Wasamaria wakimsaidia mwathirika wa mafuriko baada ya kumuokoa akiwa amejishikilia kwenye mti ili asizame kwenye maji ya Mto Msimbazi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam. (Picha na Fadhili Akida)
HAIJAPATAkutokea. Ndivyo unavyoweza kuielezea hali iliyolikumba Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake jana baada ya mvua kubwa kuendelea kuitesa kwa siku ya pili mfululizo na kusababisha maafa makubwa yakiwemo ya vifo vya watu zaidi ya 15.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema mvua hiyo imevunja rekodi kwani ni ya kiwango kikubwa kisichofikiwa tangu mwaka 1954.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema mvua hiyo imevunja rekodi kwani ni ya kiwango kikubwa kisichofikiwa tangu mwaka 1954.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kwani mbali ya nyumba hasa zile za mabondeni kufunikwa kabisa na maji, madaraja kadhaa yalijaa maji na kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya upande mmoja na mwingine.
Miongoni mwa madaraja hayo ni ya Jangwani katika Wilaya ya Ilala ambalo linaunganisha sehemu kubwa ya Jiji na vitongoji vyake na linatumiwa na watu wengi kuingia katikati ya Jiji.
Lilifungwa kwa zaidi ya saa saba baada ya maji kujaa juu na katika maeneo yenye kuzunguka eneo hilo maarufu kwa viwanja vya michezo na makazi holela ambayo kwa miaka kadhaa sasa
yamekuwa yakisababisha maafa wakati wa mvua.
Daraja lingine lililosababisha adha kubwa kwa wakazi wa Jiji lililopo karibu na njiapanda ya Kawe katika Barabara ya zamani ya Bagamoyo, katika kituo cha daladala maarufu kama Bondeni.
Katika eneo la Mbezi Luis katika Barabara ya Morogoro, magari yalishindwa kufanya safari kwenda mikoani kuanzia saa tatu asubuhi baada ya daraja la Mbezi-Kibanda cha Mkaa kufunikwa na maji na kingo zake kung’olewa kabisa.
Daraja jingine lililoathirika ni Kigogo linalounganisha eneo hilo na Jangwani, ambako gari la Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji cha Jiji la Dar es Salaam, lilijaribu kupita na kujikuta
likikita kwenye daraja hilo na kuharibika.
Eneo la Kigogo Sambusa, pia daraja lilikuwa limefunikwa kabisa na maji. Idadi ya waliokufa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alisema watu watano waligundulika kufa kutokana na mvua hizo juzi na jana wamefikia 13, lakini idadi hiyo inaaminika ni zaidi
kutokana na baadhi ya matukio hayo ya vifo kutotolewa taarifa kwa mamlaka husika ikiwemo Polisi.
Waliokufa na kutambulika hadi kufikia jana ni Tulihama (65), mkazi wa Ubungo Msewe, Maganga Said (8), mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Kanjenje iliyopo Tabora,
aliyekufa baada ya kunaswa na waya wa umeme uliokatika kutokana na mvua katika maeneo ya Kiwalani Kigilagila.
Wengine ni Gathi Mseti (30) na mwanawe Thomas Rashid (8) wakazi wa Kipunguni B waliopigwa na radi katika eneo la Kiwalani Kigilagila, wakati wakitoka kuwatembelea ndugu
zao waishio Kurasini pamoja na mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Mkwawa, Vian Maxmilian (13) ambaye maiti yake ilikutwa ikiwa chini ya uvungu wa kitanda baada
ya nyumba yao kuanguka katika eneo la Mburahati.
Aidha, pia mtoto mdogo mkazi wa Luhanga, Magreth Makwaya (6), alisombwa na maji yaliyokuwa yanapita kwenye mfereji ambapo maiti hajaonekana hadi hivi sasa wakati
Ibrahim Lusuma (60), mkazi wa Ubungo Msewe maiti aliokotwa Sinza karibu na Shule ya Sekondari Iteba baada ya kusombwa na maji wakati alipotaka kuyakimbia mara baada ya
kuanza kujaa nyumbani kwake.
Pamoja na hao pia maiti ya mtoto mchanga ambaye hata hivyo jina lake halijapatikana hadi hivi sasa aliopolewa wakati alipokuwa akielea katika maji eneo la Mtogole, lililopo Tandale.
Katika eneo la Kigogo Darajani kwenye Bonde la Msimbazi, maiti wawili waliopolewa katika maji wote wanaume, ambapo mashuhuda walisema mmoja alikufa baada ya paa alilokuwa amejihifadhi kuvunjwa na maji na yeye kuzidiwa na kushindwa kujiokoa.
Mwingine alionekana akielea kwenye maji kwenye bonde hilo hata hivyo taarifa ya vifo vyao haikuweza kutolewa rasmi na Mkuu huyo wa Mkoa.
Taarifa kutoka eneo la Kimara Suca kwa Ndembo, zilieleza kuwa watu watatu, watoto wawili na mwanamke mmoja wamekufa baada ya ukuta wa nyumba jirani kuangukia nyumba waliyokuwa wamejisitiri mvua, baada ya ukuta huo kuloa maji na tope.
Maiti wamepelekwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani. Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema hadi jana jioni watu waliokufa ni 13, na uwezekano wa idadi hiyo kuongezeka ni mkubwa.
Hali halisi ilivyokuwa
Aidha, pia gari la Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji lilinusurika kuzama mtoni baada ya kuvunja kingo za Bonde la Msimbazi likiwa katika harakati za uokoaji.
Gazeti hili lilifika maeneo yaliyoathirika sana kama Kigogo (Darajani, Sambusa), Jangwani na
Mbezi Luis ambapo Jangwani barabara ilifungwa tangu saa nne asubuhi huku wanajeshi, polisi na wasamaria wakiokoa watu waliokuwa juu ya mapaa baada ya nyumba zao kufunikwa na maji.
Vifaa mbalimbali vya nyumbani vilionekana vikisombwa na kuelea juu ya maji. Miongoni mwa vifaa hivyo ni pamoja na majokofu, kontena, matangi ya maji, mabeseni na magodoro.
Baadhi ya watu wanasadikiwa kufa ndani ya nyumba zao kutokana na wengine kuonekana wakitoa mikono juu ya milango yao kuomba msaada.
Helikopta ya Polisi ni miongoni mwa vyombo vya moto vilivyoonekana kuokoa watu eneo la Jangwani.
Maji yalikuwa yakipita juu ya daraja huku mtoto mchanga akiokolewa baada ya kuelea kwenye beseni alikodaiwa kuwekwa na mama yake baada ya nyumba yao kujaa maji huku mtoto mwingine mwenye umri kati ya miaka minne hadi sita, akiokolewa na wasamaria waliomweka kwenye deli la kuuzia vinywaji baridi.
Kwa upande wa kampuni ya Wachina ya Kajima yenye ofisi zake Jangwani, ilifunikwa na maji na kupata hasara kubwa baada ya makontena mawili kuvunja ukuta na kupelekwa na maji huku watu wakijizolea mbao za kampuni hiyo zilizokuwa zikielea kwenye maji, Kituo cha Polisi cha Jangwani pia kilifunikwa.
Gazeti hili pia lilishuhudia watu wakiopoa meza, makochi, sahani, vibakuli, viti vya mbao, friji na seti za televisheni zilizokuwa zikielea juu ya maji na kukwama kwenye daraja la Jangwani huku boti binafsi kwa kushirikiana na askari Polisi na wanajeshi, zikiokoa watu walioita msaada
juu ya paa.
Watu walisikika wakisema, “Tulikuwa tunaona Indonesia kwenye televisheni sasa ipo kwetu kabisa, hii ni zaidi ya el-nino, Mungu aturehemu jamani,” huku wengine wakiilaumu Serikali kwamba imechelewa kuokoa watu na wengine wakiwanyamazisha kulaumu.
“Mnailaumu nini Serikali, itafanya mangapi, mara ngapi hawa watu wa Jangwani wameambiwa wahame, lakini hawasikii, mnataka Serikali ije imshike mtu mkono kumuokoa uhai wake mwenyewe?” Walihoji baadhi yao.
Wabunge Musa Zungu wa Ilala na Iddi Azzan wa Kinondoni, walionekana maeneo la Jangwani na Kigogo wakiwatuliza watu na kusimamia uokoaji. Mpaka saa 10 jioni jana, magari yanayotoka mjini kwenda Ubungo na yanayotoka Ubungo kuingia mjini, hayakuwa
yameruhusiwa tangu saa nne.
Zungu akizungumza na gazeti hili alisema, “Hali ni tete kama unavyoona, watu wengi bado wanasadikiwa wako ndani humo, maji yamejaa mpaka kwenye mapaa, tumeongea na Serikali wanasema Kikosi cha Ukoaji cha Jeshi kinakuja, ndiyo tunasubiri.”
Baada ya muda mfupi, magari mawili ya Polisi aina ya Land Rover Defender yenye namba za usajili PT 0880 na T213 AMV pamoja na ya Jeshi namba 2975JW04 ziliwasili na askari Polisi na wanajeshi kwa uokoaji.
Watu waliokuwa wakipeleka chakula kwa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni miongoni mwa watu walioonekana wakiwa na vyakula wakihangaika namna ya kuvuka upande wa pili bila mafanikio huku wengine wakirudi eneo la Magomeni.
Eneo la Kinondoni Mkwajuni ambako nyumba zilizo mabondeni zilishuhudiwa zikiwa zimefunikwa na maji isipokuwa paa pekee.
Baadhi ya paa za nyumba walionekana watu wakiwa juu wakisubiri kuokolewa. Zilishuhudiwa pikipiki za magurudumu matatu zikiwa zimepakia vifaa mbalimbali vya nyumbani kuashiria kwamba baadhi ya familia zilikuwa zikihama.
Abiria wa mikoani walionekana kujaa katika kituo cha basi cha Mbezi Mwisho huku mvua ikinyesha hali iliyosababisha foleni kubwa.
Magari yalianza kuruhusiwa kusafiri saa tatu asubuhi katika eneo hilo. Msaada kwa waathirika
Aidha, Mkuu wa Mkoa Sadiki alisema tayari kuna mahindi kilo 100 zitaanza kugawiwa kwenye vituo vya shule za msingi karibu na maeneo ya maafa pamoja na mahema ya kujihifadhi
kwa waathirika wakati hatua nyingine zikichukuliwa.
Aidha, alisema zimetengwa kambi maalumu katika maeneo mbalimbali ya Jiji kuwasaidia waliopatwa na matatizo hayo na kuzitaja kuwa Shule ya Sekondari ya Msimbazi, Shule ya
Msingi Mchikichini na Shule ya Msingi Muhimbili.
Kambi zingine ni Shule ya Sekondari na Msingi ya Kibasila, Gongolamboto, Mzambarauni huku akiwataka wananchi wenye mapenzi mema kuwasaidia waliopatwa na matatizo kwa kuwapa misaada mbalimbali wakati wa kipindi hiki kigumu kilichotokea.
TMA:Haijawahi kutokea
Kwa upande wake, Mamlaka ya Hali ya Hewa imesema leo pia mvua itanyesha ingawaje haitarajiwi kufikia kiwango kikubwa na kwamba katika sikukuu ya Krismasi itapungua na
kuwa katika kiwango cha kawaida.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Agnes Kijazi alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akitoa taarifa za hali ya hewa na kuongeza kuwa mvua iliyonyesha juzi na jana imefikia jumla ya milimita 216 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kwa muda mrefu.
Wastani wa mvua za kawaida kwa mwezi ni milimita 118. Kijazi alitolea mfano mvua iliyonyesha Desemba 15, 1999 kuwa ilikuwa ni milimita 110.3 na Desemba 16, 2006 milimita 108.
“Mwishoni mwa Septemba mwaka huu, TMA ilitabiri kuhusiana na mvua hizo, maeneo mengi yamepata mvua juu ya wastani na kwa mvua ya leo (jana) kwa Dar es Salaam hadi saa 3:00 asubuhi, ilikuwa milimita 156.4 wakati ile ya juzi ilikuwa milimita 60, huku kituo cha Kibaha mkoani Pwani kilipima mvua milimita 67.8,” alisema Kijazi.
Aidha, alisema mvua hizo zimetokana na kuongezeka kwa msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo na kusababisha makutano ya upepo katika eneo la
Mashariki na Kusini Magharibi mwa nchi.
Watu waliokufa Mara Mkoani Mara, watu wanne wamekufa maji wakiwemo watatu
waliosombwa na maji wilayani Bunda kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Robert Boaz, alisema watu wawili waliokuwa wakichunga ng’ombe walikufa maji baada ya kusombwa na maji wakati wakivuka mto Rubana, kwenda kutoa ng’ombe walioingia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Aliwataja watu waliokufa katika tukio hilo kuwa ni Marwa Maranya (25), raia wa Kenya na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Enock, ambaye umri na makazi yake hayajafahamika na kwamba wote kwa pamoja walikuwa wanachunga ng’ombe wa Kichera Nyamhanga mkazi wa
wilayani Bunda.
Alimtaja mwanamume mwingine aliyekufa kuwa ni Raphael Mahuta (63), mkazi wa Kijiji cha Hunyari, ambaye alikufa maji kutokana na kusombwa na maji baada ya mvua kubwa kunyesha
kijijini hapo.
Kifo cha nne ni cha mtu aliyekuwa amelewa chakari na kulala njiani, Seta Masoro wa Kijiji cha Sarawe.
Reli ya kati yafungwa Mkoani Dodoma, njia ya Reli ya Kati imefungwa kwa muda usiojulikana baada ya mvua kuharibu reli katika eneo la Gulwe wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
Hali hiyo ilisababisha abiria zaidi ya 1,500 waliokuwa wakisafiri kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam kukwama Stesheni ya Dodoma Mjini ambapo wamekuwa wakisubiri hatima yao tangu juzi usiku.
Kwa mjibu wa taarifa zilizopatikana kwenye Ofisi za Reli mkoani hapa, tayari abiria wameanza
kusafirishwa kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kwa njia ya mabasi.
Rais atuma salamu Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki kuomboleza vifo vya watu 13 ambao wamepoteza maisha katika mafuriko makubwa yaliyotokana na mvua ambazo zimekuwa zinanyesha tangu juzi.
Aidha, Rais Kikwete amempa pole Mkuu huyo wa Mkoa kutokana na uharibifu mkubwa wa nyumba, makazi na mali nyingine za wananchi uliosababishwa na mvua hizo ambazo pia zimesababisha uharibifu wa miundombinu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Kikwete pia ameuelekeza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kusaidiana na taasisi na vyombo vyenye uzoefu wa maafa kushirikiana katika
kuendelea kuokoa maisha ya watu, kusaidia waliozingirwa na mafuriko kuwahifadhi na kuwasaidia wale wote waliopoteza nyumba na makazi kutokana na mafuriko hayo.
Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Mkuu wa mkoa: “Chini ya usimamizi wako, ningependa kuona uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na taasisi na vyombo vyenye ujuzi na uzoefu wa kupambana na majanga na dharura za namna hii, kuhakikisha kuwa tunaendelea
kuokoa watu ambao bado wamezingirwa na mafuriko, tunawapa matibabu wale walioumia katika mafuriko hayo, na tunawahifadhi na kuwapa huduma za kibinadamu wote waliopoteza nyumba na makazi yao katika mafuriko hayo.”
Majira
No comments:
Post a Comment