ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 22, 2011

Ngeleja: Wauza mafuta wafungwe gerezani

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja
James Magai
SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) iwachukulie hatua za kisheria, wafanyabiashara wa mafuta waliosababisha kuwapo kwa uhaba wa nishati hiyo na amependekeza wafungwe gerezani.Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alitoa agizo hilo kwa Ewura jana wakati akizungumza na viongozi na wawakilishi wa kampuni za kuuza mafuta nchini jana jijini Dar es Salaam kuhusiana na tatizo la uhaba wa mafuta lililojitokeza wiki hii.

Mapema wiki hii, upatikanaji wa nishati hiyo ilikuwa tete baada ya baadhi ya wauzaji kuficha mafuta kufuatia hatua ya Ewura kutangaza bei elekezi na mafuta kushuka kwa Sh100.Ngeleja alisema licha ya kuwapo uhaba huo kuna akiba yakutosha ya mafuta nchini inayoweza kutumika kwa muda zaidi ya siku 30.
 “Upungufu huo ulikuwa ni wa makusudi uliofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasiyo waaminifu. Baadhi yao waliacha kununua mafuta kutoka kwa wauzaji wakubwa wakisubiri bei kushuka, matokeo yake imeathiri sana uchumi wa nchi.

“Kitendo cha uhaba wa bidhaa hiyo vituoni ni kuwahujumu wananchi," alisema Ngeleja.Alisema wafanyabiashara hao wamekuwa wakiichezea serikali na kwamba sasa umefika wakati wa serikali kuchukua uamuzi mgumu dhidi yao.“Sheria imewapa Ewura uhuru wa kudhibiti kasoro hizi na wigo mpana wa adhabu kama vile kuonya, kuwasimamisha na kuwafutia leseni, hivyo chukueni hatua,wasimamisheni au wafutienikabisa leseni.
Siyo wote, wako wafanyabiashara waaminifu, lakini hawa wakorofi lazima tuwafungie au tuwafute kabisa.

Najua wengine mmechukua mkopo benki na wengine mmeajiri watu wengi, lakini sasa umefika wakati wa serikali kuchukua uamuzi mgumu," alisema.Alisema adhabu ambazo Ewura imekuwa ikizitoa kwa wafanyabiashara wakorofi kama vile kuwatoza faini ya Sh3 milioni haitoshi na kwamba badala yake wanastahili kufungwa.Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Kanuni za Sheria ya Ewura za mwaka 2009, mtu anayesababisha usumbufu wa kupatikana kwa mafuta bila sababu za msingi, anafanya kosa la jinai.
"Miongoni mwenu mnafanya makusudi ili kupata faida ya kinyonyaji au kuyumbisha nchi, hivyo huo ni uhujumu wa nchi na usumbufu kwa wananchi.

"Najua mtaniita majina yoyote mkitoka hapa, lakini nasema hapa kuna watu wanastahili kufungwa. Sipendi kuwaona watu wakifungwa, lakini hawa wanataka kufungwa na bila kufungwa nchi haiendi."Mmewahurumia sana kwa kuwaandikia maonyo, lakini sasa hawa lazima wawe washtakiwe, hakuna sababu ya kuendelea kuwasamehe,” alisisitiza Waziri Ngeleja.

Alisema kumekuwa na maneno kwamba baadhi ya vigogo wa serikali wamekuwa wakishawishi wafanyabiashara hao wasichukuliwe hatua kali, lakini akawataka wawataje vigogo hao.
 “Anayesema ameiweka serikali mfukoni aseme. Siko hapa kuwatisha na wala sijalewa. Msidhani  serikali iko hapa kucheza. Tukiwafunga miongoni mwenu mtapata adabu.
"Mmetuchezea sana, lakini sasa ni mwisho, Tunajua mna nguvu ya kifedha, lakini mjue kuwa fedha siyo kila kitu. Mimi sitaondoka hapa mjini nitaendelea kuwapo na nitakuwa msitari wa mbele kupambana na wakorofi,” alisisitiza Waziri Ngeleja.

Alisema ingawa anatambua mchango wa wafanyabiashara hao katika kuchangia kukuza uchumi wa nchi kupitia kodi mbambali wanazaozilipa, lakini akawapasha kuwa wasidhani kuwa bila wao nchi haiwezi kwenda.

Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu alimwakikishia Waziri Ngeleja kuwa agizo lake litatekelezwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.Waziri Ngeleja alitoa fursa kwa wadau hao kutoa maoni na mapendekezo yao ili kurekebisha kasoro katika biashara hiyo.

Mkurugenzi wa MOIL, Alkarim Hiran aliishauri Ewura isitangaze bei mpya za nishati hiyo mwishoni mwa wiki ili wafanyabiashara wasio waaminifu wasipate nafasi ya kufanya udanganyifu.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mtendaji wa Mangala Farm Company Ltd, Francis Noni alishauri mfumo wa kurekebisha bei mpya, ufanyiwe marekebisho badala ya kurekebisha kila baada ya majuma mawili ili iwe mwezi mmoja.

Waziri Ngeleja na Masebu kwa nyakati tofauti walisema mapendekezo hayo tayari yameanza kufanyiwa kazi.Akizungumzia mafanikio ya kuwapo kwa Ewura, Masebu alisema Ewura wamesaidia mlaji baada ya kuokoa Sh600 kwa kila lita ya mafuta wanayonunua.

Kwa mujibu wa takwimu za Ewura, mafuta aina ya Petroli yanatosha kwa matumizi ya siku 33, dizeli siku 32 na mafuta ya taa ya  siku 38. Ewura ilisema kwa siku nchi nzima inatumia lita  875,000 za petroli, lita 3,100,000 za dizeli na lita 615, 240 za mafuta ya taa.

Mwananchi

No comments: