ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 6, 2011

Kili Stars kufa au kupona leo

MSHAMBULIAJI wa Zanzibar, Amir Hamad Omary akigombea mpira na kipa wa Rwanda, Ndori Jean Claud wakati robo fainali ya Chalenji kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Rwanda ilishinda 2-1. Picha na Jackson Odoyo
Calvin Kiwia
KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Kilimanjaro Stars, Boniface Mkwasa amesema amekijaza nguvu mpya ya ushindi kikosi chake kitakachoshuka dimbani leo kupambana na Malawi (The Flames), katika mechi ya robo fainali Kombe la Chalenji Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huku pia akibeza kelele za zomeazome toka baadhi ya mashabiki na kusema hazitaathiri kampeni yao ya ushindi.
Tangu kuanza kwa michuano hiyo mwishoni mwa mwezi uliopita, Stars imekosa sapoti toka kwa baadhi ya mashabiki wake, huku pia ikivuka hatua ya makundi na kucheza robo fainali kupitia kapu la mshindi bora wa tatu (best loser), ikifungwa mara mbili na kushinda mara moja.
Kocha Mkwasa anatambua changamoto kubwa anayoipata kutoka mashabiki hao, lakini amesema amekifanyia marekebisho makubwa kikosi chake kilichopoteza dhidi ya Rwanda (1-0), Zimbabwe (2-1), na ushindi wa 3-1 (Djibouti) katika hatua ya makundi.
"Kimsingi hatufurahishwi nidhamu mbaya ya kutuzomea toka kwa mashabiki, lakini hili si tatizo--tumeiandaa timu vizuri kushinda mchezo wa leo.
"Tumefanya marekebisho ya msingi, imani yangu tutakwenda nusu fainali na kisha fainali," alisema Mkwasa ambaye mapema juzi aliwaondolea mbali kwenye kikosi chake wachezaji Haruna Moshi na Geofrey Taita kwa utovu wa nidhamu.

Stars inakutana na Malawi leo ikiwa ni mechi 14 tangu mwaka 1975, huku waalikwa Malawi wakishindi mara tano na Stars ikitoka kifua mbele mara tatu, na sare sita.
Nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Nurdin Bakari alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa wana kila sababu ya kuifunga Malawi na kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
"Nia, uwezo na nguvu za kuwafunga Malawi tunazo. Hatuna sababu ya kuongea sana kwa vile soka ni vitendo zaidi, nawaomba mashabiki wajitokeza kwa wingi kutushangilia," alisema Nurdin.
"Leo mtoto hatumwi dukani, kuzomewa katika soka ni jambo la kawaida, hilo nafikiri makocha wametueleza hakuna cha kuharibika," alisisitiza Nurdin.
"Wote tunafahamu umuhimu wa mechi ya leo, tumejiandaa tukitambua uwezo wa timu tunayokwenda kucheza nayo," alisema zaidi.
Stars ilitwaa ubingwa mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kuifunga timu ya taifa ya Ivory Coast bao 1-0 likiwekwa wavuni kwa kiki ya penalti ya nahodha wa wakati huo, Shedrack Nsajigwa.
Kabla ya mechi ya Stars, kutatangulia mechi nyingine itakayoanza saa nane mchana kati ya Uganda na Zimbabwe.

Rekodi Cecafa tangu 1975.
Makundi
1-11-1975 Malawi       3-1 Tanzania
7-11-1976 Tanzania     1-1 Malawi
1-12-1977 Malawi       0-0 Tanzania
17-11-1981Tanzania     2-2 Malawi
19-11-1982 Malawi       2-0 Tanzania
6-11-1988 Malawi       0-0 Tanzania
11-12-1990 Malawi       1-0 Tanzania
1992         Tanzania     1-1 Malawi
28-11-2006 Tanzania     2-1 Malawi
Nusu fainali
13-11-1979 Malawi       1-1 Tanzania
Marudio
14-11-1979 Malawi       4-0 Tanzania
24-11-1980 Tanzania     1-0 Malawi
1992        Tanzania B   1-0 Malawi 

Mwanachi

No comments: