ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 6, 2011

Mashallaaah Kili Stars

Kikosi cha timu ya Malawi kikiwa katika picha ya pamoja.
Kikosi cha timu ya Malawi kikiwa katika picha ya pamoja.(picha zote na FULL SHANGWE)
NI raha kwa Watanzania baada ya jana timu ya soka ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro 
Stars’ kuifunga Malawi bao 1-0 na sasa itakutana na Uganda katika nusu fainali kesho. 

Mchezo huo wa Uganda ‘The Cranes’ na Kilimanjaro Stars utakuwa marudio ya nusu fainali ya michuano hiyo mwaka jana, ambapo Stars ilishinda kwa mikwaju ya penalti. Stars ndio mabingwa watetezi. 

Bao hilo pekee la jana lilifungwa na Nurdin Bakari dakika ya 36 kwa shuti la mbali kutokana na pasi ya Mrisho Ngasa na kuamsha shangwe kutoka kwa mashabiki ambao kwa mechi zilizopita walikuwa wakiizomea timu hiyo. 

Hata mchezo wa jana, baadhi ya mashabiki wa Tanzania waligawanyika kabla ya mchezo kuanza, huku wengine wakiizomea timu, lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo walivyokuwa wakibadilika na kuanza kuiunga mkono timu. 

Licha ya kushinda mchezo huo, Stars ingeweza kuondoka na ushindi mnono zaidi kama ingetumia nafasi kadhaa ilizopata, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kulenga lango. 

Nayo Malawi ikiongozwa na mshambuliaji anayeongoza kwa kufunga kwenye ligi ya Malawi, Ismael Thindwa, ilipata nafasi kadhaa za kufunga lakini nayo ilikuwa butu. 

Dakika ya 78 Thomas Ulimwengu aliyeingia badala ya Hussein Javu alitengewa pasi nzuri na Ramadhan Chombo, lakini wakati akijiandaa kufunga mpira uliokolewa na mabeki.

Ngasa, Chombo na Ulimwengu mara kadhaa waliingia kwenye eneo la hatari, lakini walishikwa na vigugumizi vya miguu na kushindwa kumtungua kipa Charles Swin. 

Kwa upande wa Malawi ambayo ni timu mwalikwa kwenye mashindano hayo, wachezaji wake Ndaziona Chatsalira, Loti Chawinga na Philip Masiye waliingia eneo la penalti mara nyingi, lakini walipiga pembeni ya lango au kuokolewa na kipa Juma Kaseja. 

Katika mchezo wa awali jana, Uganda 'The Cranes' ilitinga nusu fainali baada ya kuifunga Zimbabwe bao 1-0, lililofungwa dakika ya 14 na Hamis Kiiza kwa kichwa. 

Wakati huohuo, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za kufunga michuano ya Chalenji Jumamosi. 

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa sherehe za ufungaji wa mashindano hayo zitafanyika Jumamosi wiki hii. 

Mashindano hayo yalishirikisha mataifa 10 wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa 
Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) na timu mbili mwalikwa.

Chanzo:Habari Leo

No comments: