ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 28, 2011

Anakupenda au anakutumia?-2


HERI ya Krismasi na Mwaka Mpya wapendwa marafiki ambao mmekuwa nami katika ukurasa huu kila wiki.
Bila shaka mlisherehekea vyema Sikukuu ya Noeli, Jumapili na sasa mpo katika maandalizi ya shamrashara za kuupokea mwaka mwingine.
Mada iliyopo mezani marafiki ni kama inavyoonekana hapo juu, ambapo leo nahitimisha.
Tunamwangalia mwenzi ambaye yupo na wewe kwa ajili ya kukutumia bila ya wewe kufahamu. Sifa zake ni zipi? Wiki jana tulianza, leo tunamalizia. Twende tukaone… 
Msiri
Ni mpenzi wako, lakini ni msiri kuliko kawaida, ni msiri wa mambo yake, lakini pia hataki uhusiano wenu ujulikane. Hata kama utamwambia unataka kujulikana na ndugu zake, hatakubali.

Anasingizia bado ni mapema wewe kwenda kwao.
Ni lini mwanamke akakataa mwanaume mwenye msimamo asijitambulishe kwao?
Hata kama unampenda sana, lakini unapoona alama hii lazima uwe makini.
Huenda alishapeleka msururu wa wanaume au tayari yupo au hakupendi tu! Umeona eeh!
Hukidhi viwango!
Hapa mwanamke wa aina hii hashindwi kukuonyesha dalili kwamba wewe siyo chaguo lake.
Mwanamke huyu ni mjanja sana na mwenye akili nyingi kwelikweli. Anapanga mipango yake taratibu, anaifanyia mazoezi kabla ya kuonyesha wazi.
Hapa atakuonesha kwamba huna viwango hasa vya kuwa naye, anaweza akamuona mwanaume fulani kwenye filamu, gazeti au jarida akamsifia.
Hata kama mmetoka pamoja, anaweza kumsifia mwanaume mwingine aliyepita karibu yenu.
Siyo ajabu kumsikia akisema: “Ah! Napenda sana wanaume warefu, yaani huyu kaka mh...” kama anasema maneno haya na wewe ni mfupi, maana yake huna sifa za kuwa naye, na anachokifanya ni kukuonyesha kuwa yupo na wewe kwa muda na wala hutakiwi kufikiria mipango ya baadaye.
Lakini pia, hashindwi kumsifia mwanaume ambaye ana rasta au ameweka nywele zake wave wakati wewe huna. Anafanya mambo haya ikiwa ni alama kwamba, hafikirii kuwa na wewe katika maisha yake badala yake anakula good time tu! 
Wewe si mume wake!
Kipengele kilichopita hakikinzani sana na hiki, mwanamke huyu anaweza kuzungumzia kuhusu kuolewa lakini siyo na wewe.
Mathalani, anaweza kusema: “Duh! Mwanaume atakayenioa, atakuwa na kazi sana.” Kauli hii huwa tata na mara zote haina maelezo mengine yoyote mbele yake.
Ni kweli anajua kwamba ataolewa siku moja, lakini wewe huna lako.
Anamuwaza mwanaume mwingine kabisa. Hata hivyo hawezi kukuambia moja kwa moja, atatumia tenzi, ngano na methali katika kufikisha ujumbe huu kwako.
Masharti yake hayaeleweki
Mwanamke huyu ni mjanja sana, anaonekana ana mambo mengi, ni kama hataki mapenzi yajulikane, lakini mbaya zaidi kwa kuwa anajua wazi kwamba hana mapenzi na wewe hataki umharibie!
Ana masharti kibao ambayo hayaeleweki.
Hapendi muongozane sana, hasa kwenye sehemu zenye watu wengi.
Hata kama ikilazimika kuongozana naye, anaweza kukuchagulia mahali pa kupita. Ukiona hivi, ujue unaibiwa!

Hana wivu
Hafikirii sana kuhusu kusalitiwa, hana muda na simu yako na wala haonyeshi dalili zozote za kujali sana penzi lako.
Hafikirii kwamba siku moja unaweza kumsaliti.
Hana muda huo.
Anaweza kukudhihirishia hili moja kwa moja, hata pale utakapokuwa umepanga kutoka naye, halafu ghafla akakuambia amepata dharura lakini atakupa rafiki yake uende naye kwenye pati.
Hili ni tatizo na ni lazima uwe nalo makini kwa kiwango cha mwisho.
Mwanamke ambaye hana wivu, kuna mapenzi kweli hapo? Hana shida na wewe na ndiyo maana basi hafikirii sana kuibiwa.
Iache akili yako itafakari hili kwa makini, mwisho utajua cha kufanya. 
Ratiba zake tata   
Ana mambo mengi sana ambayo hayaeleweki, pengine ana ratiba zake kabisa, lakini hakuweki! Yeye anawaza mipango yake yeye kama yeye na inawezekana kabisa, hujui ratiba zake na hajakuambia.
Hata kama alikuambia, siyo ratiba yake kamili.
Kimsingi hataki ufahamu kabisa juu ya mambo yake.
Hii nayo ni alama tosha ambayo itakufanya uelewe kwamba upo katika penzi la wizi.
Hakuna anayekupenda hapo.
ZINGATIO LA MWISHO
Mapenzi siyo kitu cha mchezo, umakini ni jambo la kwanza kabisa ambalo unatakiwa kuwa nalo katika uhusiano. Siku zinazidi kwenda mbele, sasa hakuna sababu ya kuendelea kupoteza muda kwa mtu ambaye umeshagundua kwamba hakupendi.
Hana malengo na wewe, hawazi kwamba unaweza kuwa wake wa maisha siku moja, wakati wewe ukiwaza hayo, mwenzako anawaza mambo mengine kabisa. Upo naye kwa ajili ya mapenzi ya dhati, mwenzio yupo kwa sababu ya kustarehe tu.
Upo tayari kuendelea kupoteza muda au kufanya maamuzi yaliyo sahihi na kuanza upya maisha yasiyo na maumivu? Uamuzi upo mikononi mwako.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.

No comments: