ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 7, 2011

Waziri ataka wanafunzi waandamane kuwadai wenzao waliokopa walipe

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
Peter Saramba, Arusha
NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo amewasihi  wanafunzi wa elimu ya juu nchini kuandamana ili kushinikiza waliokopeshwa fedha za elimu miaka ya nyuma walipe ili wapewe wengine.

Amesema wahitimu wengi walikopeshwa zaidi ya Sh21 bilioni  ili kusoma kwenye vyuo mbalimbali, lakini baada ya kupata kazi wanakwepa kulipa mikopo hiyo.

Mlugo alisema wanaosoma vyuoni sasa hawana budi kuandamana ili kuwashinikiza waliotangulia walipe fedha hizo ili ziweze kukopeshwa kwa wanafunzi wengine zaidi.


“Fedha hizo zilikopeshwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu tangu utoaji wa mikopo ulipoanza mwaka wa masomo wa 2004/05 na kama zitapatikana zitaiwezesha Serikali kukopesha wahitaji wengi zaidi kuliko idadi ya sasa”, alisisitiza.

Naibu Waziri Mulugo alisema hayo alipozungumza kwenye sherehe za mahafali ya Saba ya Chuo Kikuu cha Mount Meru eneo la Ngaramtoni, nje kidogo ya mji wa Arusha.

Alisema baadhi ya wanaodaiwa fedha hizi wamefanikiwa kupata ajira rasmi huku wengine wakijiajiri wenyewe baada ya Serikali kugharamia elimu yao kupitia mikopo ambayo sasa hawataki kurejesha.

“Tusiandamane (wanafunzi)  kudai mikopo kutoka bodi ya mikopo pekee, sasa tuandamane  pia kushinikiza waliokopeshwa sasa wanafanya kazi au kujiajiri warejeshe fedha walizokopeshwa ili ziingizwe kwenye mzunguko utakaowezesha wengi kufaidika,” alisema Mulugo akipigiwa makofi.

Alisema Serikali ina nia ya dhati kuhakikisha wote wanaofaulu na kupata sifa za kujiunga na elimu ya juu wanapata fursa hiyo bila kujali uwezo kiuchumi wa mhusika, wazazi au walezi wake, lakini lengo hilo linakwamishwa na kipato kidogo na changamoto nyingi zinazohitaji kushughulikiwa na Serikali akitaja uboreshaji wa huduma za afya, miundombinu na huduma zingine za kijamii.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Naibu waziri huyo, idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaokopeshwa imekuwa ikiongezeka kila mwaka wa masomo ambapo mwaka 2004/5 , Sh  9.9 bilioni zilitumika kuwakopesha wanafunzi 16,345 kabla ya idadi hiyo kuongezeka hadi kufikia wanafunzi 42,729 mwaka uliofuata.

Kuhusu maendeleo katika sekta ya elimu, hasa elimu ya juu, Naibu waziri huyo alisema nchi ilipopata uhuru mwaka 1961 kulikuwa na chuo kikuu kimoja pekee lakini sasa vipo vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 41, kati ya hivyo 12 vikiwa vy umma na 29 vya binafsi huku udahili ukiongezeka kutoka wanafunzi 14 kwa wakati huo hadi 155,757 kwa sasa.

Katika risala yao kwa mgeni rasmi, wahitimu 414 wa Chuo Kikuu cha Mount Meru waliishauri serikali kuwa pamoja na kuanzisha dawati la mikopo vyuoni, muda umefika wa kufikiria kuanzisha Ofisi za Kanda za Bodi ya Mikopo ili kurahisisha na kuongeza ufanisi kiutendaji.

Mwananchi

No comments: