ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 25, 2012

Mabomu ya kutoa machozi yasambaratisha wanafunzi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala,
Faustine Shilogile
Wanafunzi wa Shule tatu za msingi na sekondari zilizopo Kata ya Kipawa jijini Dar es Salaam, wamelazimika kusitisha masomo yao na kurudishwa nyumbani kabla ya muda unaotambulika kisheria, baada ya Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuwapiga mabomu ya kutoa machozi.

Katika tukio hilo ambalo lilitokea jana saa 3:30 asubuhi, lilisababisha mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Majani ya Chai, Maria Alfred (16), kupata mshtuko na kupoteza fahamu.
Mwanafunzi huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Amana kwa matibabu.
Wanafunzi waliopigwa mabomu na polisi hao ni wa Shule za Msingi na Sekondari Majani ya Chai na Shule ya Sekondari Ilala.


Aidha, vijana wanaofanya biashara ya kuponda kokoto na kuuza, pia waliathiriwa na mabomu hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema polisi walikwenda maeneo ya jirani na shule hizo kwa lengo la kukamata vibaka ambao huwapora watu vitu mbalimbali.
“Sina taarifa za wanafunzi kupigwa mabomu, lakini namtuma OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) kwenda eneo la tukio na baada ya hapo nitatoa taarifa kamili,” alisema Kamanda Shilogile.
 Baadhi ya watu wanaoishi jirani na shule hizo walieleza kuwa chanzo cha vurugu hizo zilizoanza tangu juzi, ni kujengwa kwa ukuta na kuzuia barabara iliyokuwa inatumiwa na wakazi wa eneo la Kipawa.
Kufuatia kuzibwa kwa barabara hiyo ambayo pia ilikuwa ikitumiwa na wanafunzi wa shule hizo, kuliamsha hasira kwa wakazi wa eneo hilo ambao waliamua kuchukua hatua za kubomoa ukuta huo.
Baada ya ukuta huo kubomolewa ili kurejesha njia iliyokuwa inatumiwa na wananchi tangu awali, mmiliki wa kiwanja hicho namba 135 alikwenda kutoa taarifa polisi.
Jana polisi walifika eneo hilo na kuanza kuwakamata vijana wanaouza kokoto, lakini katika purukushani hizo, ndipo polisi walipoanza kufyatua mabomu ya kutoa machozi na kusababisha wanafunzi wa shule hizo kukimbia hovyo na mmoja wao kupoteza fahamu.
Kutokana na hali hiyo, uongozi wa shule hizo uliamua kuwaruhusu wanafunzi kurejea nyumbani saa 4:00 asubuhi kabla ya muda wa kawaiada wa kutoka saa 11:00 jioni kutokana na hofu ya wanafunzi zaidi kuathirika na mabomu.
Mkuu wa Shule ya Sekondali Ilala, Anna Selasini, alisema aliamua kuruhusu wanafunzi kutoka shuleni kabla ya muda kwasababu ya kuogopa mabomu yasije yakawadhuru wanafunzi.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Said Mtipa, alisema njia hiyo wamekuwa wakiitumia tangu mwaka 1980 wakati eneo hilo likimilikiwa na raia mwenye asili ya kiasia aitwaye Chavda.
Diwani wa kata ya Kipawa, Bonah Kilua, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba yeye pamoja na Ofisa Mtendaji wa kata wametuhumiwa kuchochea vurugu hizo na kwamba wametakiwa kwenda polisi kutoa maelezo.
“Mimi nipo kwenye kikao, lakini nikitoka hapa nakwenda polisi kituo cha Sitakishari kuandika maelezo kwani nami ni mtuhumiwa,” alisema diwani huyo.
Kwa upande wake, mmiliki wa kiwanja hicho, Mohamed Kilua, alisema alianza kumiliki eneo hilo tangu mwaka 2006 na anavyo vielelezo vyote.
Pia alisema hakuna njia inayopita eneo hilo.
Kilua alisema Januari 18, mwaka mwaka huu, alipewa kibali cha kujenga ukuta huo chenye namba 10138, lakini baada ya kuanza kujenga, viongozi wa kata walianza kuwahamasisha wananchi wa eneo hilo waubomoe.
Hata hivyo, mmiliki wa kiwanja hicho alikataa madai yanayotolewa na wakazi wa eneo hilo kwamba alikodi polisi na mabaunsa kwenda kupiga mabomu eneo hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: