Gari la polisi Iringa likiwa limeharibiwa vibaya katika tukio lililomuhusisha mfanyabiashara maarufu wa mjini Iringa Mama Mbilinyi anayetuhumiwa kuwa anaishi na watu wanaodhaniwa kufa. (Picha na Frank Leonard). WAANDISHI wa habari zaidi ya 10 na askari Polisi zaidi ya 10 pia wamenusurika kuuawa na wananchi waliotaka kuchoma moto nyumba ya mfanyabiashara maarufu wa mjini Iringa wanayemtuhumu kuishi kishirikina na misukule. Akizungumza na wanahabari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Evarist Mangala, alimtaja mfanyabiashara huyo kwa jina la Mama Mbilinyi ambaye pamoja na mumewe aliyetajwa kwa jina la Mzee Mbilinyi, walinusurika kuuawa na wananchi hao waliowashambulia kwa mawe na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa. Tukio hilo lililovuta hisia kali za wakazi wa hapa na vitongoji vyake, lilitokea juzi saa 11 jioni maeneo ya Frelimo ilipo nyumba ya kifahari ya mama huyo, baada ya jitihada za polisi hao kudhibiti wananchi hao kugonga mwamba. Pamoja na mama huyo kujeruhiwa kwa mawe, mwandishi wa habari hizi naye alipigwa jiwe lililomjeruhi taya la kushoto, huku mwandishi wa ITV, Laurian Mkumbata, akivunjiwakamera na Ofisa wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Iringa, katika mazingira ya kutatanisha. Wengine waliojeruhiwa na kukimbizwa katika hospitali kwa matibabu ni pamoja na polisi wanne na watu wengine saba akiwamo mmoja aliyepigwa risasi ya mguu alipotaka kuimwagia nyumba hiyo petroli ili aitie moto. Mangala hakutaja majina ya majeruhi hao zaidi ya kuahidi kuwa suala la mwandishi huyo wa habari kuvunjiwa kamera atalishughulikia baada ya kupata barua yenye maelezo ya jinsi ofisa huyo alivyofanya. Baadhi ya wananchi hao wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 2,000 waliokuwa wameizingira nyumba ya mama huyo yenye uzio wenye nondo kubwa waliirushia mawe baada ya madai yao ya kutaka misukule waliodaiwa kuwa ndani ya nyumba hiyo kutoonekana. Kazi ya kutafuta misukule hao ndani ya nyumba ya mfanyabiashara huyo, ilifanywa na askari hao waliokuwa wamefuatana na familia ya mama huyo, wanahabari, wachungaji na wawakilishi wa wananchi wa maeneo hayo. Baada ya kupekua nyumba nzima kikiwamo anamolala mfanyabiashara huyo, hakuna msukule aliyeonekana ndipo wananchi hao walipopaza sauti zao wakidai walioshiriki upekuzi wamepokea rushwa ili wasiwatoe misukule hao. Wakati Jeshi la Polisi likitaka kumnusuru mama huyo kutoka kundi hilo la wananchi, ndipo wananchi hao walipoonesha hasira kwa kurusha mawe wakati akiingizwa ndani ya gari la Polisi ili apelekwe kituo cha Polisi. Pamoja na jitihada za askari hao kutumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za moto kuwatawanya, hali ilizidi kuwa tete baada ya kuzidiwa nguvu. Mazingira hayo yaliwalazimisha askari, wanahabari na watu wengine walioshiriki upekuzi wa misukule ndani ya nyumba hiyo, wakimbilie gereji ya mama huyo na kujifungia ili kunusuru maisha yao. Wakiwa humo, wananchi hao waliendelea kuvurumisha mawe dhidi ya gereji, nyumba anayoishi mama huyo na mali zingine yakiwamo magari yake matatu na la Polisi, ambayo yaliharibiwa vibaya kutokana na mawe hayo. Wakati wananchi hao wakijiandaa kuichoma moto nyumba hiyo askari wengine zaidi ya 20 kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walifika na kusaidia kutawanya watu hao. Baada ya kutawanyika baadhi ya askari waliendelea kuilinda nyumba hiyo, ili kuzuia wananchi kurudi kuichoma moto. Taarifa za baadaye zilizotolewa na Kamanda Mangala zilithibitisha kwamba baada ya kupewa matibabu, mama huyo aliruhusiwa kurudi nyumbani kwake baada ya kuomba hivyo. |
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake