ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 22, 2011

Wanafunzi walazimika kulala msikitini kwa kukosa mabweni



Wanafunzi 100 wa Chuo cha Ufundi cha Kengeja Pemba, wanalala msikitini kutokana na ukosefu wa nafasi katika mabweni.
Wanafunzi hao ni kati ya wote 156 wanaochukua mafunzo mbalimbali ya fani za ufundi kutoka Zanzibar.
Mjumbe wa Kamati ya Ustawii wa Jamii, Wanawake na Watoto ya Baraza la Wawakilishi (BLW) Jaku Hashim Ayoub, alisema wanafunzi hao wanalala msikitini na wengine kwenye jiko la chuo hicho kwa muda wa miaka miwili sasa.
Hakueleza uamuzi wa wanafunzi hao kutafuta hifadhi katika msikiti huo lakini habari zinaeleza kuwa baada ya kuona tatizo uongozi wa msikiti umeamua kutoa msaada huo.

“Wanafunzi wanalazimika kulala msikitini chuo kina mabweni mawili yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 56 tu,” alisema Jaku ambaye pia Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni.
Chuo cha Ufundi Kengeja kinamilikiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ni miongoni mwa vyuo vikongwe visiwani humo.
Jaku alisema mbali ya ukosefu wa huduma za malazi, kamati yake pia imebaini kuwa chuo hicho kina tatizo kubwa la ukosefu wa mifereji ya maji machafu jambo ambalo linatishia afya ya wanafunzi na jumuiya ya chuo hicho kwa ujumla.
Alisema walimu pia hufanya kazi katika mazingira magumu kutokana na ukosefu wa vifaa vya kufundishia kwa njia ya vitendo na pia upungufu wa walimu.
Jaku alisema kamati hiyo ipo Pemba kukagua huduma za serikali katika wizara tatu za SMZ ikiwemo ya elimu, afya na wanawake na watoto.
Alisema tatizo lingine linalowakabili wanafunzi wa chuo hicho ni ukosefu wa chakula.
“Wanafunzi hupata mlo mmoja kwa siku, serikali imeacha kabisa kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi wote,” alisema Hija.
SMZ iliamua kuondoa utaratibu wa huduma ya chakula kwa wanafunzi katika shule za bweni na vyuo kwa zaidi ya miaka minne sasa.
Hata hivyo, alisema hali katika chuo ni mbaya na kushauri serikali kurudisha utaratibu kwa kutoa huduma ya chakula katika shule za bweni na vyuo vyote nchini.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamad, alikiri chuo hicho kukabiliwa na ukosefu wa mabweni ya kukidhi mahitaji ya wanafunzi.
Alisema serikali imekuwa ikichukua hatua za kuondoa tatizo la ukosefu wa malazi pamoja na mengine lakini kutokana na ufinyu wa bajeti matatizo hayo bado hayajapatiwa ufumbuzi.
Alisema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na matengenezo kwa upande wa ukarabati wa maeneo mbalimbali ya chuo hicho.
Pamoja na kukagua Chuo cha Ufundi cha Kengeja, kamati ya Hija, pia imekagua shule ya Sekondari ya Kengeja na kupendekeza ifungwe kutokana na uchakavu wa majengo yake.
CHANZO: NIPASHE

No comments: