
Baada ya kutimuliwa madaktari 229 waliokuwa wakifanya mazoezi ya vitendo kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), hospitali hiyo imewaleta madaktari wapya kutoka sehemu mbalimbali nchini ili kuziba nafasi zao.
Aidha, uongozi wa Muhimbili umepinga vikali kuwa vifo vya wagonjwa vimeongezeka kwenye wodi za hospitali hizo kutokana na kuondolewa kwa madaktari hao, ambapo umeeleza kwa kipindi hicho vifo vimepungua.
Afisa Uhusiano Msaidizi wa Muhimbili, Jezza Waziri, alisema wakati madaktari hao wametakiwa kuondoka kurudi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kupangiwa kwenye hospitali zingine, hakuna athari yoyote kubwa iliyotokea baada ya nafasi zao kuzibwa haraka.
Alisema katika kujipanga huko, madaktari bingwa na wale wa kawaida wanafanya kazi zilizokuwa zikifanywa na madkatari hao ambao kwa sasa wanatakiwa kurudi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kupangiwa hospitali zingine.
Hata hivyo, imebainika moja ya hatua iliyochukuliwa katika kuziba upungufu huo ambayo Afisa habari huyo hakutaka kuigusia, ni kuwaleta madaktari wengine.
Katika kudhihirisha jambo hilo, wakati waandishi wa habari walipotembelea kitengo cha wagonjwa wa dharura kuona utendaji wa kazi, walielezwa kitengo hicho kimepokea madaktari 12 na wameanza kufanya kazi.
Pamoja na Waziri kutokuwa tayari kutaja idadi ya madaktari walioletwa hospitalini hapo, lakini Profesa Victor Mwafongo, Mkuu wa Idara hiyo alithibitisha kuwapokea madaktari hao.
“Profesa Mwafongo umemsikia mwenyewe alivyosema, sasa ya nini nikutajie idadi ya madaktari ndugu yangu, kitu muhimu hapa ni kwamba hakuna athari kama inavyoelezwa huko mitaani, madaktari wote wanafanya kazi kwa moyo mmoja kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu,” Waziri alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment