NIANZE kwa kuwasalimu marafiki wote ambao siku ya jana tumesherehekea vema Sikukuu ya Wapendanao, Valentine Day. Natumaini wote hamjambo na mnaendelea na ujenzi wa taifa. Ni jambo la busara sana kuishi katika upendo, kwani bila upendo hakuna maelewano miongoni mwa marafiki.
Siku zote upendo unatakiwa kudumishwa katika ngazi tofauti, iwe ni baba kwa mama, watoto kwa baba na mama, familia kwa familia nyingine na hata jamii nzima kiujumla.
Siku zote upendo unatakiwa kudumishwa katika ngazi tofauti, iwe ni baba kwa mama, watoto kwa baba na mama, familia kwa familia nyingine na hata jamii nzima kiujumla.
Siku ya jana ni muhimu pia endapo tumeitumia kutatua migogoro tuliyokuwa nayo awali. Anza sasa ukurasa mpya wa mapenzi tena kwa vitendo. Iweke siku ya jana katika historia na uikumbuke kama ishara ya kutotoka tena nje ya mstari kwa kujifanyia tathmini juu ya pale ulipoteleza ili usiteleze tena.
Safu yetu maridhawa, Lets Talk About Love, inatambua vema marafiki waliodumisha zaidi mapenzi yao kupitia Sikukuu ya Wapendanao. Kwa wewe ambaye bahati mbaya imekupita ukiwa katika migogoro na umpendae, basi chukulia ni kama changamoto za mapenzi na darasa letu la leo litakujenga ili urudi katika mstari endapo tu utaweka utulivu katika siri hizi za kufurahisha mapenzi.
Wiki iliyopita tuliishia katika kipengele cha 13 kwa wale marafiki ambao wanajiandaa kuingia katika ndoa. Hivyo basi, leo tutamalizia kipengele cha 14 kisha tutaingia katika sehemu (b) inayowahusu zaidi wanandoa. Tabasamu lako linahitajika na usikivu utakufanya ujifunze siri usizozijua na ufurahie mapenzi yako.
14. JADILINI KUHUSU NDOA
Hii ni hatua ya muhimu kabisa katika kuelekea kwenye ndoa. Mnapaswa kuijadili ndoa yenu ni ya namna gani? Kama imani zenu zimetofautiana, nini kifanyike? Pindi mtakapojadiliana, mtaweza kupata muafaka juu ya ndoa ambayo ni sahihi kwenu.
Ndugu yangu, usilazimishe kumbadilisha mwenzako akufuate katika imani yako kama yeye hataki au pengine kuna vipingamizi katika familia yao. Kila mmoja wenu anapaswa kuweka hoja mezani na mnazijadili kwa mapana yake na mwisho muafaka utapatikana, mtaoana.
Hakuna kinachoshindikana katika majadiliano, tumia lugha nzuri kumshauri mwenzako ili ajue unamjali hivyo ni rahisi kuridhia ulichomshauri. Ieleweke tu ndoa yoyote mtakayokubaliana kupitia majadiliano yenu, basi itadumu kuliko mkitumia njia ya kulazimishana.
(b) Kwa wanandoa hapa sasa mnisome kwa makini maana wengi wamekuwa wakifeli katika hatua hii kutokana na kujisahau. Mikikimikiki ya maisha inapoibuka inaweza kuwafanya kila mmoja wenu akawa na maamuzi yake katika maisha hata kama mwanzoni (kabla ya ndoa) dhamira yenu ilikuwa njema.
Siku ya leo, Lets Talk About Love itakumegea vipengele sita ambavyo kimsingi ukivisoma kwa makini itakuwa ni dozi sahihi kama mwanandoa kuweza kujua siri hizi muhimu za kufurahia mapenzi yenu na nikushauri kuitumia kila siku.
15. WEKENI MIPANGO PAMOJA
Wanandoa wengi wamekuwa wakijisahau pindi wanapokuwa ndani ya ndoa. Inawezekana awali walikuwa na mikakati mizuri lakini baadaye mmoja wao huanza kujiamulia bila kumshirikisha mwenzake. Tatizo hili lipo zaidi kwa wanaume, mfumo dume unachukua mkondo wake. Utakuta mwanaume anafanya maamuzi peke yake akiamini yeye ndiyo kila kitu.
Jeuri hii inakuja hasa pale mwanaume anapoamini kuwa yeye ndiyo chanzo cha fedha wanayotaka kufanyia kitu fulani. Ataamua bila kumshirikisha mkewe kwa kuwa fedha anakuwa nazo yeye bila kujua mipango yote inapaswa kuzungumzwa pamoja kabla ya kufanya maamuzi.
Ndoa ni makubaliano baina ya watu wawili hivyo basi, katika kila jambo la maendeleo litafanikiwa pale tu mtakapolipanga pamoja. Ndugu yangu, acha kujiona wewe ni zaidi katika ndoa kutokana na kipato ulichonacho. Fedha si lolote si chochote katika maisha ya ndoa. Fedha zisibadilishe maamuzi ya mipango yenu, kila mnachotaka kukifanya basi mkifanye pamoja.
16. TUMIA MAJADILIANO ZAIDI
Yamkini wote wawili mlifanya majadiliano kabla ya kufikia maamuzi ya ndoa, basi ni wajibu wenu kuishi katika majadiliano kila siku. Wapo watu wasiopenda kuona ndoa za watu zinakuwa na furaha. Wataingilia na kuwafanya mgombane. Inawezekana pia mkapishana kauli katika mazungumzo, busara huhitajika.
Kutofautiana kwa kauli pamoja na vitu vingine, vinaweza kumalizwa kwa njia ya majadiliano. Jadilini katika lugha nzuri itakayomfanya mwenzio aone thamani yake.
Mkijadili yote kwa uyakinifu, mwisho mtagundua kumbe kilichokuwa kinawatatiza ni kitu kidogo ambacho hakikuhitaji nguvu kubwa kukitatua. Mnapojadiliana ni rahisi pia kutambua kosa lilikuwa wapi au lilisababishwa na nani, hivyo ni rahisi kumuepuka.
17. PALIZI YA NDOA
Kama ilivyo kwa mazao yakiwa shambani yanavyohitaji kupaliliwa ili yaweze kushamiri, vivyo hivyo katika ndoa. Ndoa inapaswa kupaliliwa kila siku. Jaribu kila wakati kusoma alama za nyakati, vitu gani anavipenda mwenzako basi umfanyie kila wakati.
Mfano unaweza kupanga siku moja katika wiki ukamchukua mkeo au mumeo na kumtoa nje kimatembezi. Ndoa hupaliliwa na vitu kama hivyo. Zawadi za hapa na pale zisipungue, acha kuishi kwa mazoea eti kwa kuwa tayari ni mkeo au tayari ni mumeo.
Unapoipalilia ndoa katika staili za zawadi, mitoko na vitu vingine huifanya ionekane mpya kila siku. Mnunulie mkeo au mumeo vazi unaloona linaendana na wakati mlionao.
Rafiki yangu nilitamani kumalizia vipengele vitatu kama nilivyokuahidi, lakini nafasi yangu hainiruhusu, basi tukunane wiki ijayo Mungu akipenda. USIKOSE!
Joseph Shalua ni mtaalam wa mambo ya mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Lets Talk About Love na Who is your Valentine? Ambacho ni maalumu kwa siku ya wapendanao.
No comments:
Post a Comment