ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 30, 2012

Hamad Rashid atikisa Pemba

Aziza Masoud, Pemba
MBUNGE wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed ambaye alitangazwa kuvuliwa uanachama na chama chake, jana alipokewa kwa mbwembwe na kuimarishiwa ulinzi alipowasili Pemba. Msafara wake uliongozwa na magari manne ya polisi yakiwa na ving'ora na askari takriban 30.

Hamad amefungua kesi Mahakama
Kuu akipinga uamuzi wa chama chake kumvua uanachama huku akiitaka iwatie hatiani viongozi wakuu wa chama hicho akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharrif Hamad kwa tuhuma za kukiuka amri ya Mahakama.

Jana, Hamad aliwasili Uwanja wa Ndege wa Chake Chake, Pemba saa 5:45. Baada ya kushuka katika Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), alipokewa na mamia ya mashabiki wake waliokuwa wakiimba: “Anamereta...,”

Wengi wa mashabiki hao walikuwa wamevaa fulana nyeusi zilizoandikwa ‘Anti Virus’ na mara baada ya kuteremka katika ndege hiyo, alitumia takriban dakika 20 kusubiri kutoka nje ya uwanja katika kile kilichoelezwa na uongozi wa uwanja huo kuwa ni kuandaa mazingira ya usalama kutokana na umati mkubwa wa watu uliokuwa umekwenda kumlaki.

Mbali na ulinzi huo wa polisi, mapokezi hayo yalikuwa na zaidi ya pikipiki 85, magari 30 na umati wa watu. Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida wananchi hao waliimba nyimbo mbalimbali bila kukitaja CUF kama ilivyozoeleka.

Nyimbo zilizokuwa zikiimbwa katika mkusanyiko huo zilikuwa ni za sifa kwa mbunge huyo... “Hamad anameremeta... tumpambe maua... Hamad ni nuru ya Wawi... hao vibua macho wanataka kushindana na Hamad hawawezi haoooo na mwingine ukisema Maalim Seif, Serikali ya mseto haikufanya kitu, tunataka mabadiliko.”

Ilipotimu saa 6:15, msafara wake ulielekea hadi katika Uwanja wa soka wa Ditia, ulioko katika Jimbo hilo la Wawi ambako Hamad alihutubia. Hata hivyo, tofauti na ilivyokuwa siku za awali, hakuna bendera ya CUF iliyokuwa ikipepea mbali na ile ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza katika mkutano huo, Hamad alisema alishaambiwa na baba yake kwamba atapambana na ugumu katika maisha ya kisiasa kwa kuwa anasimamia haki na ukweli.

“Marehemu baba yangu aliniambia katika siasa yatakukuta mambo manne ambayo ni kufukuzwa katika chama, fitina na mwenzangu aliyeshika mpini, kuwekwa ndani na kupigwa risasi katika hayo yote yameshanitokea kasoro moja la kupigwa risasi,” alisema Hamad.

Alisema Maalim Seif akisema ndiye chanzo cha migogoro yote ndani ya chama hicho: “Namuheshimu sana Maalim lakini uvumilivu umenishinda dhambi tuliyoifanya kubwa wanachama wa CUF ni kumfanya Maalim Seif kama malaika hana dhambi na hakosei kitu chochote na harekebishwi na wanachama wengine.”

“Kama yeye ni hodari wa kutoa taarifa, aje atoe sababu ya kuweka mageti ya kuzuia kuingia karafuu katika barabara zote wakati aliahidi katika kampeni kwamba biashara ya zao la karafuu itakuwa huru. Anashindwa kupita kwenye njia zake alizoziahidi, anatumia nafasi yake kuharibu chama na kupandikiza chuki kwa watu.”

Mmoja wa wakazi wa Wawi, Khamis Baharani alisema wakazi wengi wa jimbo hilo wamestushwa na kufadhaishwa na uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF wa kuwafukuza wanachama watatu na wengine wanane kupewa karipio bila wao kushirikishwa.

Baharani alisema Hamad ni mbunge wao na kwamba wanaamini  amefanya mambo mengi ya maendeleo na mazuri katika utumishi wake jimbo ni kwao hivyo ingekuwa vyema wakashirikishwa katika hatua hiyo kubwa iliyochukuliwa dhidi yake.


Mwananchi

No comments: