Wednesday, November 16, 2011

Watanzania wajiunga kikundi cha al Shabab

WATANZANIA 10 wamekamatwa katika mipaka ya Somalia wakihusishwa na kikundi cha ugaidi cha al Shabab, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha amesema. 

“Kenya wamewakamata Watanzania 10 katika mipaka ya Somalia wakihusishwa na kikundi cha al Shabab na tayari vyombo vyetu vya usalama vimekwenda kuwahoji na kupata taarifa zao rasmi, ikiwa ni pamoja na kuchukua alama za vidole kwa uchunguzi zaidi,” alisema jana. 

Nahodha alisema Tanzania inakabiliwa na tishio la ugaidi kutokana na baadhi ya raia wake 
kushiriki harakati za kikundi hicho kinachojihusisha na ugaidi na chenye uhusiano na kikundi kingine cha ugaidi cha al Qaeda. 

Al-Shabab ni kikundi cha Kiislamu cha Somalia kinachohusishwa na matukio ya ugaidi nchini Kenya ambapo pia kinadaiwa kushirikiana na mtandao wa al-Qaeda uliofanya shambulio la kigaidi nchini na Kenya mwaka 1998. 



Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Nahodha alisema wapo Watanzania waliokwenda kujiunga na mapambano yanayoendelea katika maeneo ndani ya Somalia. 

Alisema mpaka sasa kikundi hicho kimeishambulia Kenya zaidi ya mara tatu, hivyo ni vyema kwa Tanzania kuchukua hatua mapema ingawa ulinzi wa mipaka umeimarishwa. 

Aidha, alisema zipo taarifa zinazoonesha, kwamba kuna watu wanarubuni vijana wasio na kazi nchini, kwenda kuwatafutia kazi nchi za nje na hatimaye kuwapeleka kushiriki uhalifu wa al-Shabab nchini Somalia. 

Alisema upo uwezekano mkubwa wa baadhi ya makundi ya wahamiaji haramu kutoka Pembe ya Afrika, wanaoingia nchini wakiwa na uhusiano mkubwa na kikundi hicho na kuwataka madereva kuwa makini na wageni wanaotaka kufahamu maeneo muhimu kama ofisi za balozi na kuyapiga picha kutoa taarifa Polisi. 

Kutokana na viashiria hivyo vya wazi vya ugaidi, Nahodha alisema Serikali imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuvitaka vyombo vya Dola kushirikiana kufanya operesheni ya pamoja katika kupambana na ugaidi na maharamia na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mienendo ya wahalifu hao. 

Pia Nahodha aliwataka wananchi kutoa taarifa Polisi wanapoona wageni na wenyeji wananunua kwa wingi nyenzo za milipuko au wanapowaona watu wanawarubuni vijana kwenda kuwatafutia kazi nchi za nje. 

Aidha, aliwataka wamiliki na wafanyakazi wa hoteli na nyumba za kulala wageni wafuatilie taarifa za wageni wao, ili kuimarisha usalama wa nchi na hatimaye Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani. 

Katika hatua nyingine, Nahodha alisema anaendelea kusaka watu wanaojihusisha na biashara ya wahamiaji haramu, ili wachukuliwe hatua za kisheria na kuongeza kuwa yawezekana wahamiaji hao wanatumwa na kikundi hicho, ili kufanya tathmini ya nchi. 

Alisema kwa sasa anayafanyia kazi majina manane ya maofisa wa Uhamiaji ambao wanatuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo haramu na kuwapa mwezi mmoja wa kujirekebisha, vinginevyo atawachukulia hatua kali za kisheria. 

Kuhusu suala la Watanzania 21 wenye asili ya Zanzibar walioko Somalia, Waziri alisema wako katika harakati za kuangalia jinsi ya kuwarudisha, kwa kuwa wameongezeka kwa kuzaliana na wengi wao kuwa na familia kubwa. 

Watanzania hawa walikimbia Zanzibar Januari 2001 baada ya machafuko yaliyotokea kisiwani Pemba yakihusishwa na uchaguzi mkuu, ambapo wengine walikimbilia Shimoni, Mombasa 
, Kenya. 

Hivi karibuni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, alitoa hadhari ya kuwapo tishio la ugaidi kama ilivyotokea Kenya na uharamia unaojitokeza katika ukanda wa Bahari 
ya Hindi na kuwataka wananchi kuchukua hadhari na kutoa taarifa wanapoona watu au makundi wanayoyatilia shaka.


Habari Leo

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake