Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, 'ilijinyima' ushindi baada ya kushindwa kutumia nafasi kadhaa ilizopata katika sare ya 0-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Mshambuliaji anayeongoza kwa magoli katika ligi kuu ya Tanzania Bara, John Bocco 'Adebayor', alipoteza nafasi mbili nzuri za kufunga kwa kichwa wakati aliposhindwa kulenga lango. Krosi ya nahodha Shadrack Nsajigwa ilitua vyema kichwani mwa Bocco katika dakika ya 15 lakini mshambuliaji huyo mrefu alilenga nje ya lango na angeweza kufunga goli tamu la kichwa cha mbizi katika dakika ya 65 kama angeruka ipaswavyo ili kuifikia krosi safi ya mchezaji mwenzake wa klabu ya Azam, Abdi Kassim.
Aliishia kuuparaza badala ya kuupiga kichwa mpira huo ulioenda kutoka pembeni ya lango akiwa mbele ya kipa Kidiaba Muteba.
Nyota wa DRC ambaye alipata kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Arsenal ya Uingereza, Tresor Mputu, alionyesha sehemu ya cheche zake katikati ya dimba na kipa mwenye vituko Kidiaba alipiga magoti na kunyoosha mikono juu kuomba dua kabla ya kipindi cha pili kuanza, lakini hapakuwa na matukio mengi katika mechi hiyo ya kirafiki ambayo haikupata mahudhurio makubwa.
Kipa anayeng'aa Azam, Mwadini Ali, alipangwa kwa mara ya kwanza Stars wakati alipoingia kutokea benchi kuchukua nafasi ya kipa chaguo la kwanza Juma Kaseja katika kipindi cha pili huku mshambuliaji Mzanzibari anayecheza soka la kulipwa nchini Misri, Ally Badru, ambaye aliripotiwa kuwa asingeweza kuwahi mechi hiyo kutokana na kunyimwa ruhusa ya mapema na klabu yake, alikuwa katika benchi la wachezaji wa akiba.
Stars ilikuwa ikiitumia mechi ya jana kwa ajili ya maandalizi ya kuikabili Msumbiji Februari 29 katika mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2013.
Vikosi vilikuwa; Stars: Juma Kaseja/ Mwadini Ali (dk.46), Shadrack Nsajigwa/ Said Nassoro (dk.46), Stephano Mwasika, Aggrey Morris, Juma Nyosso, Shabani Nditi, Hussein Javu/Nsa Job (dk. 46), Mwinyi Kazimoto/ Jonas Gerard (dk. 67), John Bocco, Abdi Kassim na Mrisho Ngassa/ Uhuru Selemani (dk.46).
DRC: Bolongo/ Kidiaba Muteba (dk. 46), Issama Mpeko, Kasusula Kilisho, Mampuya, Kimwaki Joel, Mutombo, Lema Mabidi, Tresor Mputu/ Emomo Ngoy (dk.75), Deo Kanda, Ilunga/ Botayi (dk.65) na Angai Kayiba.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake