ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Rais Jakaya Kikwete alilipenda jengo analodaiwa kusababisha hasara katika ununuzi wake.
Akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili ya uhujumu uchumi na kuipatia Serikali hasara ya Sh bilioni mbili pamoja na Ofisa Mwandamizi wa Ubalozi huo Grace Martin, Mahalu alisema kuwa Rais Kikwete akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alitembelea jengo hilo na kuliona.
Alisema Desemba 2001, Rais Kikwete alienda kwenye mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) mjini Roma, Italia na ubalozi wa nchi hiyo ulifanya mipango akalione jengo hilo na alipoliona aliridhishwa nalo, na katika mazungumzo na mmiliki wake alisifia sana jengo hilo ni zuri na linafaa.
“Wakiwa kwenye maongezi na mwenye nyumba alisifia jengo hilo na pia aliwapa mualiko wa kutembelea Ngorongoro,” alisema na kuongeza kuwa aliwaahidi mara atakapofika nchini atashughulikia fedha za malipo ya awali zinazotakiwa kulipwa.
Hata hivyo Rais Kikwete aliuliza kwanini kuna mikataba miwili katika ununuzi wa nyumba hiyo na alijibiwa kuwa huo ni utaratibu wa nchi ya Italia.
Alisema baada ya mazungumzo hayo akiwa njiani alimpigia simu Katibu Mkuu wa Wizara yake kumueleza kuwa wafanye mchakato wa kutuma fedha inayotakiwa kwa malipo ya awali dola milioni moja kabla mwaka huo haujaisha na pia alimuagiza Mahalu akafatilie fedha hizo za malipo hapa nchini.
Awali Mahalu alizitoa mahakamani barua mbalimbali ambazo ni za mawasiliano kati ya ubalozi wake na serikali kuanzia mwanzo wa uchaguzi wa nyumba hizo ambapo awali zilipendekezwa tatu na baadaye wakakubaliana kuinunua hiyo iliyonunuliwa.
Katika barua hizo alizozitambua Mahalu akiongozwa na Wakili wake Alex Mgongolwa na Mabere Marando, alidai Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na ya Mambo ya Nje ilikuwa ikimpa maelekezo mbalimbali kuhusiana na ununuzi wa jengo hilo na kabla mtathmini kutoka serikalini alikwenda Roma kukagua jengo na kuridhishwa nalo.
Mahalu na Martin wanadaiwa Septemba 23, 2002 katika Ubalozi wa Tanzania jijini Rome, Italia, kwa nia ya kumdanganya mwajiri wao, walighushi hundi ya malipo namba D2/9 yenye maelezo ya kununua jengo kwa Euro 3,098,741.58. ilidaiwa kuwa Oktoba mosi, 2002 wakiwa waajiriwa wa Serikali ya Tanzania walitumia mkataba wa mauzo ukiwa na maelezo ya kughushi.
Ilidaiwa Oktoba mosi, 2002, washitakiwa wakiwa katika Ubalozi wa Tanzania walitumia hati hizo kuonesha kuwa mmiliki wa jengo alipokea Euro 3,098,741.58.
Katika shitaka la tano, ilidaiwa kuwa washitakiwa walifanya hivyo kwa nia ya kuipotosha Serikali ya Tanzania. Pia wanadaiwa kuiba Euro 2,065,827.60 kwa kutumia vyeo na nafasi za ajira walizokuwa nazo.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake