ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 20, 2012

Papic awatetea Mwape, Asamoah

Kocha Kostadin Papic wa Yanga



Kocha Kostadin Papic wa Yanga amewatetea washambuliaji wake Davis Mwape na Kenneth Asamoah waliokosa mabao mengi ya wazi katika mechi yao ya awali ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri iliyomalizika kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Papic ambaye ni raia wa Serbia, alisema kwamba washambuliaji wake hao wa kimataifa, Mzambia Mwape na Mghana Asamoah, wamekuwa wakicheza kwa ushirikiano mkubwa katika Ligi Kuu ya Bara na kufanya vizuri; hivyo Wanayanga wanapaswa kujua kuwa hali iliyowakuta juzi, ya kukosa mabao katika maeneo ambayo huwa wanafunga, wakati mwingine hutokea kwenye mchezo wa soka.
     
Hadi sasa, Asamoah ndiye kinara wa upachikaji mabao katika timu ya Yanga na pia anakabana koo na John Bocco wa Azam kileleni mwa orodha ya wafungaji wanaoongoza katika ligi ya Bara.
"Hali kama hii ( ya kukosa mabao) hutokea katika kwenye mchezo wa soka, hawa ni washambuliaji waliochezaji pamoja katika mechi nyingi za ligi na ndio sababu ya kuwaanzisha kwa pamoja. Walipata nafasi za kufunga, wakashindwa. Ni makosa ya kawaida, hawapaswi kutupiwa mzigo, bali sote tunatakiwa kuyafanyia kazi kwa pamoja," alisema Papic.
Papic aliongeza kuwa hivi sasa, yeye, wachezaji wake na Wanayanga wote wanapaswa kusahau mchezo uliopita na kuelekeza nguvu kwenye maandalizi yao ya mechi ya marudiano watakayocheza jijini Cairo, Misri; ambako hakutakuwa na mashabiki kwa vile Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) linahofia hali ya usalama baada ya kuuawa kwa mashabiki 74 na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mechi ya ligi kuu kati ya Al Masry na Al Ahly mjini Port Said.
Katika hatua nyingine, Papic amesema kuwa licha ya kutopata ushindi katika mechi yao ya nyumbani, bado hawajakata tamaa na watacheza kwa uwezo wao wote ili kuhakikisha kuwa wanasonga mbele.
Akieleza zaidi, Papic alisema kuwa kikosi chake kilizidiwa uzoefu katika mechi hiyo na kwamba, pamoja na matokeo hayo, wana imani kuwa watawaduwaza Zamalek kwa kuwang’oa.
"Siku zote mimi huwa sio mtu wa kukata tamaa, ijapokuwa matokeo haya si mazuri kwetu, lakini hayajanikatisha tamaa... tutakwenda kwao (Misri) kupambana," alisema Papic.
Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha klabu kadhaa kubwa barani zikiwemo Kaizer Chiefs na Orlando Pirates za Afrika Kusini na Enyimba na Enugu za Nigeria, alisema kuwa ana uzoefu wa kutosha wa kukabiliana na timu kubwa za soka Afrika na hivyo anajua namna atakavyowaandaa wachezaji wake kuhakikisha kuwa katika marudiano wanaonyesha mara mbili zaidi ya kiwango walichocheza juzi.
Papic aliwasifu wachezaji wake, hasa wa viungo kutokana na namna walivyounganisha timu na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini wakaangushwa na umaliziaji mbaya.
Yanga wanatarajiwa kurudiana na Zamalek jijini Cairo kati ya Machi 2, 3 na 4 ambapo mshindi atasonga mbele kwa hatua inayofuata
CHANZO: NIPASHE

No comments: