ya haki na madaraka ya Bunge.
Ya tano, ni kuangalia nafasi ya mamlaka ya uteuzi kwa ngazi ya makatibu wakuu katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya anaowateua na kuangalia mambo mengine yoyote yanayohusiana na masuala hayo.
MNYIKA APANIA KUFUFUA RICHMOND
Mbali ya kamati ya Jairo, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, anakusudia kuwasilisha hoja binafsi bungeni, inayotaka mjadala wa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, ufunguliwe na kujadiliwa upya.
Akizungumza na NIPASHE mjini hapa, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), alisema maazimio hayo 23 hayajatekelezwa ndio maana kumekuwepo na migogoro inayoendelea nchini.
“Maazimio hayajatekelezwa ndio maana kuna migogoro inayojitokeza hapa nchini na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kwa wahusika wa suala hiyo,” alisema.
Alipoulizwa kwanini hoja hiyo haikuwa kwenye orodha ya shughuli za Bunge, Mnyika alisema kanuni ya 55 inamtaka mbunge anayewasilisha hoja binafsi awasilishe siku moja kabla ya mkutano wa Bunge kuanza.
Kwa mujibu wa Mnyika, taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja hiyo aliiwasilisha jana kama Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007 kifungu cha 54 (4) na 55 (1) kinavyosema.
Alisema lengo la hoja yake ni kutaka uamuzi wa Bunge uliofanyika katika Bunge la Tisa Mkutano wa 18 wa Februari, 2010 kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya mkataba baina ya Shirika la Umeme (Tanesco) na kampuni ya Richmond Development Company LLC; ubadilishwe.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema bado hawajapokea taarifa ya hoja hiyo.
Sakata la Richmondo lilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa pamoja na waliokuwa mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini, Nassir Karamagi, Ibrahim Msabaha kujiuzulu nafasi zao za uongozi Februari 2008.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment