Na Augustino (Tino) Malinda
Kwanza napongeza uamuzi wa serikali ya Rais Jakaya kikwete kukubali kufanya mabadiliko ya katiba ni jambo ambalo watawala wengi hawalipendi kwani katiba zinazowaweka madarakani ndizo katiba nzuri, kwa mujibu wa mitazamo yao katiba hizo hazipaswi kubadilishwa.
Lakini kwa raisi Kikwete kukubali inahitaji pongezi bila kuangalia utata ambao umezuka wa wabunge kukataa na bunge kuburuza muswada wa mabadiliko ya katiba, bado naita mwanzo mzuri kwani nia ni mabadiliko ya katiba.
Sasa wakati tunajiandaa kuijadili na kupata vipengele vya kuondolewa ama kutiliwa mkazo katika katiba ni vyema tukaangalia kwa undani mustakabari na mwenendo wanchi yetu hasa katika swala la ubunge na uongozi wa kuchaguliwa, nina mengi ambayo ningependa yafanyiwe mabadiliko ndani ya katiba lakini leo nataka niongelee jambo moja tu la UBUNGE NA UONGOZI WA KUTEULIWA.
Nimeamuwa kuliangalia suala hilo kutoka na matukio yaliyojili hivi karibuni katika vyama vyote vya siasa ,kuanzia CCM,CHADEMA,NCCR-MAGEUZI hadi TLP, kuhusu kutishiana hadi kufukuzana, CCM bado kufukuzana lakini walishawahi kutishiana na kumekuwa na kauli za kuelekea huko.
Labda tukumbushane tu yaliyojili CCM, wakati akiwa spika bwana Samuel Sitta alitishiwa kufukuzwa nasikia akamwangukia rais Kikwete amuokoe, juzi nilimsikia kiongozi mstaafu wa CCM akisema kuwa mafisadi wana nguvu kwakuwa wana vyeo na kama wakiondolewa katika vyeo hivyo nguvu zao zitakwisha na kumekuwa na misukumo ya dhati ya kutaka kuwaondoa baadhi ya viongozi ndani ya CCM kama wasipojiuzuru wenyewe.na kwa mujibu wa katiba iliyoko kama wakiondolewa/wakinyang’anywa uanachama ubunge nao kaputi.Naomba nieleweke sitetei ufisadi, na nasema kama kiongozi ni fisadi hafukuzwi chama anashitakiwa na sheria ya nchi inasema ukipatikana na makosa unapoteza uongozi.
CHADEMA walishafukuza wale madiwani wa Arusha ambao sasa si madiwani tena ingawa swala lao liko mahakamani lakini mwisho wake ni kuupoteza udiwani kwa mujibu wa katiba hii, NCCR-MAGEUZI nayo ina sakata la Kafulila na CUF bwana Hamad hawa wote kwa mujibu wa katiba hii wanaondoka tu, TLP ilishafanya vitu vyake kwa diwani wake wa kuteuliwa imemuondoa kwa kumpokonya uanachama.Hawa wote ni viongozi wa kuchaguliwa ukiondoa huyo wa TLP ambaye ameteuliwa.
Ukiangalia matukio hayo utaona kuwa uongozi wowote wa kuchaguliwa si ridhaa ya wananchi tena bali ni ridhaa ya chama ulichotumia kuombea uwakilishi na kuishi katika nafasi hiyo tunayoiita uwakilishi wa wananchi kutatokana na juhudi zako za kubusu pete za wakubwa wa chama lasivyo unaondoka.
Wakati Tanzania ilipokuwa ikipata msukumo wa kuingia katika vyama vingi kulikuwa na kiongozi mmoja anaitwa Christopher Mtikila alifungua mashitaka ya kutaka kuwe na mgombea huru kwani katiba ilikuwa ikisema mtanzania anahaki ya kugombea nafasi ya uongozi ingawa kulikuwa na sifa za umri. Nakumbuka kesi hiyo aliifungulia mkoani Dodoma na jaji wa mahakama kuu kanda ya Dodoma akampa ushindi. Wadau wengi na wanaharakati, wasomi na kila mtu akaona sasa mambo sio mabaya ugombea huru sasa tiki.
Kitendo hicho hakikuifurahisha CCM nakumbuka vizuri sana rais wa wakati huo Ali Hassan Mwinyi akaitisha kikao katika ukumbi wa bunge wakati huo ukiwa mjini Dar es Salaam katika jengo la Karimjee kutaka wabadilishe katika iwe mtanzania anahaki ya kugombea lakini kupitia chama, yaani waongeze setensi ya kupitia chama cha siasa.
Nikiwa pale bungeni nilipata fursa ya kuongea na mmoja wa wabunge ambaye alitokea kunipenda sana Dr Ngunangwa alikuwa mbunge wa Njombe.akanieleza azma ya mkutano huo na kwamba yeye amemuelewa vizuri rais Mwinyi na yuko tayali kumuunga mkono katika kukarabati hicho kifungu.
Kwa tashwishwi nikamuuliza hoja alizozipata ni zipi za kumfanya akubaliane na rais kukarabati kifungu hicho, akasema rais ametuasa kuwa kama tukiachia tuwe na mgombea huru itakuwa ngumu ukimshinda mtu katika kura za mwanzo ndani ya chama au akikushinda halafu kamati kuu ikikurudisha , yeye atatoka na kugombea kwa sera za CCM kama mgombea huru, na kwa kuwa atadai yeye ni mwana CCM hayuko upinzani, ndugu mtakuwa na hali ngumu, “unaona hilo kijana ndo maana naona kauli yake ina mantiki” akanieleza Dr Ngunangwa.
Baada ya kumsikiliza nilimuuliza sasa hilo ni kwajili ya nyie kuendelea kuwa wabunge na kuminya watu wengine au kwa ajili ya nchi, kumbuka haya hayakuwa mazungumzo ya habari za gazeti haya yalikuwa ya kama baba na mwana.
Nikamweleza Dr Ngunangwa hii sheria mnayopitisha kwa maslahi binafsi itawaumiza nyie , nikamuasa yeye kama mbunge atunge sheria kwa maslahi ya vizazi vijavyo na maslahi ya nchi na wala sio maslahi ya chama wala binafsi, mzee akashusha pumzi mi nikaondoka nilikosa amani sana kwa mstakabari wanchi kuamuliwa kwa maslahi binafsi. Kipengele kilifanyiwa ukarabati na wabunge wakapiga kura ya ndio kifungu cha mgombea binafsi kikafa kikazikwa.
Baada ya muda kidogo mama Ann Makinda akiwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma akaanza kukinyemelea kiti cha Dr Ngunangwa,mama Makinda akiwa na pesa lukuki alizotoka nazo akiwa waziri wa maendeleo ya kinamama na watoto jumlisha ukuu wa mkoa wa Ruvuma akaanza kugawa mazawadi zikiwemo baiskeri kwa viongozi wa CCM wa vijiji, kata, tarafa na wilaya katika jimbo la Dr Ngunangwa.
Dr Ngunangwa akawa na wakati mgumu akafoka na kuja na msamiati wa “ALIKWINA” yaani kwa kibena alikuwa wapi?, hiyo ikiwa ni kijembe kwa mama Makinda kwamba aliwaacha wabena siku zote sasa anataka ubunge ndo analeta mazawadi lakini ndugu kifo cha nyani miti yote inateleza Dr Ngunangwa akaangushwa na hakukuwa na nafasi ya mgombea huru ikabidi ajiunge na NCCR-MAGEUZI ya Mrema akaitwa mpinzani na wakati huo vijijini ukiiitwa mpinzani ni hukumu ya kifo cha kisiasa,unaonekana unapingana na rais Julius Nyerere, mzee akapoteza ubunge. Tulipoonana akasema kijana ulisema kweli.
Kwanini nakumbushia habari ya miaka mingi iliyopita, kama mwandishi na mwanahistoria ninaamini tunajirekebisha kutoka na matukio pita (past Events) na ninaogopa kwani ninavyoona kuna ukakika wa historia kujirudia kutokana na upitishwaji wa muswada wenyewe bungeni.
Tuangalie hata jinsi muswada ulivyopitishwa, ulipitishwa kiushabiki bila kuangalia na kuutafakari kwa makini, wakati wasomi na wanaharakati wakiomba ujadiliwe kwa kina na huku baadhi ya wabunge wakisusia vikao, wabunge wengine walikuwa wakiwapiga wenzao vijembe kama vile ni masuala ya chama na sio nchi.
Ni vyema wabunge wakatafakari kwani kina sheria hii ya viongozi wakuchaguliwa, kupoteza nafasi zao kwa kura ya turufu ya chama, kwani inawanyima haki wale waliomchagua ambao ni wengi kuliko wale wanaomfukuza.
Wote tunaelewa kuwa kura za mwanzo za vyama hazizidi hata elfu tatu mtu anashinda lakini kwenye uchaguzi mkuu mtu anachaguliwa kwa kura hata laki moja, ni vyema wabunge wakaliona hilo na viongozi wetu wakaacha ubinafsi na kuangalia maslahi ya nchi zaidi.
Wakati mwingine unaona wabunge wanashindwa kuikosoa sana serikali kwani anaweza akapoteza ubunge kwa kunyang’anywa uanachama, watu kama Nape Nnauye wanaweza kukalipia wabunge na wabunge nao wanashindwa kujibu mapigo kwani wanaweza kuula wa chuya.Sisemi kusiwe na nidhamu ndani ya chama hapana nataka nidhamu iwepo na maslahi ya nchi yaangaliwe.
Kama wabunge watakuwa huru na hata kama wakifukuzwa kwenye vyama wanabaki na ubunge wao itasaidia sana kuwafanya wawajibike zaidi kwa wananchi na kuifanya serikali iwajibike zaidi, lakini ikiwa ni kinyume tutaendelea kuwa na bunge la muhuri (rubber stamp).
Tuangalie yaliyowakuta wabunge wa zama za Dr Ngunangwa, basi na nyie mliopo madarakani sasa msitumbukie katika mtego huo, wakati wa muswada wa mabadiliko ya katiba ukija msisahau kuangalia na kupitisha la mgombea huru ili demokrasia na uwajibikaji uwe mzuri.
Aksante kwa leo mie kona ya diaspora naweka hoja.
No comments:
Post a Comment