Sweetbert LukongeUWANJA wa Jeshi wa Arab Contractors jijini Cairo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 22,000, ndio utakaokuwa mwenyeji wa mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Zamalek dhidi ya Yanga hapo Machi tatu.
Utata kuhusu wapi itakapochezwa mechi hiyo ya marudiano ilitokana na vurugu zilizotokea Misri kwenye uwanja wa Port Said na kusababisha watu 74 kupoteza maisha wakati wa mechi ya Ligi Kuu nchini humo kati ya Ahly dhidi ya Al Masry.
Kutokana na hali hiyo Zamalek walisema kama serikali itashikiria uamuzi wa kuzuia mechi za soka kuchezwa nchini Misri watalazimika kucheza mechi yao ya marudiano na Yanga nje katika nchi ya Algeria au Sudan.
“Tunatumaini tutafahamu vizuri kuhusu hali ya usalama hapa na kama serikali itatupa ruhusu ya kucheza mchezo wetu hapa au laa,” alisema msemaji wa Zamalek, Ali Aboul-Naga Said.
Zamalek imepokea maombi kutoka klabu ya Algeria, ES Setif na Hilal ya Sudan kuwa wenyeji wa miamba hiyo ya Cairo inayopewa nafasi ya kusonga mbele baada ya kupata sare ya 1-1 ugenini Jumamosi iliyopita.
Lakini, jana serikali ya kijeshi ya Misri ilitoa ruksa kwa Zamalek kucheza mechi hiyo nyumbani kwenye uwanja wa chuo cha jeshi uliojengwa mwaka 1989 kwa lengo la kutumika kwa michezo ya majeshi pekee ukiwa kwenye Mtaa wa Onouba kaskazini mwa jiji la Cairo umbali wa maili 7 kutoka uwanja wa kimataifa wa Cairo.
Baadhi ya wachezaji wa Yanga wamesema wapo tayari kukabiliana na Zamalek katika nchi yoyote kwenye mchezo wao wa marudio.
Akizungumza na Mwananchi jana kiungo mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima alisema tupo tayari kucheza na Zamalek sehemu yoyote ile itakayopangwa na CAF.
"Jambo kubwa ni usalama wetu hata kama utachezwa jijini Cairo, sisi tupo tayari kupigana kwa ajili ya kuhakikisha tunasonga mbele katika mashindano hayo," alisema Niyonzima.
Naye beki wa kushoto wa timu hiyo, Oscar Joshua alisema kuwa hivi sasa wanajifua zaidi kwa ajili ya mechi hiyo na wapo tayari kucheza sehemu yoyote ile.
"Kila mmoja wetu hivi sasa anajifua kwa ajili ya mechi yetu ya marudiano ikiwa ni pamoja na zile za Ligi Kuu, jambo la muhimu kama tutacheza Misri ni usalama wetu kwanza," alisema Joshua.
Mechi hiyo itachezwa bila ya mashabiki kutokana na Shirikisho la Soka Afrika, CAF kuwafungia mashabiki wa Zamalek kutokana na vurugu walizofanya kwenye mchezo dhidi ya Club Africain ya Tunisia uliofanyika mwaka jana kwenye uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
Zamalek ilitwaa ubingwa mara ya mwisho wa Afrika mwaka 2002, wiki iliyopita ili nusurika kipigo baada ya kupata sare ya 1-1 na Yanga kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Zamalek wanategemea kurejea kwa wachezaji wake majeruhi katika mchezo huo kutawafaidia watapocheza dhidi ya Yanga hapo Cairo.
“Kocha Hassan Shehata amekuwa akifanya kazi ya kuwatengeneza wachezaji wote waliokosa kwenye mchezo wa kwanza waliotoka sare ya 1-1 kutokana na kuwa majeruhi,” alisema kocha msaidizi Osama Nabih.
“Benchi la ufundi wanajua ubora na udhaifu wa Yanga na wanafanyia kazi suala hilo ili kuufanya mchezo wa Machi 3 kuwa rahisi,” aliongeza Nabih, akizungumzia kupona kwa viungo wake Mahmud Abdel-Razik “Shikabala” na Ahmed Hassan.
Washambuliaji Amr Zaki na Ahmed Hossam “Mido,” ambao kwa sasa wapo kwenye viwango vya juu wanategemewa kutoa mchango muhimu kwao.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake