ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 20, 2012

Umempoteza na unataka kumrudisha mikononi mwako?-2

Truth #387: Relationships Are Messy
..dondoo hizi zitakusaidia sana
BILA shaka mpo wazima wa afya njema na maisha yanaendelea. Kama ndivyo, vizuri sana. rafiki zangu, leo sina maneno mengi, hebu tuendelee kwenye mada yetu.
Yes! Nilianza wiki iliyopita, nilieleza kuwa, kurudiana na mwezi wako wa zamani si dhambi. Ni suala la moyo wako tu. Moyo ukiridhika, ukikuthibitishia kwamba bado unamhitaji mwenzako, ni jambo jema. Unaweza kuchukua uamuzi.
Hapa katika Let’s Talk About tunakubaliana na maamuzi ya moyo wako, lakini tunakupa dondoo zitakazokurahisishia kwanza kumpata, lakini pia kujua kama mwenzi wako huyo bado anaweza kuwa wako.

Rafiki zangu, kumbuka kwamba, unaweza kuwa na mwenzi wako, mkapendana kwa dhati na mkadumu kwa muda mrefu, lakini kwa bahati mbaya mkaachana kwa sababu ambazo mnazifahamu wenyewe.
Katika muda mfupi ambao utakuwa umeachana naye, anaweza kufanya mambo ya ajabu sana. Pamoja na kwamba moyo wako unamhitaji, lakini anaweza kuwa tayari ameshapoteza sifa za kuwa na wewe. Katika hali hiyo, ni sahihi kurudiana naye? Bila shaka jibu hapa ni siyo sahihi.
Wiki iliyopita tulianza kuangalia kama ni sahihi kurudi kwa mwenzi huyo, faida utakazopata kwa kurudiana naye, kuchunguza sehemu anayopatikana na kufuatilia historia yake baada ya kutengana kwenu.
Enheee! Sasa twende kwenye vipengele vingine. 

MAWASILIANO
Ukishachunguza mahali alipo na kuridhika na historia yake ya kimapenzi baada ya kuachana na wewe, sasa unatakiwa kutafuta mawasiliano yake. 
Kupata mawasiliano yake ni hatua ya kwanza, kitakachofuata baada ya hapo ni kujenga mawasiliano. Hapo sasa inategemea na namna mlivyoachana, lakini kama hamkuwa na ugomvi mkubwa sana, basi unaweza kumtumia meseji za kichokozi mara nyingi uwezavyo kwa siku.
Majibu yake ndiyo yatakayokupa mwanga wa kuendelea na kipengele kingine. Kikubwa hapa ni kutozungumzia kabisa mambo ya mapenzi, badala yake iwe ni kumjulia hali na utani wa hapa na pale.

MPE MWALIKO
Baada ya kutengeneza mawasiliano naye, sasa unatakiwa kumwalika katika shughuli mbalimbali za kifamilia na binafsi. Mathalani umepata mwaliko wa kwenda kwenye sherehe au hafla fupi ya usiku, omba kampani yake.
Kama mtu mzima atagundua kitu kilichopo moyoni mwako. Hata kama atakuwa mwenye moyo wenye kutu, kutoka naye mbele za watu, kutamfanya akumbuke enzi zenu mlipokuwa mkitoka pamoja, hivyo kufikiria kurudi tena kwako.
Ikiwa ataamua kukuambia kwamba anaona mrudiane litakuwa jambo zuri zaidi, maana atakuwa amekurahisishia, lakini akinyamaza, basi njia inayofuata hapa chini ni muafaka kwake.

MVUTE KARIBU YAKO
Sasa unatakiwa kumsogeza karibu zaidi na wewe. Lazima afahamu kwamba, kuna kitu fulani kipo ndani ya moyo wako. Meseji zako zibadilike, kama ulikuwa unamwandikia, “Vp uko poa?” au “Mambo yanaendaje?”,  sasa unatakiwa kubadilisha hadi “Niambie sweetie, uko poa?”
Meseji za aina hiyo zitamfanya aone tofauti na inawezekana kabisa akagundua kwamba upo kwenye mawindo ya kumrudisha tena kwako. Katika hatua hii katu hutakiwi kufungua mdomo wako kumwambia kuwa unataka kurudiana naye na badala yake unatakiwa kuacha vitendo vizungumze vyenyewe. 
Mada bado haijaisha, wiki ijayo itaendelea katika sehemu ya mwisho, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.

No comments: