ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 1, 2012

Nahodha Twiga Stars asaini miaka miwili Uturuki

Beki wa kati na nahodha wa timu ya soka ya taifa ya wanawake maarufu Twiga Stars, Sophia Mwasikili
Beki wa kati na nahodha wa timu ya soka ya taifa ya wanawake maarufu Twiga Stars, Sophia Mwasikili, ambaye aliondoka nchini juzi alfajiri kuelekea Uturuki kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa, amesaini mkataba wa miaka miwili na klabu ya huko.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa Mwasikili, ambaye alikuwa akiichezea timu ya Sayari Women, amejiunga na klabu ya Luleburgazgucu Spor Kulubu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Wanawake nchini humo.
Alisema kwamba timu hiyo ilikuwa inamuhitaji Mwasikili kwa muda mrefu lakini TFF ilimuombea ruhusa ili aweze kuitumikia nchi yake katika mechi ya marudiano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Twiga Stars na Namibia (Brave Gladiators) ambayo ilichezwa Jumapili na kuibuka na ushindi mnono wa magoli 5-2.
"Ameshasaini mkataba wa miaka miwili na hivyo akifika huko anaanza kuichezean timu hiyo moja kwa moja na si kufanyiwa majaribio," aliongeza Wambura.
Kabla ya kuondoka nchini, Mwasikili, aliliambia gazeti hili kwamba amefurahi kupata timu nje ya nchi na matunda ya kujituma kwao yameanza kuonekana.
Alisema kuwa ushiriki wao wa fainali zilizopita za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini mwaka 2010 kuliwasaidia kuwavutia makocha wa timu mbalimbali.
"Hasa ile mechi tuliyocheza na Nigeria, tulifungwa lakini kazi haikuwa rahisi kwa mabingwa hao wa wanawake kupata magoli kirahisi, naamini nimeanza na wenzangu watafuata," alisema beki huyo.
Mbali na Mwasikili, mshambuliaji, Asha Rashid 'Mwalala' naye huenda akaenda nchini humo kwa mara ya pili baada ya safari yake ya awali kushindwa kufikia makubaliano na klabu iliyomuita.
Mchezaji mwingine wa kike wa Tanzania aliyewahi kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ni Esther Chabruma 'Lunyamila' lakini sasa amerejea nchini na hayuko kwenye kikosi cha Twiga Stars.
Twiga Stars itavaana na wapinzani wao Ethiopia katika mchezo wa raundi ya kwanza ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Mei 25 na 27 jijini Addis Ababa.
Twiga Stars ambayo ilishiriki fainali za Mataifa ya Afrika zilizopita ilisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa magoli 7-2 dhidi ya Namibia, wakati Ethiopia iliyopoteza mchezo wa kwanza jijini Cairo kwa kufungwa 4-2, iliwatoa Misri baada ya kuwapa kichapo cha 4-0 na hivyo kuwafungisha virago kwa jumla ya magoli 6-4.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa Twiga Stars watarejeana na Ethiopia kwenye Uwanja wa Taifa Juni 17.
Wambura alisema kuwa kabla ya wawakilishi hao wa Tanzania hawajakutana na Ethiopia, wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Zambia itakayochezwa mwezi Aprili.
"Hayo ndiyo mapendekezo ya mwalimu na taratibu za kusaka mechi hiyo ya kirafiki zimeanza, itaingia kambini mapema kujiandaa na mchezo huo muhimu," alisema Wambura.
Alisema pia TFF inawashukuru wadau wote wa soka nchini walioshiriki katika maandalizi ya mechi ya Twiga dhidi ya Namibia na wote waliojitokeza uwanjani kuwashangilia.
Timu nyingine zilizosonga mbele kwenye mashindano hayo ni pamoja na Ivory Coast, Ghana, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia.
Nchi nane ndio zitashiriki fainali hizo zijazo zitakazofanyika baadaye mwezi Novemba mwaka huu na ambapo mabingwa watetezi wa mashindano hayo ni Nigeria.
CHANZO: NIPASHE

No comments: