Advertisements

Monday, January 2, 2012

Afsa uhamiaji azua rabsha, atiwa mbaroni

 Adaiwa kumpiga mwanamke raia wa DRC
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma linamshikilia afisa uhamiaji mkoani humu, Rogastian Rukoo, kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Stella Kale (25).

Stella amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni kutokana na kipigo hicho ambapo inadaiwa kuwa mtuhumiwa alimpiga makofi usoni na mateke mbavuni hadi kuzimia kwa madai kuwa hana dola 100 za viza kwa ajili ya watoto wawili mmoja mwenye umri wa miaka saba na mwingine ana umri wa mwaka mwaka mmoja na nusu.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 8:00 mchana eneo la mwalo wa Kibirizi katika Manispaa ya Kigoma, baada ya kuteremka kwenye boti ambayo ilikuwa ikitokea Kalemii, DRC.
Akizungumza na NIPASHE, mume wa Stella, Bedi Zakwame, alisema: “Mimi ninakaa Nairobi, nimekuja kutembea hapa Kigoma wakati huu wa sikukuu ya mwaka mpya, nikaona sio vema mimi kula sikukuu peke yangu. Hivyo nikamuita mke wangu Stella pamoja na watoto wangu wawili mmoja ana miaka saba na wa pili ana mwaka mmoja na nusu ili tuuone mwaka mpya pamoja na familia yangu.”


Zakwame alisema mkewe alitokea Kalemii akiwa na vibali vyote na kwamba alipofika Kibirizi Desemba 31, mwaka jana saa 8:00 mchana, alimkuta akimsubiri na baada ya Stella kuteremka walikwenda katika ofisi ya Uhamiaji Kibirizi.
Alisema baada ya kufika walielezwa kuwa na watoto wao wanatakiwa walipe viza ambayo ni dola 50 za Marekani kwa kila mtoto ndipo alipomwambia afisa uhamiaji kuwa anakwenda mjini kuchukua fedha ili alipe dola 100 na kumkubalia.
“Mimi nikampa mke wangu dola 60 na nikamwambia anisubiri hapa hotelini wakati anapata chai, kisha nikaondoka na mtoto mmoja wakati yule mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu akabaki na mke wangu,” alisema.
Zakwame alisema aliporudi kutoka mjini, alikuta umati mkubwa wa watu ukiwa umezunguka kituo kidogo cha polisi Kibirizi na aliposhuka kwenye teksi  aliambiwa kuwa mkewe  amezimia kwa kupigwa na Afisa Uhamiaji, Rogastian Rukoo, makofi usoni na mateke mbavuni hadi kazimia.
Akizungumza na NIPASHE katika wodi namba 5 ya Hospitali ya Maweni, Stella alisema: “Kilichofanya anipige makofi na mateke huyu afisa uhamiaji ni baada ya mume wangu kuondoka kwenda mjini naye akanitongoza lakini mimi nilikataa na kumwambia kuwa hana aibu kwani mume wangu ameondoka tu naye anaanza kunitongoza. Mimi nilimkataa na ndipo aliponiambia kuwa kama sina jibu leo hii basi atanirudisha Congo. Hapo ndipo alipoanza kunipiga makofi usoni na mateke mbavuni hadi nikazimia.”
Shuhuda wa tukio hilo, Jumanne Mussa, mkazi wa Kibirizi, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4:00 asubuhi: “Mimi nilikuwa nimekaa hapa ziwani kwenye mchanga nikaona ghafla afisa uhamiaji anampiga Mkongomani makofi usoni na mateke mbavuni hadi akazimia.”
Aliongeza: “Baada ya kuzimia, wananchi waliokuwepo walimkimbiza afisa uhamiaji ili naye wampige lakini bahati yake alikimbilia kituo cha polisi Kibirizi kujisalimisha, baada ya hapo wananchi wakamchukua Mkongomani na kumpeleka Hospitali ya Maweni kwa matibabu.”
Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Adoroth Milinga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtembelea Stella wodi namba tano alikolazwa. Alikuwa amefuatana na Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibirizi, Inspekta Omari Diwani.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa polisi wanafanya uchunguzi wakati mtuhumiwa anashikiliwa.
Alisema uchunguzi utakapokamilika mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: