ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 11, 2012

Wewe unaweza kuwa chanzo cha maumivu yako!-2

NAKUKARIBISHA kwa moyo mkunjufu kabisa katika safu yetu nzuri ya All About Love. Nina imani kubwa kuwa, kila siku umekuwa ukibadilika kifikra kutokana na mada unazosoma katika ukurasa huu.
Rafiki zangu, kama mtakumbuka wiki iliyopita nilianza kwa kuwaeleza mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kusababisha maumivu katika maisha yako. Kikubwa zaidi ambacho nilikizungumzia ni suala la hisia. Namna zinavyoweza kukuongoza vibaya na kufanya maamuzi ambayo mwisho yanakuwa na matokeo mabaya.
Ndugu zangu, unapojipa muda wa kujifunza vitu vipya, unaupa ubongo wako nafasi ya kuwa mpya katika mambo ya mapenzi. Kama ulikuwa unafahamu kitu fulani, basi unapata kingine kitakachokufanya uendelee kuwa bora zaidi katika uhusiano wako.
Hebu tujadili kwanza kuhusu hisia, wapo wanaongozwa nazo, mpenzi wake anaingia na kumtizama tu usoni, anagundua kuna tatizo fulani.
Ni sahihi? Ni kweli kwamba hisia huwa zinaongoza sawa au zinapotosha? Hapa katika All About Love utapata majibu yakinifu.

Ni nini hasa?
Hisia ni hali ya kuamini jambo la kufikirika kwa kufikiria. Hisia zinaweza kutumika lakini siyo kwa kila mtu, ambaye anaweza kutumia hisia kama njia ya kugundua usaliti au aina yoyote ya tatizo kutoka kwa mtu mwingine ni yule ambaye yupo karibu zaidi na mhusika.
Mathalani, kama unafanya kazi na rafiki yako, mpo ofisi moja, mnakwenda mgahawani pamoja, mpo karibu kwa kila kitu, wakati mwingine hata mnapokuwa katika mapumziko ya mwisho wa wiki huwa mnakuwa pamoja.
Mtu wa aina hii, akija na mabadiliko fulani lazima utamgundua tu. Upande wa pili ni kwa wapenzi (hasa wanaoishi pamoja), hawa ni rahisi kugundua mwenza anapobadilika. Ratiba zenu zote mnazijua, akiwa na furaha unajua na hata akiwa na msongo wa mawazo ni rahisi kugundua, hapa napo kuna uwezekano mkubwa wa kuogozwa na hisia. Kikubwa tunachoangalia hapa ni ukweli wa kile unachofikiria.
Ni kweli mwenzi wako ana matatizo? Je, si wewe labda ndiye mwenye matatizo? Kama ni yeye, umefanya nini kuhakikisha anakuwa vile upendavyo? Kwa namna yoyote, kama mwenzi wako ana matatizo ya kujirudiarudia na hatarishi katika maisha yako, ni lazima uchukue uamuzi sahihi.
Kila kitu katika mapenzi ni kuchagua rafiki zangu. Enheeee...hebu tuone unatakiwa kufanya nini baada ya kuhisi jambo fulani kwa mwenzi wako.

Fanya uchunguzi
Kabla ya kufanya chochote ni lazima ufanye uchunguzi kwanza. Unaweza kuhisi jambo fulani kumbe haipo hivyo, huenda ana mabadiliko mengine ya kawaida ambayo yamemchanganya ofisini kwake au kwa marafiki zake.
Mathalani mpenzi wako amekuja, anaonekana amechoka-choka, hana furaha na uso si muangavu kabisa! Tabasamu lake halipo na kwa kumwangalia tu usoni unagundua kwamba ana alama ya busu kwenye shavu lake! Wakati mwingine mwingine ananukia manukato ambayo siyo aliyoyatumia mlipoachana. Hapo kuna tatizo.
Au anaweza kuja na furaha kupitiliza, uchangamfu kupitiliza, kukumbatia kwa muda mrefu zaidi kuliko kawaida ambavyo mmezoeana n.k.
Katika hali kama hiyo lazima uwe na mashaka na inawezekana kabisa akawa ametoka kwa mtu mwingine. Lakini je, unatakiwa kuwa mkali kwake na kuleta ugomvi baada ya kuona dalili hizo? Hapana.....! Kipo kitu unachotakiwa kufanya, unakijua? Soma hapa chini.

Endelea kuchunguza zaidi
Unatakiwa kwenda mbali zaidi ya hisia zako za kawaida zinavyokutuma, mchunguze! Awe mpole sana au mkali sana, lakini unatakiwa kumwambia akae chini na awe makini kukusikiliza! Anza na sentesi hii: “Unajua mimi nina akili sana kuliko unavyofikiria...ukifanya jambo lolote lazima nitajua....” ukifika hapo nyamaza kimya, kisha macho yako yatulize katikati ya macho yake bila kupepesa. Utajifunza kitu.
Kama alifanya usaliti au alikuwa na mpenzi mwingine muda mfupi uliopita utajua tu. Uwoga wake, upole zaidi na kutoa macho sana au kuangalia chini kwa aibu ni tiketi yako ya kuelekea kwenye kuujua ukweli zaidi ambao anajaribu kukuficha.
Usiishie hapo, mnuse kama aina ya vipodozi anavyotumia siku zote ndiyo vile vile. Ni rahisi tu kugundua, maana wengi wao baada ya kumaliza kufanya mapenzi huingia bafuni, huko atakutana na sabuni nyigine, akitoka atatumia mafuta mengine na hata manukato mengine. Lazima utaujua ukweli.

Amua mwenyewe
Hisia zinaweza kukuongoza sawa na wakati mwingine kukuangusha, sasa unachotakiwa kufanya zaidi ni wewe kuwa mwangalifu kabla ya kuchukua hatua. Ikiwa baada ya kupitia vipengele vyote hivyo na kugundua ni kweli penzi lako linasalitiwa, ni wakati wako wa kufanya uamuzi sahihi.
Uamuzi wa kwanza ambao ni sahihi zaidi ni kuzungumza naye, mweleze hali ilivyo mbaya na jinsi mnavyokuwa katika hatari ya kuelekea kwenye matatizo.
Kosa hili kama siyo mara ya kwanza litakuwa ni kubwa sana katika uhusiano wenu lakini anayejua thamani ya penzi lenu na jinsi mlivyokutana ni wewe mwenyewe, hivyo basi uamuzi wa kuachana au kuendelea naye upo mikononi mwako.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.

1 comment:

Anonymous said...

Kumekucha, na Mpwa nae anaandika mambo haya.mmmmm//?