ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 28, 2011

Mtoto afariki baada ya kukeketwa

Ngariba wa miaka 70, mkazi wa kijiji cha Irienyi Kinesi, wilayani Rorya, mkoa wa Mara, Nyaisanga Marwa, amekamatwa na Polisi na anatarajia kufikishwa mahakamni kujibu mashitaka ya kumkeketa mwanafunzi wa darasa la pili wa Shule ya Msingi Irienyi (jina tunalihifadhi) na kumsababishia kifo, baada ya kutokwa na damu nyingi kwenye sehemu aliyokatwa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, jana alisema kuwa, tukio hilo lilitokea Desemba 19, mwaka huu, katika kijiji cha Irienyi Kinesi, wilaya ya Rorya na kwamba baada ya mtoto huyo kukeketwa, alitokwa damu nyingi iliyoendelea kutoka bila msaada wowote kwa matumaini kuwa atapona kwa miti shamba.

Kamanda huyo alisema, Desemba 23, mwaka huu, mtoto huyo (9) alipoteza maisha na kwamba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na ndugu wa marehemu walimkamata ngariba huyo kabla hajatoroka na hadi sasa yupo mikononi mwa Polisi na wanatarajia kumfikisha mahakamani wakati wowote kujibu shitaka la kukeketa na kusababisha kifo.
MTOTO ANUSURIKA KUOZWA
Katika tukio lingine, mtoto wa darasa la nne katika shule moja ya msingi jijini Dar es Salaam ambaye ni yatima, amenusurika kuozwa kwa nguvu na baba zake wakubwa, ili zipatikane ng’ombe za kumwezesha kaka yake kuoa.
Tukio hilo llitokea hivi karibuni baada ya mwanafunzi huyo kwenda na mlezi wake kwenye msiba wa mama yake katika kitongoji cha Nyamoko, kijiji cha Mahanga, kata Mihingo, Tarafa ya Chamriho, wilayani Bunda, mkoa wa Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Francis Isack, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) alinusurika kuozwa na baba zake wakubwa baada ya mlezi wake kutoa taarifa kwake kuhusiana na mpango huo.
Isack alisema kuwa, mama mzazi wa mtoto huyo alifariki Desemba 10, mwaka huu na kufanyiwa mazishi kijijini hapo na kuongeza kuwa mtoto huyo alifuatana na mlezi wake, Noela Haruni Chacha, mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Mkuu huyo wa wilaya alifafanua kuwa mtoto huyo alinusurika kuozwa kwa nguvu, baada ya mlezi wake kutoa taarifa ofisini kwake.
Alisema baba zake wakubwa wanataka kumuoza kwa mwanaume kijijini hapo ili zipatikane ng’ombe za kumwezesha kaka yake kuoa, kwani hadi sasa hajaoa kutokana kukosekana kwa ng’ombe.
Aliongeza: “Kufuatia hali hiyo, nilimwagiza Kaimu Katibu Tarafa wa tarafa hiyo kufuatilia tukio hilo.”
 Hata hivyo, Isack, alisema kwa sasa hawezi kuchukua hatua dhidi ya watu hao, kwa sababu hakuna ushahidi wa kutosha wa kuwapeleka mahakamani, lakini alisema lazima wafike ofisini kwake ili waohojiwe kutoa maelezo.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Tarafa ya Chamriho, Juma Mkami, alisema baada ya kufuatilia aligundua kilichoelezwa ni kweli, kwani baba zake wakubwa walimkatalia asirejee jijini Dar es Salaam kuendelea na masomo yake.
Alisema wazazi hao walisema kuwa, wameshamwandalia mwanaume wa kumuoa kwa lengo la kupata mahari ili imwezeshe kaka yake kuoa.
“Watuhumiwa walitaka kumkatalia mtoto huyo asirudi Dar es Salaam, nilitumia sauti ya serikali ya ukali kidogo ndipo wakanipatia na leo hii (jana) nimempeleka kwa DC ambaye amesema kesho asubuhi mlezi wake aende akamchukue,” alisema.
Mkami aliongeza: “Na nimewaita hao baba zake wakubwa nao waje ili watoe maelezo kwa DC.”
Alisema kuwa tayari jana alimkabidhi mtoto huyo kwa DC na kwamba mlezi wa mtoto huyo leo asubuhi ataitwa kukabidhiwa mtoto huyo ili arejee naye Dar es Salaam kuendelea na masomo.
Aliongeza kuwa watuhumiwa hao pia wametakiwa leo asubuhi wafike ofisini kwa mkuu wa wilaya.
Kwa mjibu wa Mkami, wakati wakimhoji mtoto huyo, alisema anataka shule na si kuolewa kama ndugu zake wanavyotaka na kwamba kwenye darasa lao lenye watoto zaidi ya 100, amekuwa akishika nafasi ya kwanza, ya pili na ya tatu kwenye mitihani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: