ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 17, 2011

Simba yasajili 28 CAF

  Kaseja nje wiki mbili
Juma Kaseja
Uongozi wa klabu ya Simba umesema kuwa unatarajia kuwasilisha majina ya wachezaji wake 28 katika Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ambao watawatumia katika mechi za mashindano ya Kombe la Shirikisho yatakayoanza kufanyika kuanzia mwezi Februari mwakani.
Simba iliyomaliza msimu uliopita wa ligi 2010/ 2011 ikiwa katika nafasi ya pili itaanza kuwania ubingwa wa mashindano hayo kwa kuivaa Kiyovu ya Rwanda jijini Kigali na kurejeana Machi 4 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa viongozi wa klabu hiyo alisema kwamba wako katika hatua za mwisho za kukamilisha zoezi hilo ili wayapeleke majina hayo kwenye Shirikisho la Soka Nchini (TFF) ili wayatume CAF kama taratibu zinavyoeleza.

Kwa mujibu wa chanzo cha gazeti hili baadhi ya wachezaji ambao wataipeperusha bendera ya Simba kwenye michuano hiyo ni pamoja na Juma Kaseja, Ally Mustapha 'Barthez', William Mweta, Juma Jabu, Kelvin Yondani, Juma Nyosso, Shomari Kapombe, Derick Walulya, Uhuru Suleiman, Haruna Moshi 'Boban', Emmanuel Okwi, Mwinyi Kazimoto na Gervais Kago.
Wachezaji wengine ni Patrick Mafisango, Victor Costa, Felix Sunzu, Salum Machaku, Obadia Mungusa, Ibrahim Rajab na Said Nassor 'Chollo.
Pia Simba inatarajiwa kuyapeleka CAF majina ya nyota wake iliyowapandisha kutoka katika kikosi cha mabingwa wa mwaka huu wa mashindano ya Kombe la Uhai, Simba B, ambao ni pamoja na Ramadhani Singano 'Messi', Edward Christopher, Frank Sekule, Abdallah Seseme, Jonas Gerald na Hassan Rajab.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa mwaka huu wamepanga kuwasilisha majina hayo mapema kama CAF ilivyoeleza ili

INATOKA UK. 24
waweze kuendelea na maandalizi mengine ya mzunguko wa pili na michuano hiyo ya kimataifa.
"Wakati wowote tutakitangaza kikosi chetu lakini hakitakuwa na mabadiliko sana, zaidi ni wale vijana wetu tuliowapandisha," alisema Kamwaga.
Katika kujiandaa na mashindano hayo, Simba iliamua kumrejesha kocha wake wa zamani Mserbia Milovan Cirkovic akiongoze kikosi hicho na kuachana na Mganda Moses Basena.
Mbali na Simba, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga wao watachuana katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na mechi yao ya kwanza itakuwa hapa nyumbani dhidi ya Zamalek kutoka nchini Misri kati ya Februari 17 na 19.
Wakati huo huo, kipa namba moja wa Simba, Juma Kaseja atakuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili baada ya kuumia kifundo cha mguu.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema Kaseja aliumia akiwa na timu ya taifa ya Tanzania bara 'Kilimanjaro Stars' wakati ikishiriki kwenye mashindano ya Kombe la Chalenji yaliyomalizika wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kamwaga alisema kuwa baada ya mashindano hayo kumalizika, daktari wa Simba, Cosmas Kapinga alimfanyia uchunguzi Kaseja na kugundua kuwa ameumia kifundo cha mguu na hivyo anatakiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki mbili.
"Wachezaji wengine wanaendelea na mazoezi kama kawaida isipokuwa kwa Kaseja ambaye yeye atakuwa nje kwa angalau wiki mbili," alisema Kamwaga.
Aidha, alisema kuwa uongozi wa timu hiyo umempa mapumziko ya siku saba mshambuliaji wake Emmanuel Okwi ambaye ataanza mazoezi wiki ijayo.

CHANZO: NIPASHE

No comments: